Makala

UBUNIFU: Otieno atengeneza karatasi kwa kutumia magugumaji

March 12th, 2020 2 min read

Na RICHARD MAOSI

MAGUGUMAJI yana faida nyingi kinyume na ilivyofikiriwa na baadhi ya jamii zinazotegemea uvuvi kutoka kwenye maziwa maarufu nchini kama vile Victoria, Naivasha na Ziwa Baringo.

Hata hivyo mmea huu ambao ni kero kwa wavuvi mjini Kisumu, umetengeneza nafasi za ajira miongoni mwa vijana wanaotumia magugu-maji kutengeneza karatasi kwa ajili ya matumizi mbalimbali.

Matumaini ya kupata samaki ziwani huathiriwa kwa sababu ya magugu maji, yanayowanyima samaki wa kutosha. Aidha, idadi ya watalii katika ziwa Victoria inaendelea kushuka, kwani mashua haziwezi kupenya baina ya mmea huu.

Hali ni kama hiyo kwa Michael Otieno kijana mwenye umri wa makamo mkaaji wa mtaa wa Mamboleo kilomita 7 hivi kutoka mjini Kisumu, ambaye anamiliki kiwanda cha kutengeneza bidhaa kutokana na magugu-maji.

Kulingana naye, gugumaji linaweza kutumiwa kutengeneza viti, vikapu, bayogesi, kuzalisha kawi na pia mbolea, akiongezea kuwa hii ni fursa kwa serikali kuwekeza katika mradi huu ambao unaweza kuwainua vijana mashinani.

Alikatiza masomo yake mnamo 2000 kutokana na ukosefu wa karo, kisha akajiunga na mashirika ya kibinafsi ambapo alijifundisha taaluma ya kutengeneza karatasi na samani.

Hatimaye aliamua kujiajiri 2004 ili kuisaidia jamii yake kukabiliana na kero ya magugu-maji katika ziwa Victoria. Alilenga kutengeneza nafasi nyingi za ajira miongoni mwa vijana mbali na kuwa balozi wa kuyahifadhi mazingira.

Kwa mtaji wa 10,000 alinunua mitambo ya Pestel inayotumiwa kupaka rangi, penseli, fremu na kulipia umeme katika karakana yake ndogo ya kuendesha ufundi ambayo inapatikana mbali na makazi ya watu.

Ni kawaida yake angalau kila siku za wiki kutembea katika ziwa Victoria na kukusanya magugu-maji ambayo hukatwa vipande vipande, kuchemshwa, kukaushwa na baadaye kuandaa karatasi.

Hatimaye vipande vya magugu-maji hukaushwa kabla ya kulowekwa ndani ya maji kwa saa 24 hivi , kabla ya kuopolewa na sasa huwa tayari kuongezewa thamani.

Alieleza Akilimali kuwa mchanganyiko huu huchujwa ili kutenganisha mawe, vidudu na mategu ili abakishe magugu ndani ya maji safi ambayo ndio hutumiwa kutengeneza karatasi.

“Magugu-maji hukaushwa kwenye fremu maalum za umbo la mstatili, ili chembechembe za magugu-maji zilizokaushwa ziweze kushikamana vyema,”akasema.

Kwa mujibu wa Otieno yeye hushirikisha makundi ya kijamii mara nyingi ili kuwasaidia kupigana na janga la magugu maji, wengi wao wakiwa ni wafanyabiashara wanaotegemea uvuvi kukidhi maslahi yao ya kila siku.

Anasema wavuvi kwa ada maalum wamekuwa wakimsaidia kukusanya magugu-maji kwani wana uwezo wa kufikia kina kirefu cha ziwa ili kuyakusanya magugu maji ya kutosha.

Ingawa dhoruba ya maji wakati mwingine ni kali kupita kiasi, upepo na mawimbi makali yanaweza kusukuma magugu-maji mbali na ufuo wa ziwa, jambo linalowapa wavuvi kazi ya ziada kuopoa magugu maji.

Kutokana na magugu-maji, Otieno anasema anaweza kutengeneza bidhaa nyingi kama vile kadi za mialiko, karatasi za kawaida, mifuko ya kubebea bidhaa pamoja pamoja na kufanya maandishi kwenye karatasi.

Otieno anasema amefanikiwa kuwaajiri jumla ya vijana watano ambao humsaidia katika shughuli za kila siku wakati wa kuyaongezea magugu maji thamani.

Utaalamu wa kutengeneza karatasi kutokana na magugu-maji umemsaidia kuzuru mataifa kadhaa ndani na nje ya Afrika, ili kuwaelimisha wakazi kuhusu namna ya kuyalinda mazingira.

“Septemba mwaka uliopita nilishiriki kwenye warsha nchini Ghana ambapo niliwafundisha namna ya kujipatia kipato kutokana na magugu-maji” asema.

Mafanikio

Mnamo 2012 alishiriki katika mashindano ya Green Innovation Award, kwa hisani ya Net Fund ambapo aliwasilisha bidhaa zake katika hatua ya kujitafutia soko pana hadi katika kiwango cha kimataifa.

Kisha 2013 Otieno anasema aliteuliwa kushiriki katika kitengo cha wajasiria mali, kwa jina National Commission Science and Technology ambapo alipata tuzo iliyomsaidia kuongeza mtaji katika karakana yake ya kufanyia kazi inayopatikana mtaani Mamboleo.

Otieno anasema amefanikiwa kustawisha kiwanda chake, cha kutengeneza karatasi za A1 ambazo huuzwa kwa shilingi 150 katika kila umbo la mstatili.

Hivi sasa fremu zake zimebeba jumla ya karatasi 800.