Habari

Ubaguzi wa wazi?

July 19th, 2020 2 min read

DERICK LUVEGA na BENSON AMADALA

SERIKALI imekashifiwa kwa kuonekana kupendelea viongozi wa kisiasa wanaomuunga mkono Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM, Raila Odinga, katika utekelezaji wa kanuni za kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona.

Kwa upande mmoja, wanasiasa wanaounga mkono handisheki kati ya Rais Kenyatta na Bw Odinga waonekana kuruhusiwa kuandaa mikutano ya hadhara, huku wale wanaoegemea upande wa Naibu Rais, Dkt William Ruto wakitawanywa na polisi hata ndani ya maboma yao.

Serikali ilikuwa imepiga marufuku mikutano ya kisiasa kama njia mojawapo ya kuepusha mikusanyiko ya watu ambayo hutoa nafasi yao kuambukizana corona.

Jumamosi, hali hii ilishuhudiwa katika eneo la Magharibi mwa nchi ambapo wandani wa Dkt Ruto walifurushwa kikaoni kwa nguvu ilhali wale wa upande wa handisheki wakiendesha mikutano yao chini ya ulinzi wa polisi.

Katika Kaunti ya Vihiga, polisi Jumamosi walitumia vitoa machozi kuwatawanya wafuasi wa kikundi cha Tangatanga waliopanga kukutana nyumbani kwa Mbunge wa Hamisi, Charles Gimose, katika kijiji cha Simbi.

Polisi waliwalaumu wabunge hao kwa kukiuka kanuni za kuzuia kusambaa kwa virusi vya corona.

Walipokuwa wakiwatawanya wabunge hao, Waziri wa Ugatuzi Eugene Wamalwa na Gavana wa Kakamega Wycliffe Oparanya walikuwa wakiwahutubia viongozi waliokusanyika katika Chuo Kikuu cha Masinde Muliro na hawakuchukuliwa hatua.

Maafisa wa usalama walifika nyumbani kwa Bw Gimose saa moja asubuhi na kufunga njia zote za kuingia bomani humo.

Mbunge wa Mumias Mashariki, Bw Ben Washiali na aliyekuwa Seneta wa Kakamega, Dkt Boni Khalwale walifaulu kupenya hadi ndani ya makazi ya mbunge huyo.

Dkt Khalwale alianza kuwahutubia madiwani wachache waliokuwa wamefaulu kuingia lakini Mkuu wa polisi wa eneo la Hamisi, Bw Johana Chebii akaagiza warushiwe hewa ya kutoa machozi na wakalazimika kutimua mbio kwa usalama wao.

Bw Washiali aligubikwa na wingu la gesi hiyo huku Khalwale aliyekuwa amemmwagia maji mkuu wa polisi akafanikiwa kutoroka.

Alipotoka nje ya boma, Dkt Khalwale na madiwani kadhaa waliungana na wakazi kwenye barabara ya Gambogi-Jebrok na kuwarushia polisi mawe.

Dkt Khalwale aliyezungumza kwa niaba ya viongozi hao alilaumu serikali kwa kutumia nguvu kuzima mikutano ya wandani wa Dkt Ruto.

Alisema mnamo Ijumaa, Bw Oparanya aliruhusiwa kufanya mkutano mwingine pia katika Kaunti ya Vihiga. Bw Oparanya na kikundi chake wamekuwa wakifanya mikutano mingi eneo la Magharibi.

“Tulikuwa watu takriban 60 hapa na mkutano wetu umesimamishwa. Oparanya na wenzake kwa sasa wanakutana na watu karibu 2,000 Kakamega na wanalindwa na polisi,” akasema.

Katika mkutano wa Kakamega, Bw Wamalwa na Bw Oparanya walihimiza wakazi kuunga serikali na Mpango wa Maridhiano (BBI) wakiahidi miradi ya maendeleo eneo hilo.

“Kama jamii, tumeendelea kuwa katika baridi ya kisiasa kwa sababu tuko katika upinzani. Wakati huu hatutaki kurudia kosa hilo tena,” Bw Oparanya alisema.

“Ni lazima tuunge BBI mkono kwa sababu hii ndiyo njia itakayotuingiza serikalini. Tumechoka kupiga kelele katika upinzani,” aliongeza Bw Oparanya.

Wakati huo huo, viongozi wa Ford Kenya waliilaumu serikali kwa kuwahangaisha kila wanapotaka kukutana.

Katibu Mtendaji Chris Mandu Mandu alisema serikali inaonekana kuwa na nia ya kuwahangaisha wanachama, hasa wale wanaoegemea upande wa Seneta wa Bungoma, Bw Moses Wetang’ula.

Mnamo Ijumaa, viongozi wa chama hicho walikuwa wanajiandaa kukutana katika hoteli moja mjini Kakamega lakini polisi wakawasili ghafla na kuwaagiza waondoke.

“Tunahangaishwa na polisi kila tunapoandaa mikutano kujadili masuala ya chama. Polisi huvuruga mikutano yetu wakidai tunakiuka kanuni za Wizara ya Afya kuhusu Covid-19,” akasema Bw Mandu.