HabariSiasa

Ubishi baina ya Ruto na Raila wachacha

October 2nd, 2018 2 min read

Na VALENTINE OBARA

MABISHANO kati ya Naibu Rais William Ruto na Kiongozi wa Upinzani Raila Odinga yalichacha Jumanne huku kila mmoja akimkabili mwenzake kwa madai ya hujuma.

Dalili zinaonyesha kuwa chanzo cha mizozo yao ni mwafaka kati ya Bw Odinga na Rais Uhuru Kenyatta.

Wandani wa Bw Ruto wamekuwa wakishuku Bw Odinga ana nia fiche, na shinikizo lake kutaka marekebisho ya Katiba ni miongoni mwa masuala ambayo yamewafanya kuamini anatumia mwafaka huo kwa maslahi ya kujinufaisha kisiasa.

Hata hivyo, kiongozi huyo wa Chama cha ODM jana alisema hana nia mbaya na wanaomshambulia kwa maneno, na akadai wanaogopa kwa vile mwafaka wake na Rais Kenyatta umeongeza kasi katika makabiliano dhidi ya ufisadi.

“Tumeanza vita dhidi ya ufisadi na hiyo ndiyo inaleta kutetemeka. Unaona watu wanapiga kelele, wanabweka kama mbwa kwa sababu ya vita dhidi ya ufisadi. Wanaogopa,” akasema Bw Odinga alipohudhuria uzinduzi wa hospitali katika eneo la Mavoko, Kaunti ya Machakos.

Aliongeza: “Kama unajua huna hatia unaogopa nini? Usiogope Raila. Raila hana ubaya na mtu. Mimi nataka kuona mema kwa Wakenya wote kwa hivyo hii kazi itaendelea.”

Alikuwa ameandamana na Kiongozi wa Chama cha Wiper, Kalonzo Musyoka, aliyekuwa Seneta wa Machakos, Bw Johnson Muthama, miongoni mwa viongozi wengine.

Mnamo Jumapili, Naibu Rais alidai Bw Odinga anataka kuvuruga Chama cha Jubilee ili Bw Ruto aondoke na hivyo basi kutatiza azimio lake la kuwania urais.

Jana akiwa katika eneobunge la Voi, Kaunti ya Taita Taveta, Bw Ruto alimwambia Bw Odinga aache kuingiza siasa katika vita dhidi ya ufisadi.

“Katiba iko wazi. Tuna asasi huru zilizopewa jukumu la kupambana na ufisadi, uharibifu wa rasilimali na usimamizi mbaya. La muhimu zaidi, viongozi wanapaswa kujihusisha na kujadili masuala ambayo yanaweza kuleta mabadiliko Kenya badala ya kupoteza muda wao wakizungumza kuhusu watu wengine,” akasema.

Bw Ruto alianza kuchemka Jumapili kufuatia matamshi ya Kiranja wa Wachache Bungeni, Bw Junet Mohamed kwamba yeye ndiye aliyefadhili fujo zilizoshuhudiwa bungeni mwezi uliopita wakati wa kupitishwa kwa Mswada wa Fedha 2018, ambao uliweka ushuru wa asilimia nane kwa bidhaa za mafuta.

Bw Mohamed akiandamana na viongozi wengine wa ODM akiwemo Gavana wa Mombasa, Bw Hassan Joho, jana walimtaka Bw Ruto akome kumshambulia kinara wao na asubiri hadi kipindi cha kampeni za urais kitakapoanza rasmi.

“Tuko tayari kupambana naye wakati huo ukifika. Wakati wa kampeni bado. Handsheki ni kati ya Rais na Raila. Yeye si rais wala hakuwa mgombeaji,” akasema Bw Mohamed, na kuongeza kuwa Bw Ruto hapaswi kutafuta kisingizio ikiwa anataka kuhama Jubilee.

Kwa upande wake, Bw Musyoka alitoa wito viongozi waache kulaumiana na badala yake waungane.