Michezo

Uadui wa Argentina, Brazil wafufuka leo Ijumaa

November 15th, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

ARGENTINA itakaribisha washambuliaji matata Lionel Messi na Sergio Aguero katika kikosi chake itakapofufua uhasama leo Ijumaa dhidi ya maadui wake wa tangu jadi Brazil katika mechi ya kirafiki jijini Riyadh, Saudi Arabia.

Mechi hii ni ya 111 kati ya mabingwa hawa wa zamani wa Kombe la Dunia.

Messi, ambaye anashikilia rekodi ya mfungaji bora wa Argentina, anarejea kikosini baada ya kukamilisha marufuku ya miezi mitatu.

Nahodha huyo wa klabu ya Barcelona, amekosa mechi nne za Argentina kutokana na marufuku hiyo aliyopokea baada ya kudai kuwa Shirikisho la Soka la Amerika ya Kusini (CONMEBOL) lilionyesha ufisadi katika makala ya 46 ya dimba la Copa America nchini Brazil mwezi Julai.

Brazil ilichapa Argentina 2-0 katika nusu-fainali na kuzima Peru 3-1 katika fainali.

Messi alitoa matamshi hayo alipolishwa kadi nyekundu katika mechi ya kutafuta nambari tatu, lakini Argentina ilifanikiwa kuzoa medali ya shaba ilipolaza Chile 2-1 na imeendelea kung’ara bila nyota huyo.

Inamaanisha kuwa Argentina ya kocha Lionel Scaloni itaingia uwanjani King Saud na rekodi ya kutopoteza mechi tano zilizopita, ikiwemo kuwaaibisha Ecuador 6-1 mwezi uliopita. Hii ni rekodi yake nzuri katika kipindi cha miaka miwili.

Matokeo ya Argentina yamekuwa mazuri baada ya masikitiko ya Copa America.

Kwa upande wa Brazil, mambo yamekuwa mabaya tangu inyakue taji la Copa America mwezi Julai.

Vijana wa kocha Tite wametoka sare mara tatu na kupoteza mechi moja katika mechi nne zilizopita. Walikabwa 1-1 na Senegal na Nigeria mwezi Oktoba.

Brazil, ambayo itakosa huduma za Neymar, haijawa na ukame wa muda mrefu bila ushindi tangu ilipopiga sare tano mfululizo kati ya Novemba 2003 na Mei 2004, ingawa ilifufuka iliponyuka Argentina 3-1.

Mechi 20

Hata hivyo, kwa jumla Brazil haijafanya vibaya katika mechi 20 zilizopita. Brazil imeshinda mechi 14 na kupoteza moja pekee katika idadi hiyo.

Brazil na Argentina zinashikilia nafasi ya tatu na tisa kwenye viwango bora vya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) vilivyotangazwa Oktoba 24.

Mshambuliaji matata wa Paris Saint-Germain, Neymar anauguza jeraha la mguu alilopata Oktoba.

Kipa wa Manchester City, Ederson na mvamizi wa Ajax David Neres pia wamelazimika kujiondoa kikosini kwa sababu ya jeraha. Tite hajawapa nafasi Dani Alves, Marcelo, Fernandinho, Vinicius Junior, Everton Soares na Douglas Costa.

Nyota wa Real Madrid, Rodrygo amejumuishwa kikosini pamoja na Douglas Luiz na Wesley kutoka Aston Villa.

Vilevile, Tite atatumia Alisson Becker, Willian, Fabinho, Roberto Firmino, Gabriel Jesus na Richarlison katika mchuano huu, ambao mshambuliaji wa City, Aguero, anarejea baada ya kuachwa nje tangu Copa America limalizike.

Angel di Maria na Mauro Icardi hawajajumuishwa katika kikosi cha Argentina kinachojivunia wachezaji wakali kama Lautaro Martinez, Paulo Dybala, Giovani Lo Celso, Nicolas Otamendi na Marcos Rojo.