Makala

UBABE: Hatari ya vita baina ya Amerika na Uchina yanukia 2019

January 8th, 2019 4 min read

NA FAUSTINE NGILA

KATIKA taarifa za kimataifa za miaka ya hivi karibuni, vita vya kiuchumi baina ya Amerika na Uchina zimetawala kwenye vyombo vya habari tangu Rais Donald Trump aingie Ikulu ya White House.

Lakini msimamo mkali dhidi ya sera za kiuchumi za Uchina wa Bw Trump ulianza wakati wa kampeni za uarais hapo 2016 na amezidi kuzipinga kufikia mwaka huu.

Tofauti na marais wa zamani wa Uchina ambao serza zao zililenga kufaidi mataifa yote mawili, Trump amebadilisha siasa za kiuchumi na kuwa za ushindani mkali wenye uadui ndani yake.

Hapo 2018, usimamizi wa Trump ulipandisha joto la siasa hizo, ulipowekea bidhaa zote kutoka Uchina ada ya juu ya ununuzi ya Sh2.5 trilioni. Hatua hii iliisukuma serikali ya Beijing kupiga bidhaa za Amerika ada ya Sh1.1 trilioni.

Na kuanzia Januari mosi mwaka huu, ada ya asilimia 10 ya Amerika kwa bidhaa kutoka Uchina ilipandishwa hadi asilimia 25, ambayo sasa imekuwa kisiki katika ukuaji wa sekta za bidhaa husika.

“Sarafu ya Uchina imedidimia dhidi ya dola ya Amerika. Kampuni zinaweza kupata hasara kubwa sana wakati ada imepanda hadi asilimia 25, na hii itakuwa na athari kubwa kwa uchumi wa Dunia,” akasema mtaalamu wa masuala ya uhusiano wa kimataifa Edward Alden.

Umaarufu wa Trump

Licha ya hayo, Trump amejizolea umaarufu zaidi katika ngome zake, na kuweza pia kuwashawishi wanasiasa wa Democrat katika kampeni yake ya ‘Kurudisha Hadhi ya Amerika.’

Uchina na taifa ambalo limeanza mapinduzi ya viwanda majuzi, ikilinganishwa na Amerika, na imetumia teknolojia nyingi za Amerika kujiimarisha kiuchumi. Kulingana na Trump, Uchina imeiba maarifa ya Amerika na kujitapa nayo kimataifa huku ikijiboresha kiteknolojia.

Amerika hudai kuwa Uchina imeiba siri zake kuu za kibiashara, ikakiuka sheria zinazolinda teknolojia, michakato ya uundaji bidhaa viwandani, na kulazimisha kampuni za Amerika zilizowekeza Uchina kutoa siri zake za ufanisi wa kiteknolojia huku ikidukua taarifa muhimu zinazolinda viwanda vya Amerika.

“Hizi ndizo mbinu za hila ambazo Uchina inatumia kujiimarisha kiteknolojia. Wanataka kuwa magwiji katika mustakabali wa teknolojia duniani, kuanzia magari ya kielektroniki hadi teknolojia zote za kiroboti,” anasema Alden.

Ruwaza ya Uchina kuhusu nia yake ya kutawala Dunia kiuchumi ilianza hapo 2015 ilipozindua kampeni ya Made in China 2025 Initiative, na inalenga kuibadilisha nchi hiyo kutoka weledi wa viwandani hadi gwiji wa teknolojia ulimwenguni.

Ikumbukwe kuwa wiki iliyopita Uchina ilituma chombo cha kwanza kutua karibu na mwezi katika harakati zake za kutafiti kuhusu anga nje ya sayari ya Dunia, ishara ya uwezo wake wa ubunifu wa kisasa.

Tisho kwa usalama

Amerika kwa upande wake imesema hatua hizi za Uchina ni tisho kubwa sana kwa usalama wake katika miaka mingi ijayo.

“Iwapo Uchina itaafikia udhibiti wa teknolojia inayolenga, itakuwa tisho kubwa kwa jeshi la Amerika kuliko ilivyo sasa. Masuala ya kiuchumi na kiusalama yako sambamba,” anasema Alden.

Lakini Uchina imejitetea vikali dhidi ya malengo yake ya kujitegemea kiuchumi na kiteknolojia, ikisema inadhamiria kuboresha uwezo wake kukabili vizuizi vya kiuchumi kutoka mataifa ya Magharibi.

Utawala wa Trump umekejeli mtindo wa Uchina kuzima viwanda vya kampuni za Amerika nchini humo, na kukataa kuruhusu kampuni za mataifa ya Magharibi kuwekeza katika nchi yao.

Tangu mwisho wa Vita vya Pili vya Dunia, kumekuwa na uhusiano wa kibaridi baina ya mataifa ya kikomunisti na yale ya kikapitalisti, huko yote yalaumiania kwa sera zake kuhusu masuala ya kiuchumi, kijamii na kisiasa.

“Tatizo hapa ni kuhusu ushindani katika teknolojia na Nyanja nyingine ambazo Uchina inafaa kukabiliwa vikali. Hii ndiyo taswira ya Amerika. Inafaa kutiba bidii zaidi katika ubunifu wa kiteknlojia kuzima uwezo wa Uchina,” anasema mwanauchumi wa mradi wa Asia na Pasifiki katika Jumba la Chatham, Bw Kerry Brown.

“Fikra za masoko kutawalwa na taifa la kikomunisti linaikera Amerika na inataka kuona mabadiliko makuu. Hili ndilo suala zima. Sina hakika kama inawezekana katika mkutano mmoja wa marais wa pande zote. Suala hili la uadui huenda likazidi kutokota kwa miaka mingi ijayo,” anasema.

Kando na ada za uagizaji wa bidhaa, Amerika pia imeiwekea Uchina shinikizo za kisiasa, na kuongeza imani kuwa hivi sasa vitakuwa vita vya moja kwa moja kupitia Nyanja mbalimbali, sawa na Vita vya Baridi baina ya Amerika na Urusi miaka ya themanini.

Vikwazo zaidi 

Agosti 2018, Amerika ilizidisha vikwazo dhidi ya Uchina, na kuzima mauzo ya bidhaa za teknolojia ya hali ya juu nchini humo. Pia ilipitisha sheria mpya ambayo inazuia Wachina kuwekeza Amerika katika sekta ya teknolojia.

Hapo Septemba mwaka uliopita, Trump alikiwekea vikwazo kitengo kimoja cha jeshi la Uchina kuhusu ununnuzi wa ndege za kivita kutoka Urusi na mabomu ya kutoka ardhini hadi angani.

Katika siasa, Amerika ilidai Uchina ilijaribu kuvuruga Uchaguzi wa mwaka uliopita wa mabunge. Uchina ilikana madai hayo, na badala yake kuikejeli Amerika kwa maandalizi ya majeshi yake katika bahari ya South China.

Kwenye kongamano la muungano wa Asia-Pasifiki hapo Novemba 2018, Naibu Rais wa Amerika Mike Pence aliikosoa Uchina kwa miradi yake ya ufadhili wa ujenzi wa barabara na madaraja akasema ni njia moja kubwa ya kuyasukumia mataifa yanayoendelea madeni makubwa ili yaiunge mkono kwa sera zake.

Akihutubu katika kongamano hilo, rais wa Uchina Xi Jin Ping alijitetea kuwa ufadhili wake ni ‘mtego’ na kwamba Beijing haina ‘ajenda fiche’ huku akikejeli sera ya ‘Amerika Kwanza’ kuhusu vikwazo.

Amerika sasa imeapa kuzidisha vikwazo dhidi ya bidhaa kutoka Uchina na hatimaye kupiga marufuku bidhaa zote, iwapo taifa hilo halitafuata masharti inayotaka.

Maafisa wakuu serikalini Amerika wamepuuzilia mbali uwezekano wa suluhu kwa zogo hili, huku wadau wa masuala ya kimataifa wakisema kuwa “masuala yanayohusu Trump hayawezi kutabiriwa, na huenda suluhu ya kiajabu ikapatikana.”

Ikikosekana, basi uhasama huu huenda ukafikia kiwango cha kuigawanya Dunia zima kwa mirengo miwili mwaka huu – Ule unaounga mkono Amerika, na ule utakaoshikilia kuwa Uchina ina sera bora za kiuchumi.