Makala

UBAGUZI SGR: Wakenya na Wachina hawakai meza moja wakila

July 18th, 2018 2 min read

Na LUCY KILALO

WAZIRI wa Uchukuzi James Macharia amekiri kuwa raia wa Kenya na wenzao wa China wanaofanya kazi katika SGR hawakai kwa meza moja katika sehemu yao ya maankuli.

Hata hivyo, waziri huyo ametetea hali hiyo kuwa inatokana na tofauti za kitamaduni na kukosa uwiano kwa njia kadha mojawapo ikiwa ni lugha wanazotumia.

Waziri huyo sasa anatarajiwa kuwasilisha ripoti katika muda wa wiki moja kuhusiana na madai ya ubaguzi dhidi ya Wakenya wanaofanya kazi kwa SGR.

“Mimi mwenyewe nilifuatilia suala hilo la sehemu ya maankuli na kupata kuwa sio ubaguzi bali ni tatizo la mwingiliano wa kitamaduni. Nilieleza CRBC ihakikishe kuwa inavunja hali hiyo na kuhakikisha uwiano,” alisema.

Kamati ya Uchukuzi ya Bunge la Kitaifa ilikuwa imemtaka waziri huyo kuelezea kuhusu madai ya ubaguzi hasa kwa Wakenya wanaofanya kazi wa SGR.

“Uwasilishe ripoti Jumanne wiki ijayo ambayo pia ionyeshe idadi ya Wakenya waliopo kwa nafasi za usimamizi katika kampuni ya China Roads & Bridge Corporations (CRBC), idadi ya Wakenya na wafanyakazi wengine wa kimataifa na pia mishahara inayolipwa kwa wote,” mwenyekiti wa kamati hiyo, ambaye ni mbunge wa Pokot Kusini, David Pkosing aliagiza.

Kampuni ya CRBC ilitia mkataba na shirika la Kenya Railways kuendesha shughuli za treni hizo.

Maswali hayo yaliibuka kufuatia taarifa iliyochapishwa na moja wapo ya magazeti nchini, ikionyesha wafanyakazi hao wakilalamikia kubaguliwa na kudhulumiwa.

Bw Macharia aliambia kamati kuwa madai hayo yanachunguzwa na atakuwa na jibu kamili baada ya kupokea ripoti ambayo ni pamoja na kutoka kwa wizara ya Leba.

“Yeyote atakayepatikana kuhusika atatimuliwa kwa kunyang’anywa kibali chake cha kufanya kazi,” alieleza.

Akijibu swali la wafanyakazi hao kutoruhusiwa kuwa kwa mitandao ya kijamii, aliunga mkono hatua hiyo akisema kuwa haiwezekani kwa mtu kumwaga mtama kuhusu kampuni iliyomwajiri.

“Hauwezi kuwa kwa mtandao wa kijamii ukizungumzia mwajiri wako. Hiyo haikubaliki,” alisema akiongeza kuwa hata baadhi yao waliapa kwa kutumia Biblia na kuna mambo hawawezi kuyazungumzia.

Vile vile, alisisitiza kuwa raia wa China wanaofanya kazi wa SGR ni 841 pekee ikilinganishwa na 2,679 ya Wakenya. Idadi hiyo ya raia wa China alisema itaendelea kupungua kadri Wakenya zaidi wanapopata ujuzi wa kuhudumu katika treni hiyo, hatua ambayo inatarajiwa kutekelezwa kwa kikamilifu kufikia 2027.

Alisema kuna wanafunzi wa Kenya 100 ambao wamedhaminiwa na CRBC kusomea katika Chuo Kikuu cha Beijing Jiatong kwa digrii ya miaka minne ya masuala ya uhandisi wa reli. Wanafunzi wa kwanza ambao walianza masomo 2016 wanatarajiwa kufuz8uu mwaka ujao na kuanza kufanya kazi kwa Madaraka Express.

Waziri Macharia alikuwa akijibu taarifa hiyo iliyochapishwa ambapo raia wa nchi hiyo walitajwa kuwa takriban 5,000 na kuchukua nafasi nyingi za kazi.

Baada ya madai hayo kuibuka wiki iliyopita, waziri wa Leba Ukur Yatani aliunda kundi la maafisa wa wizara wa ngazi za juu kuchunguza madai hayo ya ubaguzi. Waziri huyo pia alisema kuwa iwapo madai yatabainishwahatua mwafaka ambazo ni pamoja na kufunguliwa mashtaka zitachukuliwa.

Kundi hilo lilikuwa na muda wa siku saba kufanya uchunguzi wake na kuwasilisha ripoti.Wakati huo huo, jana Waziri Macharia alieleza kuwa kampuni hiyo ya China imeagizwa kuunda ua la umeme linalofaa ili kudhibiti vifo vya wanyama pori.