TZ yapuuza madai hospitali zimelemewa na wagonjwa wa corona

TZ yapuuza madai hospitali zimelemewa na wagonjwa wa corona

NA AFP

SERIKALI ya Tanzania imekanusha vikali habari zinazoenezwa katika mitandao ya kijamii kwamba hospitali za nchi hiyo zimeshindwa kuhimili wagonjwa wanaougua virusi vya corona.

Taarifa hizo zimedai kuwa hospitali zimejaa na hakuna nafasi ya kuwalaza wengine wanaofikishwa kupokea matibabu.Katibu katika Wizara ya Afya, Profesa Mabula Mchembe, jana alisema habari hizo zinapotosha na zinalenga kuzua hofu miongoni mwa wananchi wa Tanzania.

Japo majirani zake na mataifa mengine yamekuwa yakiendeleza vita dhidi ya janga la corona, Rais wa Tanzania John Pombe Magufuli amekuwa akisisitiza kuwa nchi hiyo ilishinda vita hivyo kupitia maombi na uwezo wa mwenyezi Mungu.

Prof Mchembe alifichua kwamba amezitembelea hospitali za Mloganzila na Muhimbilia ambazo ndizo kubwa zaidi jijini Dar es Salaam na alikuwa ameshawishika kwamba sio kila mgonjwa aliyelazwa huku alikuwa akiugua virusi vya corona.

“Si wagonjwa wote katika hospitali hizo wanaugua virusi vya corona. Habari hizo ni feki na zinalenga kuwatia watu wetu uoga ilhali vita dhidi ya virusi hivi tulivishinda kitambo. Wanaoeneza habari hizo za uongo watachukuliwa hatua kali,” akasema Prof Mchembe.

Matamshi yake yanajiri siku chache baada ya Waziri wa Afya, Dorothy Gwajima, kuwaonyesha wanahabari jinsi ya kutengeneza dawa inayoaminika kuangamiza virusi vya corona kwa kuchanganya dawa za kiasili na matunda, vitungu na pilipili.

Hata hivyo, hakuna ithibati zozote za kisayansi kwamba dawa hizo zinaponya virusi vya corona.Gwajima pia alivionya vyombo vya habari dhidi ya kupeperusha au kutangaza habari zozote ambazo hazijathibitishwa kuhusu corona.

Kauli yake ilichochewa na matamshi ya viongozi wa dini ya Kikatoliki kuwa kukongamana kwa wananchi kwenye hafla za mazishi kwa wingi kulikuwa kumechochea kupanda kwa maambukizi ya virusi vya corona.

Serikali ya nchi hiyo ilitoa takwimu kuhusu maambukizi ya virusi vya corona mara ya mwisho Mei 2020 wakati ambapo vifo 20 vilirekodiwa na zaidi ya maambukizi 500.

Kilichoshangaza ni kwamba mwezi uliofuatia Rais Magufuli alitangaza hadharani kwamba nchi hiyo ilikuwa imeshinda vita dhidi ya janga hilo hatari kote ulimwenguni.

Mwezi uliopita, Rais Magufuli aliwakemea baadhi ya raia wa nchi hiyo waliotoka nje akidai ndio wamesambaza aina mpya ya corona nchini humo.Kiongozi huyo pia alisisitiza kuwa Tanzania haitanunua chanjo zozote za corona kutoka mataifa yaliyostawi.

You can share this post!

Raila asema anaweza kuingia handisheki na Ruto

Wahubiri waelezea hofu yao kuhusu taharuki ya kisiasa