Siasa

Ubinafsi wa vigogo sumu kwa BBI

November 15th, 2020 3 min read

Na CHARLES WASONGA

MAPUUZA ya kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga kuhusu shinikizo za makundi mbalimbali, zinazohimiza ripoti ya Mpango wa Maridhiano (BBI) ifanyiwe marekebisho kabla ya kura ya maamuzi, huenda yakasambaratisha malengo ya handisheki ya kuunganisha taifa.

Inahofiwa kuwa hatua hiyo italigawanya taifa hata zaidi kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022 kinyume na malengo ya muafaka aliyotia saini na Rais Uhuru Kenyatta mnamo Machi 9, 2018, na uliozaa mpango huo wa BBI.

Baadhi ya wadadisi wanasema kuwa huenda msimamo mkali wa Bw Odinga ukasababisha kufanyika kwa kura ya maamuzi katika mazingira ya migawanyiko mikubwa nchini, hali itakayochafua mandhari ya kisiasa wakati wa uchaguzi mkuu ujao.

Mnamo Ijumaa, Bw Odinga alizima matumaini ya wadau wanaotaka marekebisho yafanyiwe ripoti hiyo, hasa makundi ya kidini, aliposema kuwa mapendekezo na masuala mapya hayatajumuishwa katika ripoti hiyo.

Naibu Rais William Ruto na wanasiasa wa mrengo wake wa Tangatanga, makundi ya mashirika ya kijamii, watu walemavu miongoni mwa makundi mengine pia wamekuwa wakitaka ripoti hiyo ifanyiwe marekebisho ili iakisi matakwa ya Wakenya wote.

Akiongea Ijumaa afisini mwake Capitol Hill, Nairobi alipokutana na ujumbe wa viongozi kutoka Pwani, Bw Odinga alikariri kuwa nafasi ya mapendekezo mapya haipo na kwamba hatua iliyosalia ni ukusanyaji wa sahihi milioni moja zitakazowasilishwa kwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

“Viongozi wa kidini walikuwa na muda wa miaka miwili kuwasilisha mapendekezo yao kwa jopokazi la BBI. Hakuna mapendekezo mapya yatakayoongezwa katika ripoti hii. Hayo ni maoni yao, sisi tutaendelea na maoni ya wengi yaliyomo kwenye BBI,” akasema.

Isitoshe, juzi Bw Odinga alipoonekana kulegeza kamba kuhusiana na suala hilo, alifafanua kuwa ‘marekebisho’ ambayo yatafanyiwa ripoti hiyo ni ya ‘uhariri’ pekee.

“Ripoti hii haitafunguliwa tena ila ni makosa madogo tu ya uhariri ambayo yatarekebishwa ili kufafanua masuala yaliyoibuliwa na jamii ya wafugaji,” akasema baada ya kukutana na viongozi kutoka jamii za wafugaji wakiongozwa na mawaziri Ukur Yatani (Fedha) na John Munyes (Mafuta).

Kulingana Prof Macharia Munene, msimamo kama huu wa Bw Odinga unaenda kinyume na wito wa kinara mwenzake, Rais Uhuru Kenyatta, wakati wa hotuba yake bungeni kwamba Wakenya wanaunga mkono marekebisho ya Katiba kupitia BBI.

“Lakini muafaka ambao Rais Kenyatta alihimiza hauweza kupatikana wakati mwenzake ataonekana kupuuza maoni ya wadau wengine, hasa viongozi wa kidini. Mchakato muhimu kama huu wa marekebisho ya Katiba kupitia kura ya maamuzi unahitaji uwepo wa muafaka kutoka Wakenya wengi, hasa tabaka la viongozi wa kidini. Hawa ni watu wanaoongoza idadi kubwa ya Wakenya,” anasema Prof Munene ambaye ni mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Amerika, (USIU), bewa la Kenya.

Kulingana na msomi huyo, ni migawanyiko na uhasama uliochochewa na kura ya maamuzi ya 2005, iliyoshuhudia ushindani mkali, na ndiyo “iliyopanda mbegu” ya ghasia zilizogubika uchaguzi mkuu uliofuatia mnamo 2007.

Kwa upande wake, Dkt Ruto anaunga mkono kujumuishwa kwa mapendekezo ya makundi mbalimbali katika ripoti ya BBI ili “kujenga muafaka kuhusu marekebisho ya Katiba ambao unawahusu Wakenya wote”.

“Masuala yaliyoibuliwa na viongozi wetu wa kidini yana mashiko. Hakuna milango inayopaswa kufungwa; kuta zisijengwe kuzuia mawazo mazuri; hakuna kundi linalopaswa kuachwa nyuma. Tunafaa kuendelea kujenga madaraja ya kufikia muafaka. Wanawake na walemavu sharti wasikilizwe ili kujenga taifa linalojali sote pamoja,” akasema mnamo Jumanne kupitia akaunti yake ya Twitter.

Akaendelea, “Ni kinaya kuwa tunataka kufanyia marekebisho Katiba ilhali tunadinda kuifanyia marekebisho ripoti kama hii. Kuta zisijengwe kuzuia wengine huku tukijifanya kuwa tunajenga madaraja ya umoja na maridhiano.”

Dkt Ruto alionekana kukosoa msimamo wa Bw Odinga pamoja na wandani wake ambao wameshikilia kuwa ripoti hiyo haitafanyiwa marekebisho yoyote.

Lakini wabunge Otiende Amollo (Rarieda) na Jeremiah Kioni (Ndaragua) wanaunga mkono kutofanyiwa marekebisho kwa ripoti ya BBI wakisema “kura ya maamuzi haitakuwa na maana yoyote pasi upinzani.”

“Nimeshughulikia suala kama hili hapo awali na kugundua kuwa ukitoa nafasi kwa kila mtu kuwasilisha matakwa yake, hatutasonga mbele. Hata katiba ya sasa iliungwa mkono na asilimia 68 pekee ya wapigakura kwa sababu kulikuwa na wale waliopinga. Hatuwezi kupata muafaka wa asilimia 100,” akasema Bw Kioni ambaye ni mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kusimamia Utekelezaji wa Katiba (CIOC).