Habari MsetoSiasa

Uamuzi wa kesi ya uchochezi dhidi ya Kuria waahirishwa

July 8th, 2019 2 min read

Na RICHARD MUNGUTI

UAMUZI wa kesi ya uchochezi dhidi ya Mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria uliahirishwa Jumatatu hadi Julai 29, 2019.

Hakimu mkuu Francis Andayi aliyesikiza kesi hiyo alimweleza Kuria “amekuwa na kazi nyingi hakupata fursa ya kuuandaa.”

Hata hivyo alisema atakuwa likizoni na atapata fursa ya kuchambua ushahidi huo na kuandika ushahidi.

“Nikiwa likizoni nitapa fursa ya kuandaa uamuzi na kuusoma Julai 29 nikirejea kazini. Samahani kwa kutouandaa kwa muda niliokueleza,” Bw Andayi alimweleza Mbunge huyo.

Bw Kuria ameshtakiwa kwa kutoa matamshi ya uchochezi dhidi ya kinara wa Nasa Raila Odinga.

Na wakati huo huo anakabiliwa na shtaka la kutoa matamshi ya kumkejeli mke wa kinara huyo Aida.

Upande wa mashtaka ukitamatisha ushahidi dhidi ya Kuria, afisa wa polisi alikiri hakuchunguza ipasavyo kanda ya video unaomnukuu mwanasiasa huyo akichochea dhidi ya kinara wa muungano wa Nasa Raila Odinga.

Katika kanda hiyo Bw Kuria amenukuliwa akitamka maneno ya uchochezi dhidi ya Bw Odinga huku akiwasihi wakazi wa mkoa wa kati wasikubali kumpigia kura kinara huyo wa upinzani.

Matamshi hayo katika video hiyo iliyodaiwa ilinukuliwa Septemba 5, 2017 katika eneo la Wagige kaunti ndogo ya Kikuyu imo katika lugha ya Gikuyu.

Mshtakiwa alimweleza hakimu anaelewa bayana lugha ya Gikuyu, Kiingereza na Kiswahili.

“Ninafanyakazi katika mamlaka ya mawasiliano nchini CAK lakini mimi ni afisa wa polisi katika kitengo cha uhalifu wa kimitandao,” alisema Insp Tiha na kuongeza, “Kanda hii inamnkuu Bw Kuria akitoa matamshi ya uchochezi na uhasama wa kijamii.”

Mtaalam wa uhalifu wa kimitandao Inspekta Alexande Mathenge Tiha alimweleza hakimu mkuu Francis Andayi kuwa alitumiwa kanda hiyo na Mkurugenzi wa Uchunguzi wa Jinai (DCI) mnamo Septemba 11, 2017.

“Nilitumiwa mkanda huo wa video na DCI kuuchunguza kwa lengo la kubaini matamshi ya uchochezi na uhasama wa kikabila dhidi ya Bw Odinga,” alisema Insp Tiha.

Insp Tiha alisema DCI alimtaka aukangue mkanda huo kisha “ atoe ushauri kuhusu matamashi ya uchochezi na uhasama aliodaiwa kautamka Bw Kuria na aliyekuwa Seneta wa Machakos Johnstone Muthama.”

Afisa huyo aliucheza mkanda huo mbele ya Bw Andayi na kutoa maelezo.

Akihojiwa na wakili Francis Munyororo Insp Tiha alisema “ ripoti yake ni tofauti kabisa na shtaka inayomkabili Bw Kuria.”

Katika shtaka hilo inadaiwa Bw Kuria aliwataka wapiga kura 70,000 waliompigia Bw Odinga kura wasakwe.

“Je, katika ripoti uliyowasilisha hakuna mahala Bw Kuria amenukuliwa akitaka wapiga kura 70,000 waliompigia kura Bw Odinga wasakwe , ile ulitoa ripoti iliyotofauti?” Bw Munyororo alimwuliza afisa huyo wa polisi anayehudumu katika mamlaka ya mawasiliano CAK.

“Ni kweli ripoti yangu iko tofauti,” alijibu Insp Tiha.

“Ni ukweli ulienda kinyuma na matakwa ya DCI na ukatoa ripoti ambayo haikutakiwa na DCI kumuhusu Bw Kuria?” Bw Munyororo alimtaka Insp Tiha afafanue.

“Ni kweli,” alijibu.

Akimjibu Bw Andayi afisa huyo wa polisi alikiri alitenda yale hakutakiwa na kutoa ushauri ambao haukutakiwa kumuhusu Bw Kuria.

Bw Kuria alieleza mahakama atakuwa akiiomba imwachilie kwa vile hakuna ushahidi unaomlenga katika kesi aliyoshtakiwa miaka miwili iliyopita.

Hakimu atapokea ushahidi wa Bw Kuria Juni 27, 2019.

Bw Kuria amekanusha shtaka dhidi yake na yuko nje kwa dhamana.