Makala

Ubomoaji waacha nyanya,90, binti anayeishi na ulemavu wakihangaika

February 8th, 2024 3 min read

NA LUCY MKANYIKA 

UBOMOAJI wa makao ya watu 3,500 katika eneo la Msambweni, Kaunti ya Taita Taveta, umeziacha baadhi ya familia katika hali ya umaskini huku wengine wakitegemea wahisani kukidhi mahitaji yao.

Nyanya wa umri wa miaka 90 na binti yake anayeishi na ulemavu na mwenye umri wa miaka 60, wangali wanahangaika bila makao maalum mwezi mmoja baada ya nyumba yao kubomolewa katika kijiji cha Msambweni katika eneo la Voi.

Bi Saumu Kajuma na binti yake Hadija Mkamburi ni miongoni mwa maelfu ya maskwota ambao walipoteza nyumba zao na riziki zao kwa kampuni ya kibinafsi ya Sparkle Properties Limited inayodai umiliki wa ardhi yenye ukubwa wa ekari 134.

Bi Kajuma, ambaye pia amekuwa msaidizi wa Bi Mkamburi ambaye macho yake yamefifia kutokana na ugonjwa wa kisukari, alisema hawana uwezo wa kulipa kodi ya chumba walichokodisha katika eneo la Kemkesho, Voi.

Bi Hadija Mkamburi,60, akiwa eneo la Kemkesho lililoko Voi, Kaunti ya Taita Taveta. PICHA | LUCY MKANYIKA

Mnamo Jumatano walilazimika kuhamia katika eneo la Taveta baada ya wasamaria wema kuwapa nafasi ya kuishi nao wanapotafuta suluhu ya kudumu.

Akizungumza na Taifa Leo, bibi huyo alisema kuwa alilazimika kuhamia Taveta kinyume na mapenzi yake kwani alitaka kurudi nyumbani kwake ambako ameishi tangu miaka ya 1970.

“Tangu nyumba yangu ibomolewe sijawahi kutoa machozi. Siwezi amini nimekuwa ombaomba katika umri wangu huu. Nilipenda kurudi nyumbani kwangu hata kama nitafia huko ni afadhali,” alisema.

Alisema ubomozi huo umemvunja moyo mno huku asijue la kufanya na jinsi ya kusaidia mwamawe mlemavu ambaye anamtegemea.

Bi Kajuma na binti yake wamekuwa wakiishi katika chumba cha kupanga kwa mwezi mmoja uliopita lakini hawakuweza kulipa kodi ya mwezi huu.

“Marafiki zangu wametupatia chumba cha kutukimu mimi na mamangu. Siwezi kumwacha nyuma kwa kuwa yeye ndio hunisaidia na vilevile hana mahali pa kuishi. Ndio maana tumepakia vitu vyetu vya nyumbani kuhamia huko,” alisema Bi Mkamburi ambaye ni mlemavu na anatembea kwa kutumia magongo.

Bi Mkamburi alisema kuwa kutokana na ugonjwa wake, hawezi kufanya kazi za kujikimu na wanategemea tu wasamaria wema kwa msaada.

“Mimi ni binti pekee wa mama yangu baada ya dada yangu kufariki. Maisha yamekuwa magumu sana kwetu,” alisema.

Mpwa wake Asina Mwanakombo ambaye nyumba yake pia ilibomolewa alisema hawezi kuwasaidia nyanyake na shangazi yake kwani yeye pia hana uwezo wa kifedha.

Aliwasihi wasamaria wema kusaidia familia hiyo haswa kupata makao ya kudumu.

“Kidogo ninachopata najaribu kuwagawanyia lakini hakitutoshi. Nyanya bado haamini kwamba hatarudi tena nyumbani kwake pale Msambweni…anataka akaishi kwa vifusi vya nyumba yake,” alisema.

Matatizo ya familia hiyo yanajiri wakati baadhi ya maskwota ambao nyumba zao zilibomolewa, wanatafuta mbinu za kurudi mahakamani kuhusu kipande hicho cha ardhi inayozozaniwa.

Wakati huohuo, baadhi ya waathiriwa wameanza majadiliano na mwekezaji huyo kuhusu kununua ardhi ambapo nyumba zao zilikuwa zimejengwa.

Hali hiyo imezua mgawanyiko kati ya waathiriwa hao ambapo baadhi yao wamekataa chaguo la kufanya mazungumzo yoyote na mwekezaji wakisema kwamba ardhi hiyo ni ya mababu zao na hawako tayari kuiwachilia kamwe.

“Tumeishi hapa kwa miaka nyingi na hatutakubali mazungumzo yoyote na kampuni hiyo. Tunataka haki na kuipata tutarudi mahakamani,” alisema Bw Johana Ngai mmoja wa maskwota hao.

Bi Betty Tole, ambaye ni mwathiriwa mwingine, alisema mwekezaji anafaa kukutana nao katika eneo la Voi badala ya wao kusafiri hadi Mombasa kwa mikutano.

“Ni bora kutafuta haki kupitia mahakama. Ardhi ni yetu kwa hivyo, hatutakubali anachotaka,” alisema Bi Tole.

Baadhi ya matakwa ambayo yanatafutwa na familia hizo mahakamani ni pamoja na kupewa umiliki wa ardhi hiyo kwa kukaa hapo kwa muda mrefu na kutaka fidia kutoka kwa kampuni hiyo.

Walisema kuwa mahakama haikuwapa nafasi ya kujitetea na kwamba kesi iliyokamilika mwaka 2023 ilihusisha watu wanane pekee ambao hawakuwakilisha jamii nzima.

Mwaka 2023, Mahakama ya Rufaa iliidhinisha uamuzi wa Mahakama ya Mazingira na Ardhi ya Mombasa ambayo ilitoa hukumu kwamba kampuni hiyo ndio mmiliki halali wa mali hiyo.

Gavana Andrew Mwadime alisema kuwa serikali yake itaunga mkono uamuzi wa waathiriwa hao.

Alimtaka mwekezaji huyo kutembelea waathiriwa na kusikia kilio chao.

“Tayari nimefanya mkutano na waathiriwa ili kusikia maoni yao,” akasema Bw Mwadime.

Meneja msimamizi wa mali ya kampuni hiyo Bw Francis Mulili, alisema wameanza majadiliano na waathiriwa 200 ambao wako tayari kupimiwa mashamba yao.

“Milango yetu iko wazi kuwasikiliza wengine ambao wako tayari kushirikiana na sisi ili kuwapimia ardhi,” akasema Bw Mulili.

Huku mzozo huo ukiendelea kutokota baina ya maskwota hao, viongozi na mwekezaji, waathiriwa ambao hawana uwezo wa kutafuta makao mbadala wanahangaika wasijue pa kuishi.

Bw Andrea Mwailole apakia bidhaa za Bi Saumu Kajuma na bintiye Hadija Mkamburi kwa gari. PICHA | LUCY MKANYIKA