MakalaSiasa

UBABE: Seneti na Bunge la Kitaifa kuzidi kukabiliana

June 18th, 2019 3 min read

Na CHARLES WASONGA

VITA vya ubabe kati ya Bunge la Kitaifa na Seneti vitaendelea kutokota wiki hii maseneta watakapowasilisha kesi mahakamani kupinga uhalali wa sheria 20 zilizopitishwa bila mchango wao.

Haya yanajiri siku chache baada ya maseneta kutoka kwa hasira katika kikao cha kamati ya upatanishi uliobuniwa na Maspika wa Mabunge hayo mawili kusaka muafaka kuhusu Mswada wa Ugavi wa Mapato (DORB).

Hatua hiyo ilichangia kusambaratika kwa mazungumzo kuhusu mswada huo na kupelekea Bajeti ya Kitaifa kusomwa Alhamisi kabla ya kupitishwa kwa mswada huo.

Maseneta wanasema wamechukua hatua ya kwenda kortini baada ya wenzao katika Bunge la Kitaifa kukataa kusaka mchango wao kabla ya kupitishwa kwa sheria hizo, ikiwemo ile ya Mageuzi ya Sheria mbalimbali za Afya.

Wabunge pia hawajawashirikisha maseneta katika mjadala kuhusu miswada mingine 83 ambayo iko mbele ya Bunge la Kitaifa wakati hii.

Mwenyekiti wa Kamati ya Seneti kuhusu Masuala ya Sheria, Katiba na Haki za Kibinadamu Samson Cherargei Jumatano (17/6/2019) alikutana na maseneta wote ambao ni wanasheria kuandaa kesi ambayo itawasilishwa katika Mahakama Kuu siku yoyote wiki hii.

“Tulikutana leo (Jumatatu) na wenzetu wote ambao ni wanasheria kuandaa kesi hiyo. Tunapanga kuwasilisha kesi hiyo wakati wowote, ikiwezekana, kabla ya Ijumaa,” akasema Bw Cherargei ambaye ni Seneta wa Nandi.

Maseneta pia wanapania kupinga vipengee kadhaa vya sheria ya bunge la kitaifa ambavyo wanadai vinakiuka Katiba. Haswa wanalenga sheria ya bunge nambari 12 (2) ambayo wanadai inakiuka Katiba kwa sababu inasema hitaji la mapatano kuhusu mswada linaweza tu kuwepo ikiwa swali litaibuliwa kuhusu iwapo mswada unahusu kaunti au la.

Maseneta wanadai kuwa Spika wa Bunge la Kitaifa amejipa mamlaka chini ya kipengee cha 110 (3) cha Katiba kiasi kwamba huwa anapuuza wajibu wa Seneti katika mchakato wa utayarishaji wa sheria.

Kipingee hicho kinahitaji kwamba kabla bunge lolote kushughulikia Mswada wowote, Maspika wawili sharti wasuluhishe swali lolote la iwapo mswada huo unahusu kaunti. Na ikiwa mswada huo unahusu kaunti, maspika hao wanafaa kubaini ikiwa ni mswada wa kawaida au spesheli.

Haswa maseneta wamekerwa na hatua ya Bunge la Kitaifa kujadili, kupitisha na kuwasilishwa kwa Rais Mswada wa Marekebisho ya Sheria za Afya.

Mswada huo ambayo ulifanyia marekebisho sheria 13 kuhusu Afya ulitiwa saini na Rais Uhuru Kenyatta mwezi ujao katika Ikulu ya Nairobi katika kikao kilichohudhuriwa na kiongozi wa wengi katika Seneti Kipchumba Murkomen.

Baadhi ya hizo, zilizofanyiwa marekebisho ni; sheria kuhusu Dawa na Sumu, sheria kuhusu Mamlaka ya Usambazaji Dawa (KEMSA), sheria ya Wauguzi, Sheria ya Wataalamu wa Lishe, Sheria ya Madaktar na Sheria ya Chuo cha Mafunzo ya Matibabu, kati ya mengine.

Seneta wa Siaya James Orengo, ambaye ni Wakili Mkuu, alisema sheria hiyo kuhusu sekta ya afya ilipasa kushughulikiwa na Seneti kwa sababu majukumu ya afya yamegatuliwa kwa kima cha asilimia 90.

“Bunge la kitaifa lilikiuka Katiba kwa kupitisha mswada wa mageuzi ya sheria mbalimbali za afya bila mchango wa Seneti ilhali asilimia ya sekta ya afya imegatuliwa. Hii ndio maana tunataka mahakama ibatiliishe sheria hii yote,” akasema Bw Orengo ambaye ni kiongozi wa wachache katika seneti.

Hatua ya maseneta kwenda kortini inaungwa mkono na Baraza la Magavana (CoG). Wiki jana Mwenyekiti wa Kamati ya Afya katika baraza hilo Mohamed Kuti alisema baraza hilo liko tayari kuweka rasilimali katika kesi hiyo kwa lengo la kuifanikisha.

Lakini kiongozi wa wengi katika Bunge la Kitaifa Aden Duale alipuuzilia mbali hatua ya maseneta kwenda kortini akisema shughuli ya utengenezaji wa sheria haifai kuendeshwa katika mazingira ya vitisho.

“Tuko tayari kutetea msimamo wetu kwa sababu shughuli zetu zote ziliendeshwa kisheria,’ akasema.

Bw Duale alisema hatua ya maseneta kwenda kortini itaathiri zaidi mahusiano kati ya Seneti na Bunge la Kitaifa,” akasema Bw Duale ambaye ni Mbunge wa Garissa Mjini.

“Bunge la kitaiafa huendesha shughuli zake kwa kuzingatia vipengee husika vya katiba sio kwa kupitia vitisho. Na wajibu wetu katika taratibu za utayarishaji wa sheria umefafanuliwa wazi katika vipengele vya 93,94,95, na 96 na maseneta wanapaswa kufahamu wajibu wao,” akaeleza.

Haitakuwa mara ya kwanza kwa mahakama kuingilia kati vita au mgongano kati ya Bunge la Kitaifa na Seneti kuhusiana na suala la utengenezaji wa sheria, Mnamo 2014 Mahakama ya Juu ilishughulikia suala hilo na kuamua kwamba Seneti inapasa kuhusishwa katika utayarishaji wa sheria zote isipokuwa zile zinazohusu gharama ya kifedha.

Kwa mujibu wa Katiba wajibu wa Serikali Kuu katika sekta ya Afya ni masuala ya Sera na Usimamizi wa Hospitali tatu za Kitaifa za Rufaa ambazo ni Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH), Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Moi, Eldoret (MTRH) na Hospitali ya Kitaifa ya Wagonjwa wenye akili punguani ya Mathari iliyoko Nairobi.