Habari

Ubunge kuokoa vigogo kisiasa

November 27th, 2020 3 min read

Na CHARLES WASONGA

MAGAVANA ambao wanahudumu kwa muhula wa pili, na wa mwisho, watalazimika kuwania nyadhifa za ubunge katika uchaguzi mkuu wa 2022 ili wawe katika nafasi bora ya kuteuliwa kwa nyadhifa za juu serikalini.

Hii ni baada ya mswada rasmi wa marekebisho ya Katiba kupitia Muafaka wa maridhiano (BBI) kutopendekeza kubuniwa kwa serikali za majimbo, ambazo baadhi ya magavana hao walipania kuongoza. Vilevile, BBI imedumisha vipengele vya katiba vinavyosema kuwa rais na magavana watahudumu kwa mihula miwili pekee.

Kulingana na mswada huo, uliozinduliwa Jumatano, Nairobi, Waziri Mkuu, manaibu wa waziri mkuu, sehemu ya mawaziri na manaibu waziri watakuwa wabunge, tofauti na hali ilivyo sasa ambapo mawaziri hawapaswi kuwa wabunge.

Baadhi ya magavana 22 watakaostaafu 2022, walikuwa wameweka matumaini yao kwa marekebisho haya ya Katiba, kwamba wangepata mwanya wa kuwania nyadhifa za magavana wa majimbo.

Wengi wao waling’amua kuwa nafasi ya kuwania urais au kuwa mgombea-mwenza 2022 utakuwa finyu.

Mapema mwaka huu, magavana Wycliffe Oparanya (Kakamega), Ali Hassan Joho (Mombasa) na Amason Kingi (Kilifi) walitetea kubuniwa kwa serikali za majimbo, kwa kile kilichofasiriwa kama nia ya kuendeleza kuwa na ushawishi wa kisiasa. Magavana hao, ambao awali walikuwa wametangaza nia ya kugombea urais, walitoa mapendekezo hayo wakati wa mikutano ya hamasisho kuhusu BBI katika uwanja wa Tononoka (Mombasa) na ule wa Bukhungu (Kakamega).

Wakili wa masuala ya kikatiba, Bw Bobby Mkangi anasema kuwa japo wadhifa wa ubunge unaonekana kuwa wenye hadhi ya chini kuliko ugavana, mswada wa BBI sasa umeufanya kuwa kivutio kwa magavana watakaokamilisha kipindi chao cha kuhudumu 2022.

“Kuna uwezekano mkubwa kwamba baadhi ya magavana, wanaohudumu muhula wa pili na wa mwisho, watalazimika kuwania nyadhifa za ubunge ili wazitumie kucheza karata zao za kuteuliwa katika nyadhifa za Waziri Mkuu, manaibu wa waziri mkuu, mawaziri na manaibu wa mawaziri. Hii ni kwa sababu wengine wao hawataki kusalia katika baridi ya siasa baada ya kuondoka afisini,” akasema kwenye mahojiano na Taifa Leo jana Alhamisi.

Kauli sawa na hii ilitolewa na mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Herman Manyora, aliyesema kuwa haitashangaza kuona baadhi ya magavana wanaotaka kuwania urais, wakiendea nyadhifa za ubunge kama ‘daraja’ la kukwea juu serikalini.

“Ukweli ni kwamba mswada wa BBI umewaacha magavana wanaohudumu kipindi cha pili katika hali ya kujikuna kichwa hasa baada ya wazo la kubuniwa kwa serikali za majimbo kutupiliwa mbali. Kwa hivyo, itawalazimu kuwania nyadhifa nyingine kuanzia ubunge, useneta na hata urais ili waendelee kuwa na usemi katika ulingo wa siasa,” akasema Bw Manyora, mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Nairobi.

Alisema kuwa pendekezo la kubuniwa kwa maeneobunge mengine 70 zaidi litawafaa zaidi magavana hawa 22 kupata nafasi za kushindania nafasi hizo mpya.

Orodha ya kaunti 28 zilizogawiwa maeneobunge hayo mapya ina kaunti 15 zilizo na magavana wanaohudumu kwa awamu ya pili.

“Kwa mfano, Bw Oparanya anaweza kuwania kimojawapo cha viti viwili vya maeneobunge yatakayobuniwa katika Kaunti ya Kakamega. Naye Bw Joho anaweza kuwania katika mojawapo ya maeneo matatu mapya ambayo yatabuniwa katika Kaunti ya Mombasa endapo mswada wa BBI utapitishwa na Wakenya katika kura ya maamuzi,” akaeleza Bw Manyora.

Hata hivyo, wachanganuzi hao wanaonya kuwa magavana watakaowania nyadhifa za ubunge kwa lengo la kuteuliwa mawaziri watakuwa na kibarua kikubwa kujinadi kwa wapigakura.

Kulingana na Bw Mkangi, itabidi waweke matumaini yao kwa uwezekeno wa chama au muungano watakaotumia kisiasa kushinda urais katika Uchaguzi Mkuu.

Hivi majuzi, Gavana Oparanya, ambaye pia ndiye Mwenyekiti wa Baraza la Magavana (CoG), alitangaza kuwa hatastaafu siasa baada ya kipindi chake kukamilika ila atapigania kiti cha kitaifa.

Hata hivyo, mwanasiasa huyo ambaye alikuwa akiongea katika Shule ya Upili ya Shiatsala, eneobunge la Butere, hakufichua wadhifa atakaopigania.

“Kipindi changu cha kuhudumu kama gavana kinakamilika 2022. Nimeamua kuwa sitaenda nyumbani lakini nitaendelea kupambana katika siasa za kitaifa. Sijui ni kiti kipi, lakini ninaamini kuwa nitakuwa katika meza ambako keki ya kitaifa inagawanywa,” akasema.

Magavana wengine wanaohudumu muhula wa pili na wa mwisho ni pamoja na Jackson Mandago (Uasin Gishu), Sospeter Ojaamong (Busia), Martin Wambora (Embu) na Paul Chepkwony (Kericho).

Wengine ni Josephat Nanok (Turkana), Mwangi wa Iria (Murang’a), Okoth Obado (Migori), Samuel Tunai (Narok), James Ongwae (Kisii), Alex Tolgos (Elgeyo Marakwet) miongoni mwa wengine.