Habari MsetoSiasa

Uadui wa Mzee Kenyatta na Oginga Odinga ulivyoitatiza Kenya

October 19th, 2018 2 min read

Na BENSON MATHEKA

SIASA za Kenya zimeegemea familia za Jaramogi Oginga Odinga na Mzee Jomo Kenyatta, mashujaa wawili wa vita vya ukombozi, ambao miaka miwili baada ya uhuru walitofautiana na kuwa mahasimu wakuu wa kisiasa.

Wawili hao walipanda mbegu za uadui wa kikabila kwa kugoganisha makabila mawili makuu nchini, Wakikuyu na Wajaluo.

Tangu hapo siasa za Kenya zimekuwa zikikita katika uadui huo huku makabila mengine yakiunga mkono moja ya jamii hizi ama nyingine, jambo ambalo limekuwa likigawanya nchi katika mirengo miwili mikubwa ya kisiasa.

Uadui huo ulishika makali 2013 wakati mtoto wa Bw Oginga, Raila Odinga na mwenzake wa Mzee Kenyatta, Uhuru Kenyatta walipokabiliana kwenye uchaguzi mkuu na Rais Uhuru akashinda.

Hili liligawanya nchi na hayo hayo yakarudiwa mwaka jana. Hali ilichukua mkondo hatari wakati Bw Odinga na wafuasi wake walipokataa matokeo ya ushindi wa Rais Kenyatta na hata akajiapisha.

Ni katika hali hiyo ya sintofahamu ambapo walichukua hatua ambayo haikutarajiwa na wengi na kuamua kufanya kazi pamoja kuunganisha nchi. Tangu hapo utulivu mkubwa umeshuhudiwa nchini.

Baba wa wawili hao walikutana mapema miaka ya hamsini, wakati huo, Bw Oginga akiwa mfanyabiashara mashuhuri kutoka eneo la Nyanza na ni Mzee Kenyatta aliyemshawishi kujiunga na siasa.

Baadaye alimsaidia Kenyatta kuwa waziri mkuu wa kwanza wa Kenya na kisha Rais kwenye uchaguzi mkuu wa 1963. Hata hivyo, tofauti zao zilianza Bw Oginga alipoanza kukumbatia usosholisti, jambo ambalo halikumfurahisha Mzee Kenyatta na nchi za Uingereza na Amerika zilizounga mfumo wa utawala wa upebari.

Kulingana na ripoti za Shirika la Ujasusi la Amerika, Bw Oginga alianza kununua silaha kutoka Urusi na China kwa lengo la kupindua serikali ya Mzee Kenyatta.

Akiungwa na Urusi na China, Bw Oginga alianza kukosoa serikali ya Mzee Kenyatta. Mnamo 1966, alijizulu kama makamu wa rais na waziri wa masuala ya ndani na akaanza kukosoa vikali serikali ya Mzee Kenyatta.

Mnamo Oktoba 25, 1969, Mzee Kenyatta alienda Kisumu kufungua hospitali iliyofahamika kama Russia Hospital (sasa hospitali ya eneo la Nyanza) ambapo wafuasi wa Jaramogi walishambulia msafara wake.

Mwaka huo, Bw Oginga na washirika wake walitupwa kizuizini na chama chake cha Kenya Peoples Union kikapigwa marufuku.

Katika uchaguzi mkuu wa 1974, Be Oginga aliamua kugombea kiti cha eneobunge la Bondo lakini hakuruhusiwa. Kenyatta hakuwa akimwamini.

Walikutana tena katika serikali ya muungano chini ya Rais Mwai Kibaki 2007, Raila akiwa Waziri Mkuu naye Uhuru akiwa Naibu wake.

Walishindana kwenye uchaguzi mkuu wa 2013 ambapo Uhuru alimshinda Raila na historia ikajirudia 2017.