Makala

AKILIMALI: Ubunifu kupunguza gharama ya ufugaji samaki

August 25th, 2019 3 min read

NA RICHARD MAOSI

Kaunti ya Nakuru imeanzisha mradi wa kufuga samaki wengi kwa gharama nafuu ikilenga wakulima wadogo kutoka mashinani.

Mradi wenyewe unahusisha utumiaji wa vidimbwi vya maji katika kipande cha ardhi mita 2 kwa 4 na kila kidimbwi kinaweza kufugiwa zaidi ya samaki 500 kwa wakati mmoja.

Tayari wamepata mashiko kwa kuangalia maslahi ya mkulima mdogo, bila kujali endapo anatoka mjini wala kijijini, mradi anaweza kujifundisha teknolojia hii nyepesi isiyofahamika na wengi.

Kulingana na Shirika la Kimataifa la Chakula na Kilimo (FAO), uharibifu wa mazingira ya asili huweka usalama wa chakula cha binadamu hatarini, na kuzua haja ya kutengeneza vidimbwi katika makazi ya watu kukabiliana na changamoto za kupata lishe ambayo ni salama.

Muundo wa kisasa kufugia samaki unaotumia mbao, karatasi na paneli za sola ambao ni bei nafuu kuanzisha. Picha/ Richard Maosi

Kuanzishwa kwa mradi wa samaki kunanuia kupanua ufugaji wa ufugaji, ikiaminika kuwa bado watu wengi wanategemea mbuzi, ng’ombe na kondoo kwa nyama.

Akizungumza na Akilimali, BwElijah Sulai, mtaalamu wa samaki katika Wizara ya Kilimo kwenye Kaunti ya Nakuru, anasema kwa takriban kwa mtaji wa Sh10,000, mkulima anaweza kununua mbao, karatasi ya kutandaza ndani ya kidimbwi na mabomba ya kuhakikisha kuwa maji safi yanaingia na kutoka kwenye kidimbwi.

“Atakachohitaji zaidi ni ujuzi wa kuunganisha vifaa hivi kwa ustadi katika hatua ya kutengeneza vidimbwi,” anasema.

Aidha paneli za sola zitakuwa za manufaa ili kuzalisha nguvu ya kusukuma maji, yaliyotumika kutoka ndani ya kidimbwi hadi shambani ambapo mkulima anaweza kuyatumia kunyunyizia mimea yake maji.

Mkulima anaweza kunyunyizia mboga zake maji kutokana na maji ya kidimbwi. Picha/ Richard Maosi

Kwanza Elijah Sulai anasema kuwa samaki wanapenda kuishi ndani ya maji ya kijani kibichi ambayo haijakolea kupita kiasi.

Anatoa tahadhari kwamba endapo rangi ya kijani kibichi itakolea sana inaweza kuwanyima samaki hewa safi ya oksijeni,na miale ya jua kuwafikia

Anasema samaki ni bidhaa ambayo inazidi kudidimia ulimwenguni kwa sababu ya uharibifu wa vyanzo vya maji na chemichemi zake, aidha uchafuzi wa maziwa na mito ni pigo kubwa kwa viumbe hawa.

Ni kwa sababu hiyo bei yake imepanda zaidi ya maradufu chini ya kipindi cha miaka mitano iliyopita kwa zaidi ya asilimia 100.

Unaweza kutumia vidimbwi vidogo ama vikubwa muradi azingatie kanuni zote zinazohitajika katika ufugaji wa samaki. Picha/ Richard Maosi

Kupitia utafiti anawashauri wakulima kunyunyizia maji mbolea ya Ammonia (DAP) ili iweze kupata rangi ya kijani kibichi mazingira ambayo samaki wengi hupataa nafuu kuishi humo.

Pili anasema baada ya maji hayo kutumika yanaweza kusukumwa shambani ili kuongeza rutuba mchangani, na wala hapana haja ya mkulima kununua mbolea kwa ajili ya mimea yake.

Muundo wenyewe ukiwa tayari mkulima anaweza kununua samaki wadogo(vifaranga wa samaki) kisha akawahifadhi ndani ya vidimbwi ambavyo huwa vimekaribiana mita mbili hivi.

“Lishe ya samaki ni jambo la muhimu ambalo mkulima anastahili kuzingatia, kwanza anaweza kupanda aina ya mimea ya zoo planktons inayosaidia kusafisha hewa majini,pia lishe kwa samaki,”akasema.

Wakulima wakipata ujuzi namna ya kutengeneza vidimbwi vya kisasa kwa kutumia mbao. Picha/ Richard Maosi

Hii ikiwa ni mojawapo ya shughuli za kukwamua sekta ya uvuvi kupitia umuhimu wake kuinua uchumi wa nchi.

Ikumbukwe kaunti ndogo ya Naivasha ndiyo inategemewa katika uzalishaji samaki hadi mapema mwaka huu ilipopigwa marufuku kutokana na idadi ndogo ya samaki wanaopatikana.

“Pia tumeanzisha mradi wa kufuga samaki ili kuhakikisha watu hawategemei samaki kutoka kwa vyanzo tu vya maji kama mitoni bali pia wanaweza kujizalishia bidhaa hii majumbani mwao,”akasema.

Mafunzo kabambe yakiendelea. Picha/ Richard Maosi

Alieleza kuwa tatizo la kulisha samaki bado ni changamoto kubwa inayowakumba wakulima kutoka humu nchini, ambapo wengi wao wamekuwa wakilisha samaki wao kupitia njia duni.

Wakulima wanashauriwa kuchanganya malighafi yanayoweza kupatikana kwenye mazingira yao kuzalisha chakula, kwa mfano mihogo,dagaa waliosagwa,maharagwe na mahindi.

“Mbali na kutumia unga wa samaki,samaki wanahitaji lishe yenye kiwango kikubwa cha protini mbali na lishe za kawaida kama vile kabohidreti na vitamini,” Elijah anaongezea.

“Samaki hulishwa kulingana na uzito wake ili kupunguza uharibifu wa lishe zinazoweza kufanya maji kuchafuka,” Elijah anasema.

Kulingana naye anasema samaki wakitunzwa vizuri kwa kupatiwa chakula cha kutosha,maji safi na mazingira bora wanaweza kuchukua muda mfupi sana kukomaa na kuwa wenye faida nyingi kwa mkulima.

Samaki aina ya tilapia wanaweza kufugwa kwa wingi katika sehemu ndogo ukilinganiswhwa na aina nyingine ya samaki wanaohitaji nafasi kubwa ili kuzaana kama vile mbuta na kamongo.

Elijah Sulai akionyesha jinsi mkulima anaweza kutumia paneli za sola kunyunyizizia mimea maji. Picha/ Richard Maosi

“Mara nyingi baada ya miezi sita mkulima anafaa aweze kupata mavuno ya kwanza kwa ajili ya mauzo,”akasema.

Hata hivyo Elijah anaona kuwa jambo la manufaa sana ni endapo mkulima, anaweza kumiliki vidimbwi ili kuendeleza mradi wa kufuga samaki pasipo kukoma.

Hii itampatia fursa nzuri ya kuendeleza mradi wake pindi anapowavuna samaki kutoka kidimbwi kimoja abakishe akiba kwenye vidimbwi vingine kwa ajili ya manufaa ya baadaye.

Kulingana naye bei ya samaki mmoja ni baina ya Sh300-Sh400 kwa hivyo mfugaji anaweza kutengeneza baina ya Sh60,000 – Sh70,000 kwenye kidimbwi kimoja kila baada ya miezi sita.

Iwapo mkulima atamiliki jumla ya vidimbwi 10 anaweza kutengeneza baina ya Sh600,000 -Sh700,000 kila baada ya miezi sita.

Elijah anawashauri wakulima kuzamia kwenye miradi kama hii ili kuwatengenezea vijana nafasi nyingi za ajira na kuleta njia mbadala ya kupata protini katika lishe.

Pia anashauri kaunti nyinginezo kote nchini kutumia maonyesho ya kilimo kuhamasisha jamii katika maswala kama haya yatakayowasaidia kujiongezea kipato.