Uamuzi kortini si tishio kwa ‘Reggae’ – Raila

Uamuzi kortini si tishio kwa ‘Reggae’ – Raila

Na WAANDISHI WETU

KIONGOZI wa Chama cha ODM, Bw Raila Odinga, amepuuzilia mbali dhana kuwa uamuzi wa mahakama uliotolewa majuzi kuhusu kura ya maamuzi utaathiri mpango wa kurekebisha katiba.

Mnamo Jumatatu, majaji watano wa Mahakama Kuu waliamrisha Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) isiendeleze maandalizi ya kura ya maamuzi hadi wakati kesi zinazopinga mpango huo zitakapokamilika.

Akizungumza Jumatano baada ya kukutana na wenyeviti wa vyama vya ODM na Jubilee, matawi ya Nairobi, Bw Odinga (pichani) alisema hakuna wasiwasi wowote kuhusu uamuzi huo.

Zaidi ya hayo, alisema kiwango kikubwa cha marekebisho ya kikatiba yaliyopendekezwa yatahitaji tu kupitishwa bungeni, na ni machache yanayohitaji kufanyiwa kura ya maamuzi.

Mkutano huo ulinuiwa kuwaandaa kwa hamasisho na kampeni za kura ya maamuzi kupitia Mpango wa Maridhiano (BBI).

“Majaji wanaishi Kenya, hawaishi mbinguni. Wanaelewa hili ni jambo la dharura kwa hivyo tunaamini wataipatia umuhimu unaofaa. Hatuna wasiwasi,” akasema.

Aliongeza kuwa, uamuzi huo ulisitisha IEBC pekee kufanya maandalizi kwa hivyo shughuli nyingine zote zitaendelea jinsi ilivyopangwa.

“Isitoshe hatujafikia awamu ya kura ya maamuzi. Kwa sasa tuko katika kaunti kisha mswada uende bungeni ndipo uende kwa IEBC. Wakati huo ukifika tunatumai mahakama itakuwa imetoa uamuzi wake,” akasema Bw Odinga.

Kufikia sasa, Kaunti ya Siaya na ile ya Kisumu pekee ndizo zimepitisha mswada huo.

Kaunti ya Homa Bay imepangiwa kujadili mswada huo leo.

Hata hivyo, wanaharakati wawili wa kutetea haki za binadamu wamepinga jinsi suala hilo linaharakishwa katika bunge la kaunti.

Mabw Evance Oloo na Michael Kojo, walidai baadhi ya sheria zilizonukuliwa kwenye tangazo la bunge la kaunti kuhusu mjadala huo zimepitwa na wakati, na hivyo kufanya shughuli nzima iwe isiyofuata sheria.

Katika Kaunti ya Mombasa, Spika Arub Khatri alisema hawataharakisha shughuli hiyo kwani ni lazima wananchi wapewe nafasi kusoma mswada huo na kutoa mapendekezo yao.

Bw Khatri alithibitisha mswada wa BBI ulifikishwa bungeni Jumanne kupitia kwa Diwani wa Chaani, Kyaka Junior.

“Tuko na takriban siku 90, hakuna haja kuharakisha shughuli hii. BBI ni jambo zito. Tutakuwa na siku zisizopungua saba za kupokea maoni ya umma,” akaeleza.

Kauli sawa na hii ilitolewa na Spika wa Bunge la Kaunti ya Migori, Bw Boaz Okoth.

Alisema ingawa madiwani wamejitolea kupitisha mswada huo haraka iwezekanavyo, ni lazima kanuni zote zifuatwe kikamilifu.

“Tutafuata sheria ili kuzuia uwezekano wa kutolea watu nafasi ya kutushtaki,” akasema Bw Okoth.

Katika kaunti ya Tharaka Nithi, kamati maalumu imeundwa kusimamia shughuli nzima ya kutathmini mswada huo.

Kamati hiyo ina madiwani wote kama wanachama wake.

Gavana wa Kirinyaga, Bi Anne Waiguru, Jumatano alipigia debe mswada huo akasihi madiwani waupitishe kwa manufaa ya kaunti.

Alikuwa akizungumza alipotoa hotuba kuhusu hali ya kaunti katika bunge la kaunti.

Katika Kaunti ya Isiolo, kamati ya masuala ya haki bungeni ilisema mswada huo utajadiliwa na madiwani Jumanne ijayo.

Mwenyekiti wa shirikisho la madiwani wa Mlima Kenya, Bw Charles Mwangi, alisema watatii wito wa Rais Uhuru Kenyatta kupitisha mswada huo na watafanya hivyo haraka kabla siku 30 zikamilike.

Ripoti za Valentine Obara, George Odiwuor, Wachira Mwangi, Ian Byron, Alex Njeru, Regina Kinogu, George Munene na Mwangi Muiruri

You can share this post!

BI TAIFA FEBRUARI 11, 2021

Wembe ‘ule ule’ ndio uliomnyoa Kang’ata