Michezo

UBINGWA LA LIGA: Real Madrid sasa wahitaji alama mbili tu kutokana na mechi mbili

July 14th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

REAL Madrid wanahitaji alama mbili pekee kutokana na mechi mbili zilizosalia msimu huu ili kutawazwa mabingwa wa Ligi Kuu ya Uhispania kwa mara ya kwanza tangu 2012.

Hii ni baada ya masogora hao wa kocha Zinedine Zidane kuwapokeza Granada kichapo cha 2-1 mnamo Julai 13, 2020 uwanjani Nuevo de Los Carmenes.

Beki mzawa wa Ufaransa, Ferland Mendy aliwafungulia Real ukurasa wa mabao kunako dakika ya 10 kabla ya raia mwenzake, Karim Benzema kuongeza la pili dakika sita baadaye.

Ingawa hivyo, iliwalazimu Real kuibana sana safu yao ya ulinzi kwa zaidi ya dakika 20 za mwisho wa kipindi cha pili baada ya Granada kufufua makali yao na kuonekana kuwazidi maarifa wageni wao katika takriban kila idara.

Hii ni baada ya Darwin Machis kumwacha hoi kipa Thibaut Courtois na kufunga bao lililoonekana kuwarejesha Granada mchezoni kunako dakika ya 50.

Real kwa sasa wanaselelea kileleni mwa jedwali la La Liga kwa alama 83, nne zaidi kuliko wapinzani wao wakuu Barcelona ambao ni wa pili.

Real kwa sasa wanahitaji alama mbili pekee katika mechi mbili za mwisho dhidi ya nambari tano Villarreal mnamo Alhamisi ya Julai 16, 2020 uwanjani Alfredo Di Stefano kisha ugenini dhidi ya Leganes walioko katika hatari ya kuteremshwa daraja kwa pamoja na Mallorca na Espanyol.

Kwa upande wao, Barcelona ambao wana rekodi duni dhidi ya Real msimu huu, wamepangiwa kuonana na Osasuna mnamo Alhamisi uwanjani Camp Nou kabla ya kuwaendea Alaves ugani Mendizorrotza mnamo Jumapili ya Julai 19, 2020.

Mara yao ya mwisho kunyanyua kombe ni 2016-17 ambao Zidane aliwaongoza kuwapepeta Juventus kwenye fainali ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) iliyochezewa uwanjani Millennium Cardiff, Wales.

MATOKEO YA LA LIGA (Julai 13, 2020):

Alaves 0-0 Getafe

Villarreal 1-2 Real Sociedad

Granada 1-2 Real Madrid