Uangalizi mdogo, mahitaji machache msukumo tosha wa kukuza karoti

Uangalizi mdogo, mahitaji machache msukumo tosha wa kukuza karoti

NA RICHARD MAOSI

Zao la karoti linahitaji uangalizi mdogo, hivyo basi mkulima anaweza kupata nafasi ya kufanya shughuli nyinginezo za shambani.

Karoti zinahitaji eneo lenye joto la kadri. Aidha, endapo mmea huu utapandwa katika sehemu inayoshuhudia mvua nyingi mkulima atengeneze matuta yaliyoinuliwa ili kuzuia mmomonyoko wa udongo.

Mbolea za asilia zilizokauka vizuri na kupalilia shamba mara kwa mara ni mambo ya kimsingi wakati wa kuzuia magugu.

Akilimali ilipata fursa ya kuzuru eneo la Kaprop Marioshoni, kaunti ndogo ya Njoro ambapo tulikutana na Samson Njung’e, mkulima na mfayabiashara wa karoti.Anasema msimu huu wa Covid-19, biashara yake imeendelea kama kawaida licha ya watu wengi kupoteza kazi ama kupunguziwa mshahara.

Hapa tunamkuta Samson akiwa miongoni mwa vibarua, wakisaidiana kupakia magunia yaliyojaa karoti kwa ajili ya kusafirisha kuelekea jijini Nairobi.Anasema kuwa wakulima wengi kutoka sehemu za Molo, Njoro, Kuresoi Kusini na Elburgon wamebadilisha dhana na kugeukia ukulima wa karoti, badala ya kukuza viazi.

“Wakati wa msambao wa corona tuliendelea na biashara zetu kama kawaida, ikizingatiwa kuwa watu ni lazima wapate vyakula kila wakati,” akasema.Anaona kuwa siku zijazo wakulima wengi wataelekeza juhudi zao zote katika kilimo cha karoti, badala ya viazi mbatata, akiongezea kuwa bei yake ni nzuri sokoni.

Samson amewekeza katika biashara ya kununua karoti kutoka kwa wakulima mashinani na kuwasaidia kupata soko nje ya Kaunti ya Nakuru, pamoja na mataifa ya Uganda na Tanzania.

Kulingana naye hatua hii imesaidia kutengeneza nafasi nyingi za ajira kwa vijana kutoka eneo la Njoro ambao hufanya kazi katika viwango mbalimbali kama vile kupanda, kupalilia, kuvuna na kupakia mizigo.

Alieleza kuwa ni kazi ambayo amefanya kwa takriban miaka tisa, ambapo kila mwaka msimu wa kupanda ni kuanzia Machi mvua ya rasharasha inapoanza.

Anasema kuwa yeyote ambaye analenga kuwekeza katika biashara hii ni lazima atafute mtaji wa kutosha wa takribani 100,000 ili aweze kuhudumia soko kubwa la wanunuzi mbali na kukidhi gharama ya usafiri.

“Karoti ni zao ambalo halina gharama nyingi ikilinganishwa na viazi, kwa mfano haina mahitaji ya kupulizia dawa za kuzuia baridi,” asema.

Aidha, huhitaji kutibu mimea yako dhidi ya wadudu, isipokuwa wakati majani yanapofikia baina ya sentimita 13-15 hivi, ukungu unaweza kushambulia majani na kuyafanya yaanze kunyauka.

Pili magonjwa ya bakteria almaarufu kama bacterial disease yanaweza kutambulika mapema endapo mimea itaanza kuregea, mmea usikue (stunted growth) ama mashina kuoza kabla ya wakati wa kuvuna.

Anaeleza kuwa ili kukabiliana na changamoto hii, ni muhimu mkulima kuzuia kupanda karoti zake katika sehemu ambayo imewahi kushambuliwa na ugonjwa huu, pia anaweza kunyunyizia mimea yake dawa ili kuzuia fangasi zinazoweza kusababisha maradhi haya.

Samson anawahimiza vijana kujitosa katika kazi hii ambayo haina wengi na wanaweza kupata tija nzuri na kujiendeleza kiuchumi badala ya kusumbuka wakitafuta kazi.

“Soko la karoti ni la uhakika kwa sababu hiki ni kiungo (spice) muhimu ambacho hutumika katika mapishi mengi kama vile nyama, pilau miongoni mwa vyakula vinginevyo,” alisema.Karoti huvunwa miezi mitatu hivi tangu kipindi cha kupandwa, na mizizi yake ndiyo hutumika kama kiungo muhimu cha lishe au matumizi mengine ya dawa za kiasili.

Aidha wauzaji wengine hutumia karoti kutengeneza juisi ya saladi, huku ikiaminika kuwa madini yake yana uwezo ya kuboresha uwezo wa macho kuona mbali, pamoja na kutibu maradhi ya kiungulia.

You can share this post!

Matiang’i aahidi kuanika walanguzi wa mihadarati

KDF ashtakiwa kwa kutafuna hongo ya Sh480,000