Habari MsetoVideo

Uamuzi kuhusu dhamana kwa washukiwa 47 wa NYS kutolewa Juni 19

June 13th, 2018 2 min read

Na RICHARD MUNGUTI

WASHUKIWA wote 47 wanaoshtakiwa kwa sakata ya mamilioni ya pesa katika Shirika la Huduma ya Vijana kwa Taifa (NYS) Jumanne waliwasilisha maombi ya kuachiliwa kwa dhamana katika Mahakama kuu.

Washukiwa hao kupitia kwa mawakili zaidi ya 30 wakiongozwa na Mabw  Cliff Ombeta, Kirathe Wandugi,  Assa Nyakundi , Migos Ogamba na  Kimani wa Wakimaa walimweleza Jaji Hedwig Ong’undi (pichani) “haki za kimsingi za kuachiliwa kwa dhamana zilikiukwa na hakimu mkuu Douglas Ogoti aliyeamuru wasalie gerezani hadi kesi isikizwe na iamuliwe.”

Na wakati huo huo, Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) kupitia kwa wakili Bw Duncan Ondimu alisema “ dhamana katika kesi zote zinazohusu hujuma za kiuchumi zitakuwa zinapingwa vikali.”

Bw Ondimu alisema kesi zote za ufisadi na hujuma za kiuchumi zitakuwa zinasikizwa kwa siku chache.

Bw Ondimu alisema ushahidi wote dhidi ya washukiwa wote wa NYS wanaokabiliwa na  mashtaka ya matumizi mabaya ya mamlaka uko tayari na “ kesi inaweza kuanza kusikizwa  wakati wowote.”

Akipinga washukiwa wakiachiliwa kwa dhamana , Bw Ondimu alisema washtakiwa watawafuruga mashahidi.

“Mashahidi wengi katika kesi hii walikuwa wadogo wa washukiwa hawa kazini na ni rahisi kuwavuruga,” alisema Bw Ondimu.

Wakili Assa Nyakundi awasilisha tetezi mahakamani. Picha/ Richard Munguti

Lakini msimamo huo wa DPP ulikumbana na upinzani mkali kutoka kwa mawakili wanaowatetea washtakiwa.

Mabw Ombeta , Nyakundi , Karathe , Wa Kimaa na Ogamba walisema idara ya mahakama imethibitiwa kabisa na watu wenye ushawishi mkubwa serikalini.

Wakilaani matamshi ya afisa wa Polisi anayechunguza kesi hii Inspekta Paul Waweru kuwa “ atahakikisha  kesi hii imesikizwa kwa upesi na hata ikibidi masaa ya kuisikiza na kuiamua yaongezwe.”

“Je,  afisa huyu wa polisi ametoa wapi mamlaka ya kuwasimamia mahakimu na majaji. Matamshi haya yana maana kuwa mahakimu na majaji wameanza kuthibitiwa ,” alihoji Bw Nyakundi.

Mahakama iliombwa isipitoshwe na matamshi ya DPP kuwa kesi itaendelezwa kwa upesi.

“Ikiwa ombi la dhamana dhidi ya washukiwa 22 ilichukua muda hadi saa nane unusu usiku je kesi hizi 10 zitachukua muda gani?” Bw Nyakundi alimwuliza Jaji Ong’udi.

Washukiwa hao 47 ni pamoja na aliyekuwa Meneja Mkurugenzi wa NYS Bw Richard Ndubai , Katibu wa Wizara  Bi Lilian Omollo, mfanyabiashara Bi Ann Wambere waliomba korti iwaachilie kwa dhamana.

Jaji Ong’udi atatoa uamuzi wa dhamana mnamo Juni 19, 2018.

Awali malumbano makali kati ya mawakili wa washukiwa na Bw Ondimu kuhusu agizo la Bw Ogoti kwamba washukiwa wapeanze robota 10 za makaratasi ya kufanyia nakala za ushahidi.

“Agizo hili halifai. La fedhehesha Serikali. Kwani Serikali haina pesa. Ni sheria washukiwa wapewe nakala za mashahidi na afisi ya DPP.

Video Gallery