Siasa

Ubinafsi unavyowasukuma wanasiasa kumezea mate Ikulu huku Wakenya wakiteseka

September 29th, 2020 3 min read

Na MOHAMED AHMED

WANASIASA wanaomezea mate kiti cha urais nchini wameanza kampeni za mapema bila kujali mahangaiko ambayo raia wanapitia hasa kwa sababu ya janga la corona lililovuruga shughuli za kimaisha.

Wanasiasa hao wanaozuru maeneo tofauti ya nchi wakipiga siasa za uchaguzi wa 2022 miaka miwili kabla ya mwaka huo kufika, wanatoa ahadi ambazo wamekuwa wakirudia kila msimu wa uchaguzi lakini hawazitimizi wanapoingia madarakani.

Naibu Rais William Ruto, na vinara wa chama cha ODM Raila Odinga, na Kalonzo Musyoka (Wiper) wamekuwa mstari wa mbele kujitia makali kwa maandalizi ya 2022.

Wengine ni Musalia Mudavadi (Amani National Congress) na magavana Machakos Alfred Mutua (Machakos), Hassan Joho (Mombasa), Mwangi wa Iria (Murang’a) na Kivutha Kibwana (Makueni).

Siasa hizo za mapema zimepelekea wanasiasa hao kuanza ubishani kuhusu baadhi ya masuala ya kitaifa huku wakieneza bila aibu ahadi ambazo wamekosa kutimiza kwa miaka na mikaka licha yao hasa Dkt Ruto, Bw Odinga na Bw Musyoka kuwa na uwezo huo serikalini.

Dkt Ruto ambaye ndiye ameonekana kufanya ziara nyingi kitaifa anatumia umaskini uliovuka mipaka nchini hasa miongoni mwa vijana akijifanya ana suluhisho la kubuni mamilioni ya nafasi za kazi na mbinu za kuwasaidia kujiinua kimaisha.

Hii ni licha ya yake kuwa Naibu Rais tangu 2013 na pia amewahi kuwa mbunge na waziri katika miaka iliyotangulia.

Kulingana na mchanganuzi wa siasa, Bw Robby Muhambi, wanasiasa wanaona kama walipoteza muda mwingi wakati kanuni za kutotagusana zilipoanza kutekelezwa kuepusha maambukizi ya virusi vya corona.

“Saa hizi kila mmoja wao analenga kuhakikisha kuwa haachwi nyuma. Wameamua kuanzisha “reggae” waliokuwa wamezimiwa kwa sababu kuna mambo mengi lazima wahakikishe yote yanaafikiwa kabla mwaka wa siasa uingie rasmi,” akasema Bw Muhambi.

Wiki mbili zilizopita, baada ya Dkt Ruto kutoka eneo la Pwani ambapo aliandamana na baadhi ya viongozi kupiga siasa za BBI na kura ya maoni, Bw Odinga alifululiza eneo hilo naye kuweka mambo sawa.

Akiandamana na Bw Joho, Bw Odinga alizuru kaunti za Taita Taveta, Kwale na Mombasa ambapo alikutana na wakazi ambao aliwaeleza umuhimu wa kukubali ripoti ya Mpango wa Maridhiano (BBI) inayolenga kurekebisha katiba.

Kwa mujibu wa Bw Odinga, ni kupitia kwa ripoti hiyo ambapo taifa litafanikiwa kuleta mageuzi yatakayobadili maisha ya umma kama vile kwa kuangamiza ufisadi, kuleta usawa kwa raia na kuzima ukabila.

Masuala haya yamekuwa katika manifesto za viongozi wanaowania urais kwa miaka mingi.

Wiki moja tu baada ya kuondoka Bw Odinga eneo hilo naye kiongozi wa Wiper Bw Musyoka alifululiza Pwani kwa ziara ya siku tatu ambapo alizuru kaunti hizo ambazo Bw Odinga alikuwa.

Katika ziara yake, Bw Musyoka alidai analenga kuleta mabadiliko makubwa kwa wakazi wa Pwani endapo atashinda katika urais.

Kwa miaka mingi, viongozi wa kisiasa wamekuwa wakiahidi kugeuza Mombasa iwe kama Dubai, suala ambalo Bw Musyoka hakuona haya kulirudia.

‘Sisi tunataka bandari ibadilishwe muundo wake na iwe huru kutumika kama vile Dubai ndipo vijana wetu waweze kupata kazi ambazo zimepotea,’ akasema jana.

Kabla kiongozi huyo kufika eneo la Pwani, Dkt Ruto tayari alikuwa ametembelea maeneo takriban sita akitangamana na watu na kupiga siasa na kueleza namna atakavyominyana na wale amabo wanataka kuzima azma yake ya kuwa rais.

Dkt Ruto ndani ya wiki mbili tayari alikuwa amezuru maeneo ya Bungoma ambapo alizuru mnamo Jumapili mbali na makanisa tofauti ambayo alikuwa ametembelea na kufika eneo la Kajiado kwa sherehe za utamaduni wa Masai.

Kando na vigogo hao, Gavana Mutua kwa upande wake naye alikutana na vijana huku akilia kuwa Bw Mudavadi ameanza kuigiza mipango yake ya kuvutia vijana kumpigia kura.

Wakati Bw Mutua alipokuwa analalamika, Bw Mudavadi naye aliwahi kufika kwenye sherehe za Wamaasai eneo la Kajiado baada ya kutembea eneo la Karatina, Nyeri ambapo alikutana na watu mbalimbali.

Kwa upande wake, Bw Joho hajaficha nia yake kuzamia siasa za kitaifa baada ya kukamilisha hatamu zake mbili za ugavana 2022.