Habari Mseto

Tutazidi kuanika washukiwa mitandaoni, DCI yaambia korti

May 8th, 2019 1 min read

Na VALENTINE OBARA

IDARA ya Upelelezi wa Jinai (DCI) imelalamika kuhusu agizo lililotolewa na mahakama kuizuia kusambaza picha za washukiwa wa uhalifu wanaokamatwa, katika mitandao ya kijamii.

Mwishoni mwa mwaka uliopita, Jaji wa Mahakama Kuu Wilfrida Okwany alitoa agizo la muda kuzuia DCI kusambaza picha aina hizo hasa katika mitandao ya Facebook na Twitter.

Agizo hilo lililotolewa baada ya malalamishi kuwasilishwa kortini na Bw Henry Shitanda litadumu hadi wakati kesi itakapoamuliwa.

Mlalamishi alikuwa amedai usambazaji wa picha za washukiwa ambao hawajahukumiwa wala kesi zao kuanza kusikilizwa ni ukiukaji wa sheria na haki zao kwani hatua hiyo huwasababishia aibu kubwa katika jamii.

Lakini idara hiyo ya upelelezi inayosimamiwa na Bw George Kinoti, sasa imejitokeza kupuuzilia mbali agizo hilo na kudai uchapishaji wa picha za washukiwa wanapokamatwa ni mtindo unaoruhusiwa kimataifa kama mojawapo ya mbinu za kupambana na uhalifu.

Zaidi ya hayo, DCI ilisema kwenye taarifa kwamba ina jukumu la kikatiba kupasha habari muhimu kwa umma ikiwemo kuhusu washukiwa wa uhalifu.

“Tulipokuwa tukiwaza na kuwazua kuhusu jinsi tutakavyotii maagizo ya korti, tulitambua DCI ilibaguliwa kwani vyombo vingine vya habari ikiwemo magazeti na vya kielektroniki ambavyo hutegemewa na umma husambaza mambo sawa na haya ilhali hakuna wakati tumesikia vikizuiliwa kufanya hivyo,” idara hiyo ikaeleza.

Kwa mujibu wa DCI, usambazaji wa picha ni mbinu ambayo hutumiwa na polisi kote ulimwenguni kusaidia kutafuta washukiwa wanapotoroka au kuonya wananchi kuhusu wahalifu hatari kuanzia wakati wanapokamatwa.