Siasa

Ubabe wa kisiasa wa Ford-Kenya na DAP-K watokota Trans Nzoia

March 3rd, 2024 1 min read

NA EVANS JAOLA

MAKABILIANO makali ya ubabe wa kisiasa yamezuka baina ya viongozi wa vyama vya Democratic Party of Kenya (DAP-K) na Ford-Kenya katika Kaunti ya Trans Nzoia.

Madiwani wanaomuunga mkono Gavana George Natembeya katika kaunti hiyo, wanadai kwamba kuna njama zinazoendeshwa na uongozi wa Ford-Kenya kuhujumu serikali ya gavana huyo.

Makabiliano hayo yalijitokeza Jumamosi wakati wa mazishi ya mzee wa jamii ya Abaluhya, Ruben Masengeli, katika kijiji cha Bidii, eneobunge la Kwanza.

Kwenye makabiliano hayo, viongozi hao walizomeana hadharani kuhusu tofauti za kisiasa zinazoendelea kutokoka baina ya gavana Natembeya na Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula.

Cheche kali baina ya viongozi hao zilianza wakati diwani wa zamani wa wadi ya Kapomoi, Ben Wanjala, aliye mshirika wa karibu wa Bw Wetang’ula, kuwalaumu viongozi wa DAP-K Kwa kumdharau kiongozi huyo.

Alimwonya Bw Natembeya kwamba atapigiwa kura kwenye uchaguzi wa 2027 kulingana na utendakazi wake.

“Haijalishi utatuhangaisha kwa kiwango kipi. Utapigiwa kura kulingana na vitendo vyako ifikapo mwaka 2027,” akasema Bw Wanjala, kwenye kauli aliyomwelekeza Bw Natembeya.

Lakini wakati akitoa kauli hiyo, alizomewa na baadhi ya waombolezaji.

Mbunge wa Kwanza, Ferdinard Wanyonyi, pia aliukosoa uongozi wa DAP-K kwa madai ya kuwakosea heshima viongozi wa Ford-Kenya katika eneo hilo.

“Hebu tuheshimu Ford-Kenya kama chama cha pili kilichodumu miaka mingi zaidi nchini. Hivi ndivyo demokrasia inahitaji,” akasema Bw Wanyonyi.

Hata hivyo, madiwani, wakiongozwa na Naibu Spika wa Bunge la Trans Nzoia Obed Mwale, waliukosoa uongozi wa Ford-Kenya kwa kudai viongozi wa chama hicho wanasuka njama za kumhujumu Bw Natembeya. Alisema wako tayari kukabili njama hizo.

“Kama bunge, tumeapa kushiriana na gavana ili kuharakisha maendeleo. Tuko tayari kumtetea dhidi ya wale wanaolenga kuhujumu uongozi wake,” akasema Bw Mwale.

Mratibu wa mikakati katika DAP-K Joshua Werunga, alidai kuna njama za wandani wa Bw Wetang’ula kumhangaisha Bw Natembeya na baadaye kumlaumu kwa kutotekeleza maendeleo kikamilifu.