Michezo

Twaha Mbarak aunga Mwendwa kuzuiwa kuwania urais FKF

February 9th, 2024 1 min read

NA CECIL ODONGO

WITO kuwa Rais wa Shirikisho la Soka Nchini (FKF) Nick Mwendwa asiwanie Urais kwa mara ya tatu, unaendelea kushika kasi huku Twaha Mbarak akiwa wa hivi punde kuzungumzia suala hilo.

Kwenye mahojiano, Mbarak  alifutilia mbali madai kuwa Fifa itaipiga marufuku Kenya iwapo Mwendwa na Naibu wake Doris Petra hawataruhusiwa kusimamia kura hiyo ya Oktoba 2024.

“Inasikitisha kuwa  maafisa wa FKF hawachoki kugonganisha Kenya na Fifa,” akasema Mbarak ambaye ni Naibu Mwenyekiti wa Bandari inayoshiriki Ligi Kuu (KPL),” akasema

“Hii yote ni kwa sababu hatamu yao inatamatika mnamo Julai, 2024  na hawako tayari kushimu sheria. Kila mtu abebe msalaba wake,” akaongeza.

Mbarak ambaye aliwahi kuwa Naibu Rais wa KFF,  alishikilia kuwa Mwendwa na wandani wake ambao wameongoza soka nchini kwa miaka minane, wanazuiwa kisheria kuwa debeni.

“Mwendwa anapanga kushika nchi mateka. Hajafanya lolote la maana kupandisha viwango vya soka nchini ila anataka kuendelea kuhudumu bila mpango na ajenda. Hatutaruhusu hilo,” akasema.

Mbarak alisisitiza kuwa katiba hata hivyo inamruhusu Mwendwa  na kundi lake kuwania nyadhifa nyingine ila si zile ambazo wameshikilia kwa miaka minane.

“Hakuna mtu amemzuia Mwendwa na Petra kuwania nyadhifa nyingine FKF. Kile ambacho hawawezi kufanya ni kuwania nyadhifa zile zile walizoshikilia kwa miaka minane,” akasema.

Kauli ya Mbarak inakuja siku chache baada ya Msajili wa Michezo Rose Wasike kumwonya Mwendwa, Petra na maafisa watatu wa FKF dhidi ya kuwania.

Watatu hao ni wanachama wa Baraza Kuu la FKF ni Muriithi Nabea (Mashariki), Joseph Andere (Nyanza) na Enos Kweya (Magharibi).

 Wasike alisema kuwa hatamu ya wanne hao ilikuwa imekamilika kulingana na Sheria za Michezo 2013. Aliongeza kuwa shirikisho hilo lilikuwa limepewa cheti cha muda 2016 wakati Mwendwa na kundi lake walipochaguliwa.