Kimataifa

Ubugiaji pombe husaidia kuzungumza lugha za kigeni kwa ustadi – Utafiti

December 11th, 2018 2 min read

MSHIRIKA na PETER MBURU

UTAFITI mmoja wa kisayansi umesema kuwa unywaji wa pombe unaweza kuwasaidia wazungumzaji wa zaidi ya lugha moja kuweza kuzungumza kwa ustadi lugha za kigeni.

Utafiti huo, hata hivyo, umeonya kuwa kunywa kupita kiasi kutaadhiri uzungumzaji huo, ukisisitiza kuwa ni kunywa kwa kiwango fulani ambako kutasaidia hali hiyo.

Utafiti huo ulisema kuwa ulevi huimarisha sehemu ya akili inayomfanya mtu kufikiria jambo kwa undani na mwili kudhibiti mwendo vyema.

Ulisema kuwa haswa sehemu ya akili ambayo hushughulika na umakinikaji, kumbukumbu na uwezo wa kutofautisha jambo zuri na baya na kuzuia kufanya jambo baya ni baadhi ya mambo ambayo pombe humfanya mtumizi kufanya.

Watafiti hao kutoka chuo kikuu cha Liverpool na King’s College London aidha walidhihirisha kuwa pombe husaidia kulegeza ulimi, na hivyo kuifanya rahisi hali ya kuzungumza lugha nyingine kwa mtumizi.

Timu hiyo ilipima namna kiwango Fulani cha utumiaji wa pombe kilimwadhiri mtumiaji haswa katika suala la kuzungumza lugha isiyo ya mama.

Wanafunzi 50 walitumiwa, wote wakiwa wazungumzaji wa Kijerumani wanaosomea chuo kikuu cha Maastricht na ambao walijifunza majuzi kuzungumza, kusoma na kuandika lugha ya Dutch.

Waliofanyiwa jaribio waligawanywa katika vikundi viwili, kimoja kikapewa kinywaji cha pombe na kingine kinywaji kisicho cha pombe.

Kiwango cha pombe kilitofautiana kulingana na uzani wa mwili. Baadaye, wote waliagizwa kufanya mazungumzo na mkazi wa asili ya Kidutch kwa dakika kadha.

Mazungumzo yote yalirekodiwa, kisha uwezo wao wa kuzungumza ukapimwa na wataalam wa lugha hiyo ya Dutch, ambao hawakuwa na ufahamu ikiwa wazungumzaji walikuwa wamekunywa pombe au la. Wazungumzaji aidha walitakiwa kujipima wenyewe.

Kwa jumla, timu hiyo iliripoti kuwa kikundi ambacho kilibugia pombe kilionekana kuzungumza vyema lugha hiyo ya kigeni, waliowakagua wakisema waliweza kutamka maneno vyema wakilinganishwa na watu ambao hawakunywa pombe.

“Utafiti wetu unaonyesha kuwa kunywa pombe kunaweza kuwa na manufaa katika utamkaji wa lugha ya kigeni kwa watu ambao wameisoma muda mfupi uliopita,” akasema Dkt Inge Kersbergen ambaye alihusika katika utafiti huo.

Lakini watafiti hao, hata hivyo, walisema kuwa kunywa pombe nyingi huenda kusiwe na manufaa hayo ya uzungumzaji mwema wa lugha ya kigeni kama ilivyoshuhudiwa katika unywaji wa pombe kidogo.