Makala

Uchafu kwenye mazingira ulivyozidisha athari za mafuriko mitaani

May 15th, 2018 3 min read

Na SAMMY KIMATU

MVUA ni baraka na Wakenya wamekuwa wakiiomba inyeshe baada ya kushuhudiwa mahangaiko yaliyosababishwa na ukame na kiangazi kwa muda mrefu.

Wakati huo wa kiangazi, mito ilikauka, maua yakanyauka, mifugo wakafa na waliosalia wakakonda kama ng’onda.

Watu walilaumiwa, tetesi zikiwa ufisadi na wafisadi kuongezeka katika biashara ya kuuza makaa, sambamba na ya mbao.

Kuna viongozi wa kisiasa, kwa mfano aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga aliyesema watu wamevamia na kukata miti katika Mlima Mau eneo la Rift Valley.

Alitoa kauli yake kwamba wanaoishi maeneo hayo ya msitu huo ambao ni moja katika ile kubwa nchini kwa kuvuta mvua wahamishwe.

Lakini alipingwa sana na wapinzani wake wa kisiasa waliodai watu wao wanalengwa na kuonewa.

Lisilobidi hubidi. Hali hii ya kiangazi ilisukuma idara husika kuchukua hatua ya dharura kuokoa misitu ndipo waziri wa mazingira na misitu Bw Keraiko Tobiko akapiga marufuku ukataji miti kwa muda wa miezi mitatu.

Baada ya maombi makanisani, masokoni na misikitini Maulana alete mvua, hatimaye mvua imenyesha katika kaunti zote 47 tangu Machi.

Ajabu ni kwamba mvua hii ya masika iliyongojewa kwa hamu na ghamu imekuja na athari zake- mafuriko.

Katika vyombo vya habari tumesoma magazetini, kusikiza redioni na kutazama runingani watu na wanyama wakifariki pia baada ya kuporomokewa na nyumba. Mifano michache ni kama vile:- mkasa wa Solai (Nakuru) ambapo watu zaidi ya 40 walikufa baada ya bwawa la Solai kupasuka.

Kaunti za Murang’a na Makueni kuliripotiwa maporomoko yaliyowaacha wengi bila Makao.

Kaunti zingine ambazo wakazi waliathikika ni Tana River, Homa Bay, Nakuru, Isiolo, Moyale, Taita Taveta, Kilifi, Lodwar na Garissa.

Katika Kaunti ya Nairobi, kila kukinyesha, wanaoathirika zaidi ni wakazi kwenye mitaa ya mabanda iliyoko South B (Eneo bunge la Starehe), Mukuru-Kwa Reuben (Embakasi South) Kingstone na Lunga Lunga (Makadara)

Machi mwaka huu, shule nane zilifungwa kufuatia mafuriko yaliyokatiza masomo. Miongoni mwao ni Shule ya Msingi ya Brightstar, ya upili ya Brightstar, SDA Little Kids, New Dawn, Community Initiative and Bridge International – shule ya Upili ya Viwandani na ya msingi ya St Elizabeth miongoni mwa zingine.

Wakazi mitaani ya mabanda ya Mukuru- Fuata Nyayo, Mukuru-Kaiyaba, Mukuru-Hazina na Mukuru-Maasai hawakusazwa na janga hilo.

Nyumba zilisombwa na maji, vibanda na vyoo vikabomoka, vioski vikaingiwa na maji huku mali ya thamani isiyojulikana ikiharibika.

Mitaa yote hii imo kando ya mto Ngong. Uchunguzi uliofanywa na Taifa Leo ulibaini kwamba maji katika Mto Ngong hukosa mkondo baada ya wanyakuzi kujenga nyumba na kuta jambo linaloubana mto hivyo kunyima mto njia ya kupitisha maji.

 

Daraja limezibwa na taka

Kijijini Kaiyaba, hasa katika daraja la Kaiyaba/Hazina hapa utakuta rundo la taka kutoka kwa wenyeji na mlima wa taka zinazotupwa kutoka kwa kampuni kadhaa na kuziba daraja hilo.

Kukinyesha, taka hiyo huziba maji ndiposa nyumba hufurika licha ya mvua kuwa sio nyingi katika mtaa wa Kaiyaba na Hazina.

Takriban mita 500 kutoka katika daraja hili utakutana na bomba la kupitisha maji machafu linaloziba takataka upande wa chini na kulazimisha maji kufurika katika kijiji cha Maasai.

Taswira wakati huu ni kwamba nyumba zilizojengwa karibu na mto zilibomolewa na maji kutoka upande wa nyuma na mabati yakabebwa na maji.

Zingine huwa zoimejengwa juu ya magunia yaliyotiwa mchanga jambo linalolazimisha mto kubanika na maji kubadilisha mkondo.

Ilibidi mkuu wa tarafa ya South B, Bw Barre Ahmed na maafisa kutoka kwa Halmashauri ya Kusimamia Masuala ya Mazingira (NEMA) kuingilia suala la unyakuzi wa mto.

“Takataka iliyokuwa imeziba mto imezolewa na kwa wakati huu maji hupita vizuri na hatujapokea ripoti ya mafuriko katika vijiji vyetu tena licha ya mvua nyingi kunyesha mwezi Machi na Aprili,” Bw Barre akasema.

 

Onyo

Bw Barre ametoa wito kwa yeyote atakayepatikana akitupa taka ndani ya mto Ngong atakamatwa na kushtakiwa kwa mujibu wa sheria.

Awali, mwakilishi wa wodi ya LandMawe, Bw Herman Azangu alikuwa akileta tinga tinga kuzoa taka punde ikiziba mto kabla ya mvua kunyesha ili aokoe watu kutokana na mafuriko.

Mtaani Kingstone, wanyakuzi wa ardhi wamebadilisha mkondo wa maji baada ya kumwanga milima ya mchanga na kujenga nyumba huku maji ya mto yakilazimika kupitia katiika uga wa shule ya Msingi St Elizabeth.

Utawala wa shule kupitia Mkurugenzi Mkuu, Mtawa Mary Killeen wameomba serikali kuchukulia wanyakuzi hao hatua kali kwani kunyeshapo hulazimika kufunga shule hadi maji yatakapoisha.

“Ni shule ya kisasa iliyogharimu wahisani kutoka serikali ya ujerumani mamilioni ya pesa,” Mtawa Mary akasema.