Habari

Uamuzi ni wako!

October 22nd, 2020 2 min read

Na BENSON MATHEKA

WAKENYA sasa wako na fursa ya kuamua mwelekeo wa uongozi wa nchi, usimamizi wa serikali na uchaguzi baada ya ripoti ya mwisho ya Jopokazi la Maridhiano (BBI), ambayo wamekuwa wakisubiri wa muda wa mwaka mmoja kukabidhiwa Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa chama cha ODM, Raila Odinga jana Jumatano.

Ripoti hiyo ambayo imepigwa msasa baada ya ile ya kwanza iliyozinduliwa 2019, inapendekeza kubuniwa kwa nyadhifa zaidi za uongozi kwa kile waandalizi walisema ni kumaliza dhana ya mshindi wa uchaguzi kutwaa kila kitu.

Katika ripoti hiyo, wadhifa wa kiongozi rasmi wa upinzani utarejeshwa bungeni kulinda maslahi ya anayeibuka wa pili katika uchaguzi wa urais.

Waandalizi walisema kubuniwa kwa wadhifa wa waziri mkuu, manaibu wake wawili na kufanya wabunge kuwa baadhi ya mawaziri kutahakikisha jamii zote za Kenya zitashirikishwa katika serikali.

Rais atakuwa na nguvu za kumfuta kazi waziri mkuu moja kwa moja au kupitia kura ya kutokuwa na imani naye bungeni.

Ikiwa Wakenya wataridhika na ripoti hiyo na kuipitisha kwenye kura ya maamuzi, maafisa wa serikali watakuwa wakiajiriwa na kampuni huru ya kibinafsi ili kukomesha ukabila. Viongozi na maafisa wa serikali wamelaumiwa kwa kupendelea jamaa zao katika uajiri wa wafanyakazi wa serikali.

Wafanya kazi wa umma hawatakuwa wakipata marupurupu wakihudhuria vikao au mikutano katika hatua ya kupunguza gharama ya kuendesha serikali.

Wabunge watakaoteuliwa mawaziri hawataongezewa mshahara lakini watakuwa wakipata marupurupu kwa kazi ya ziada.

Kulingana na ripoti hiyo iliyozinduliwa Jumatano, mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka na makamishna wengine sita watateuliwa chini ya mfumo mpya wa kisheria ambapo vyama vya kisiasa vitapendekeza watu watakaoteuliwa kwa nyadhifa hizo.

“Ili kuhakikisha kuwa IEBC inaendesha uchaguzi kwa njia huru, yenye haki na itakayoaminika, imependekezwa kwamba viongozi wa vyama vya kisiasa wahusishwe katika uteuzi wa makamishna. Aidha, hii itajenga imani ya vyama hivyo kwa IEBC kupitia uungwaji mkono kutoka kwa wagombeaji,” ikasema ripoti hiyo.

Ripoti hiyo inapendekeza kuwa, wafanyakazi wote wa afisi hiyo kuu watahudumu kwa kandarasi ya miaka mitatu. Kandarasi hiyo inaweza kuongezwa mara moja pekee.

“Vile vile, wasimamizi wa uchaguzi watafanya kazi kama vibarua na hawataruhusiwa kusimamia zaidi ya uchaguzi mmoja,” inaeleza ripoti hiyo.

Mageuzi mengine ambayo yanapendekezwa kufanyiwa IEBC ni kwamba, sio lazima mwenyekiti awe mwanasheria ilivyo katika sheria ya sasa. Ili kuhakikisha kaunti zinatekeleza majukumu kikamilifu zitatengewa asilimia 35 katika bajeti ya serikali ikiwa Wakenya watakubali mapendekezo ya ripoti hiyo.

Kaunti pia zitagawiwa pesa kwa kuzingatia huduma na idadi ya watu. Kama hatua moja ya kuhakikisha usawa wa jinsia,wagombea wenza watakuwa jinsia tofauti na wagombeaji. Baada ya kupokea ripoti hiyo Rais Kenyatta aliwataka Wakenya kujiandaa kwa ajili ya kura ya maamuzi kurekebisha Katiba.