NA MASHIRIKA
PARIS, Ufaransa
ALIYEKUWA kocha wa klabu ya FC Schalke 04, Spartak Moscow na RB Leipzig, Domenico Tedesco ameteuliwa kuwa kocha mkuu wa timu ya taifa ya Ubelgiji.
Kocha huyo mwenye umri wa miaka 37 ambaye ni mzaliwa wa Italia mwenye uraia wa Ujerumani amesaini mkataba ambao utamwezesha kuwa usukani hadi baada ya kumalizika kwa michuano ya Euro 2024.
Amechukuwa nafasi ya Roberto Martinez aliyondoka baada ya kuwa usukani kwa miaka sita. Martinez alingatuka baada ya Ubelgiji kubanduliwa mapema katika fainali za Kombe la Dunia nchini Qatar.
“Ni jambo la kujivunia kuteuliwa kuwa kocha mkuu wa timu ya taifa ya Ubelgiji. Nitajitahidi niwezavyo kutekeleza jukumu hili kubwa,” alisema Tedesco ambaye kibarua chake cha kwanza kitakuwa kuongoza Ubelgiji kucheza na Sweden mnamo Machi 24 katika pambano la Euro 2024.
Martinez aliteuliwa kocha mpya wa timu ya Ureno mwezi uliopita, wiki chache tu baada ya kuagana na Ubelgiji ambayo iliondoka katika mashindano ya Kombe la Dunia baada ya kutoka sare 0-0 na Croatia.
Morocco iliongoza Kundi hilo la F kwa pointi saba, wakifuatiwa na Croatia waliokuwa na pointi tano, wakati Ubelgiji wakimaliza katika nafasi ya tatu kwa pointi nne.
Ubelgiji iliongoza orodha ya viwango vya kimataifa vya ubora kwa miaka mine chini ya Martinez, lakini haikuwahi kutwaa taji lolote kubwa.
Mhispania huyo aling’atuka wakati mastaa wengi wa timu hiyo wakistaafu baada ya kuchezea timu hiyo kwa miaka mingi.
Kevin De Bruyne, Eden Hazard, Romelu Lukaku na Dries Mertens ni miongoni mwa wanaotarajiwa kustaafu.
Jukumu kubwa la Tedesco ni kuhakikisha Ubelgiji imefuzu kwa fainali za Euro 2024 zitakazofanyika nchini Ujerumani.
Mbali na Tedesco, kadhalika chama cha soka kimemteua aliyekuwa mchezaji matata wa kimataifa, Frank Vercauteren kuwa mkurgenzi mpya wa michezo.
Vercauteren amesema Ubegiji ina wachezaji wengi waliojaliwa vipaji vya hali ya juu ambao watajaza nafasi za watakaoondoka.
Nchini Ureno, Martinez amechukuwa nafasi ya Fernando Santos ambaye aliongoza Ureno wakati wa fainali za Kombe la Dunia nchini Qatar.
Santos aliondoka baada ya Ureno kubanduliwa katika mechi ya kufuzu kwa nusu-fainali, kwenye pambano ambalo Cristiano Ronaldo aliingia kama mchezaji wa akiba lakini hakuweza kusaidia timu yake kufuta bao la Morocco ambalo lilisimama hadi kipenga cha mwisho.
Baada ya mechi hiyo kumalizika, Ronaldo alitoka nje ya uwanja huku akilia kwa uchungu, baada ya ndoto yake ya kuongeza medali ya Kombe la Dunia kutoweka.
Subscribe our newsletter to stay updated