Uaminifu wa Mutua kwa Ruto wayumba

Uaminifu wa Mutua kwa Ruto wayumba

NA CHARLES WASONGA

UAMINIFU wa Gavana wa Machakos, Dkt Alfred Mutua kwa muungano wa Kenya Kwanza unaoongozwa na mgombeaji wake wa urais, Dkt William Ruto sasa unatiliwa shaka.

Hii ni baada ya Dkt Mutua kuunga mkono mwaniaji ugavana wa Machakos kwa tikiti ya chama cha Wiper, Bi Wavinya Ndeti, kinyume cha matarajio ya wafuasi wa Kenya Kwanza katika kaunti hiyo.

Chama cha Wiper ni mojawapo ya vyama tanzu katika muungamo wa Azimio la Umoja-One Kenya ambao mgombeaji wake wa urais ni waziri mkuu wa zamani Raila Odinga.

Kinaya ni kwamba gavana huyo, anayeondoka baada ya kuhudumu kwa mihula miwili, alimwidhinisha Bi Ndeti hadharani Jumapili iliyopita katika mkutano wa hadhara mjini Machakos.

“Ninaamini Wavinya Ndeti ndiye mgombeaji bora ambaye anaweza kuleta maendeleo katika Kaunti ya Machakos. Yeye ndiye anayeweza kukamilisha miradi ambayo nilianzisha lakini kwa bahati mbaya haijakamilika. Ninawaomba wakazi wa Machakos wote wampigie kura kwa wingi Jumanne Agosti 9,” Dkt Mutua akasema.

Gavana huyo alitangaza msimamo huo akifahamu fika kwamba mwenyekiti wa chama kikuu katika muungano wa Kenya Kwanza, United Democratic Alliance (UDA), Johnstone Muthama, anawania ugavana kwa tikiti ya chama hicho.

Kimsingi, Dkt Ruto anawania urais kwa tiketi ya UDA ambayo pamoja na ANC na Ford Kenya, ndivyo vyama anzilishi vya muungano huo ambao umevutia ufuasi katika pembe zote nchini.

Hatua ya Dkt Mutua kuunga mkono Bi Ndeti, ambaye alimshinda mara mbili katika chaguzi za 2013 na 2017, ina maana Bw Muthama amesalia pweke bila mwanasiasa mkuu wa kumsaidia kisiasa.

Hii ni baada ya Naibu Gavana wa Machakos, Bw Francis Maliti kujiondoa katika kinyang’anyiro cha ugavana wa Machakos na kutangaza kuwa anamuunga mkono Bi Ndeti.

Bw Maliti alikuwa akiwania kiti hicho kwa tiketi ya chama cha Maendeleo Chap Chap (MCC) kinachoongozwa na Dkt Mutua.

Kwenye barua aliyomwandikia kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka mnamo Julai 24, 2022, Bw Maliti alisema kuwa alichukua hatua hiyo kama ishara ya kuonyesha umoja wa viongozi wa Machakos “kwa manufaa ya maendeleo”.

“Nimeamua kutembea na dadangu Wavinya kwa sababu ninaamini yeye ndiye kiongozi bora kwa kaunti yetu ya Machakos. Ninamhakikishia kuwa wafuasi wangu wote watamuunga mkono ili kufanikisha ushindi wake,” akasema.

Inasemekana hatua hiyo ya Bw Maliti iliungwaji mkono na bosi wake (Dkt Mutua).Wadadisi wa siasa za Ukambani wanasema kuwa hatua ya Dkt Mutua na naibu wake kuunga mkono mgombeaji ugavana wa Wiper inaashiria kuwa Dkt Ruto alishindwa kabisa kupatanisha gavana huyo na Bw Muthama.

“Dkt Mutua na Bw Muthama wamekuwa mahasidi wa kisiasa kwa kipindi kirefu na ni wazi kuwa Ruto hajafanikiwa kusuluhisha tofauti baina ya wanasiasa hao. Athari za hali hiyo sasa inaelekea kuathiri nafasi ya Kenya Kwanza kutwaa ugavana wa Machakos na kuvuna sehemu kubwa ya kura za kaunti hiyo,” akasema wakili Gabriel Muthuma.

Tangu Dkt Mutua alipojiunga na Kenya Kwanza mnamo Mei 9, 2022, Bw Muthama aliapa kutoshiriki jukwaa moja kisiasa naye akimtaja gavana huyo kama mwanasiasa “aliyepotoka kimaadili’.

You can share this post!

Mkuki kwa Raila, kwa Ruto mchungu

PENZI LA KIJANJA: Raha ikizidi sana si raha tena!

T L