TUZO ZA EPL: Beki Ruben Dias na kocha Pep Guardiola waibuka washindi

TUZO ZA EPL: Beki Ruben Dias na kocha Pep Guardiola waibuka washindi

Na MASHIRIKA

BEKI wa Manchester City, Ruben Dias, 24, ametawazwa Mchezaji Bora wa Mwaka wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) huku Pep Guardiola wa Man-City pia akitwaa tuzo ya Kocha Bora.

Dias ambaye ni raia wa Ureno alichangia pakubwa uthabiti wa safu ya nyuma ya Man-City walionyanyua taji la EPL kwa mara ya tatu chini ya kipindi cha miaka minne.

Dias alitawazwa Mchezaji Bora wa Msimu wa 2020-21 kwenye tuzo zilizotolewa na Chama cha Wanahabari wa Soka (FWA) mnamo Mei 2021.

Hii ni mara ya tatu kwa Guardiola kutawazwa Kocha Bora wa Mwaka katika EPL chini ya kipindi cha miaka minne.

Fowadi Erik Lamela wa Tottenham Hotspur alitawazwa mshindi wa tuzo ya Rabona kwa bao bora la msimu alilofunga dhidi ya Arsenal mnamo Machi 2021.

Dias alisajiliwa na Man-City mnamo Septemba 2020 kutoka Benfica ya Ureno kwa kima cha Sh9.1 bilioni. Tangu wakati huo, alichezeshwa mara 32 na akasaidia waajiri wake kukamilisha jumla ya mechi 15 bila kufungwa bao.

Man-City walishinda jumla ya mechi 23 ambazo Dias alisakata huku wakishinda taji la Carabao Cup na EPL pamoja na kutinga fainali ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).

Washindi wa tuzo hizo waliamuliwa kupitia kura za umma kwenye tovuti ya EA Sports pamoja na kura 20 zitakazopigwa na manahodha wote wa vikosi vya EPL na wataalamu teule wa soka kutoka Uingereza.

Wanasoka wengine waliokuwa wakiwania taji la Mchezaji Bora wa Mwaka katika EPL mnamo 2020-21 ni Kevin de Bruyne wa Man-City, Harry Kane wa Spurs, Bruno Fernandes wa Manchester United, Mohamed Salah wa Liverpool, Mason Mount wa Chelsea, Tomas Soucek wa West Ham United na nahodha wa Aston Villa, Jack Grealish.

Kwa upande wake, Guardiola aliwapiku Marcelo Bielsa, wa Leeds United, David Moyes wa West Ham, Brendan Rodgers wa Leicester City na Ole Gunnar Solskjaer wa Man-United.

Baada ya kutawazwa mshindi wa tuzo hiyo mnamo 2017-18 na 2018-19, Guardiola kwa sasa amefikia rekodi zilizokuwa zikishikiliwa na Arsene Wenger na Jose Mourinho. Aliyekuwa kocha wa Man-United, Sir Alex Ferguson ndiye anayejivunia ufanisi wa kunyanyua taji hilo mara nyingi zaidi (11).

  • Tags

You can share this post!

Sudan Kusini yakashifiwa kwa ‘kusambaza’ chanjo ya...

Mke na mwanawe Matasi kufanyiwa upasuaji Jumatatu