Uamuzi kushu operesheni Matungu kutolewa

Uamuzi kushu operesheni Matungu kutolewa

BENSON AMADALA na IVYN NEKESA

MAAFISA wa usalama katika Kaunti ya Kakamega watakutana Jumatatu kuamua ikiwa operesheni ya usalama Matungu inastahili kuendelea kwa muda mrefu zaidi.

Kamishna wa Kaunti anayeondoka, Bw Abdulrizak Jaldesa alisema uamuzi utafanywa iwapo operesheni hiyo ya polisi wa kawaida na kikosi cha GSU inafaa kuendelea baada ya kikosi cha usalama kukagua hali halisi ilivyo.

“Kwa miezi miwili iliyopita, usalama umeimarika katika eneo hili kwa sababu ya upigaji doria ulioongeza usiku na mchana kupambana na wahalifu,” akasema Bw Jaldesa.

Mwezi uliopita, oparesheni hiyo ya usalama iliongezwa kwa mwezi mmoja. Aliyekuwa kamanda wa Polisi wa Kaunti, Bi Wilkister Vera alisema ilikuwa ni juhudi za kukabiliana na wahalifu waliokuwa wakiuza bidhaa haramu ikiwemo pombe.

Alisema wahalifu kutoka kaunti jirani za Siaya, Busia na Bungoma walikuwa wanatumia Matungu kama maficho yao baada ya kutenda uhalifu.

Kamishna wa eneo la Magharibi, Bi Anne Ngetich alisema Jumamosi kwamba maafisa wa usalama waliopelekwa Matungu walifanikiwa kurudisha utulivu akaomba wakazi waendeleze shughuli zao bila hofu.

Alisifu maafisa wa polisi walioshiriki kwenye oparesheni hiyo kwa kufanya kazi nzuri akaomba wakazi kupiga ripoti wanaposhuku kuna uhalifu unaoendelea ili maafisa wachukue hatua.

Bi Ngetich alizungumza katika Kanisa Katoliki la St Joseph wakati wa ibada ya kuombea maafisa wa usalama katika eneo hilo.

Ibada hiyo iliongozwa na Askofu Salesius Mugambi wa Kanisa Katoliki la Meru.

Kaimu Naibu Chansela wa Chuo Kikuu cha Masinde Muliro, Prof Joseph Bosire alisema taasisi hiyo inashirikiana kwa karibu na polisi kuimarisha usalama kufuatia vifo vya wanafunzi kwenye mabweni ya chuo hicho.

You can share this post!

Shule hii inatulazimu tulipe Sh44m ilizokopa, wazazi walia

Mombasa yawataka wakazi kukoma kuwabagua makahaba na mashoga

adminleo