Hasira orodha ya mwisho ya kuwania tuzo ya fasihi ya Kiswahili ikijumuisha Watanzania pekee

Hasira orodha ya mwisho ya kuwania tuzo ya fasihi ya Kiswahili ikijumuisha Watanzania pekee

Na MARY WANGARI

HISIA kali zimeibuka baada ya orodha ya mwisho ya washindi katika tuzo ya uandishi wa fasihi ya Kiswahili kujumuisha Watanzania pekee.

Licha ya jopo la majaji kupokea jumla ya mawasilisho 256 kutoka kwa waandishi mbalimbali kote duniani ikiwemo Kenya, ni waandishi kutoka Tanzania pekee walioteuliwa katika tuzo hiyo ya Mabati-Cornell Kiswahili Prize for African Literature.

Kinaya ni kuwa, shindano hilo linalojumuisha tanzu tatu za fasihi andishi ya Kiswahili: Riwaya, Ushairi na Tamthilia, linadhamaminiwa na kampuni ya Kenya, Mabati Rolling Mills (MRM).

Isitoshe, malalamishi zaidi yaliibuka baada ya kubainika kuwa orodha ya mwisho ya washindi watakaotuzwa Januari 27, 2022, jijini Dar es Salaam, Tanzania, inajumuisha wanaume pekee hivyo kuzua maswali kuhusu uwakilishaji wa kijinsia.

Katika kitengo cha Riwaya, ni waandishi watatu, wote kutoka Tanzania, walioteuliwa wakiwemo Halfani Sudy (Kirusi Kipya), Lucas Lubango (Bweni la Wasichana) na Hafi Athumani (Kanzu ya Ukubwa).

Mohamed Omar Juma (Chemichemi ya Jangwani) Msusa Mohamedi (Malenga wa Masasi) na Mfaume Hamisi Mfaume (Sinaye Baba), wote kutoka Tanzania vilevile, waliteuliwa katika Kitengo cha Ushairi.

Mbwana Kidato Mtanzania anayeishi Afrika Kusini ndiye pekee aliyeteuliwa katika kitengo cha Tamthilia kupitia mkusanyiko wake wa hadithi fupi (Sinaubi).

Akitangaza orodha hiyo Alhamisi, Desemba 2, katika hafla iliyoandaliwa Sarova Stanley, Nairobi, Mwenyekiti wa Bodi ya Mabati-Cornell inayoandaa Tuzo hiyo, Abdilatif Abdalla alifichua kuwa mshindi atakayetwaa nambari moja atatuzwa Sh500,000 huku wa pili akituzwa Sh250,000.

Shindano la mwaka huu lilivutia idadi kubwa zaidi ya waandishi wa fasihi ya Kiafrika kuliko ilivyowahi kushuhudiwa tangu Tuzo hiyo ilipoanzishwa 2014.

“Tulipokea jumla ya mawasilisho 256, idadi ya juu zaidi kuwahi kushuhudiwa katika tuzo hili, kutoka kwa waandishi kote duniani ikiwemo Ujerumani, Canada, Australia na kwingineko. Tuna furaha kuwa waandishi zaidi wanajitokeza na viwango vyao vya uandishi vinazidi kuimarika,” alisema Bw Abdalla.

Hata hivyo, matokeo hayo yameibua hisia kali hasa miongoni mwa waandishi wa fasihi nchini Kenya wanaohisi mashindani hayo yamekuwa na ubaguzi.

Akizungumza na Taifa Leo, Bw Ramadhan Abdallah Savonge mmoja wa walioshiriki tuzo hiyo 2019 na mwaka huu vilevile katika uandishi wa kibunifu na ushairi, alieleza kukereka kwake.

“Imeniudhi sana. Ni kwamba mawasilisho ya Wakenya yalipotelea njiani au vipi? Ina maana hakuna Mkenya hata mmoja angeweza kutwaa nafasi ya pili bora au inayokaribia hapo. Ninahisi sitawahi kushiriki tena. Tuzo hii ifutiliwe mbali iwe Tuzo ya Waandishi wa Fasihi Tanzania badala ya Afrika Mashariki. Wakenya tuanzishe shindano letu,”

“Ikiwa sisi Wakenya tulio na ufahamu wa lugha tunafanyiwa hivi vipi kuhusu wenzetu wa Uganda na Congo ambao wangependa kushiriki shindano hili? Si itawavunja moyo kabisa!”alihoji Bw Abdallah.

Bw John Wanyonyi, mshindi aliyetwaa nafasi ya pili katika kitengo cha Riwaya 2019, ambaye pia ni mhariri wa kazi za fasihi, alisema kuwa waandishi wa Kenya wana usanifu wa kiwango cha juu hivyo basi matokeo hayo hayakusawiri usawa.

You can share this post!

Kipchoge, Chepng’etich watoka bure tuzo ya mwanariadha...

Kenya yakabiliwa na kibarua kigumu dhidi ya Misri kutafuta...

T L