Michezo

UBELGIJI HAICHEKI: Yafuzu kushiriki Euro 2020

October 11th, 2019 1 min read

Na MASHIRIKA

PARIS, Ufaransa

UBELGIJI ilikuwa timu ya kwanza kutinga Kombe la Bara Ulaya (Euro 2020) baada ya kuongozwa na Romelu Lukaku kubebesha San Marino mabao 9-0 jijini Brussels mnamo Alhamisi.

Lukaku alipachika mabao mawili na kuimarisha rekodi yake ya kufungia Ubelgiji mabao mengi hadi 50, huku vijana hawa wa kocha Roberto Martinez wakifungua mwanya wa alama 11 dhidi ya nambari tatu Cyprus kwenye Kundi I zikisalia mechi tatu.

Ushindi huo wa saba mfululizo ulitunuku Ubelgiji, ambayo inashikilia nafasi ya kwanza duniani, tiketi ya kushiriki dimba la Euro 2020 litakalochezewa katika maeneo 12 kote Bara Ulaya.

Urusi imeanza kunusia tiketi ya pili ya moja kwa moja kutoka kundi hili baada ya kulipua Scotland 4-0 na kuweka pengo la alama nane kati yake na Cyprus.

Ubelgiji ni moja ya timu zitakazopigiwa upatu kutwaa taji wakati kombe hilo litaanza Juni 12 mwaka ujao.

Ushindi wa Ubelgiji dhidi ya San Marino ulitoshana na rekodi yake ya mabao tisa iliyoandikisha dhidi ya Zambia na Gibraltar mwaka 1994 na 2017 mtawalia.

“Ushindi wa mabao tisa bila jibu ni matokeo mazuri, ingawa tungetamani kuongeza bao moja ili tuvunje rekodi hiyo,” alisema mvamizi matata wa Inter Milan, Lukaku.