Habari

Uchafu Mto Ngong waharibu sifa ya Nairobi

August 28th, 2020 2 min read

Na SAMMY KIMATU

MRADI wa kusafisha na kuboresha mazingira ya mito jijini Nairobi haujafaulu jinsi ilivyotarajiwa kwa sababu uchafuzi umeongezeka vile vile unyakuzi wa kingo za mito husika.

Aidha, aliyekuwa Waziri Mkuu, Bw Raila Odinga na waziri wa zamani wa Mazingira, marehemu Bw John Michuki mnamo mwaka 2008 walizindua mradi wa Sh2.5 bilioni kuokoa mito ya Nairobi.

Siku hiyo, kwenye hafla hiyo iliyofanyika katika Taasisi ya Mafunzo ya Utawala Nchini Kenya (KIA), Waziri Mkuu aliagiza Bw Michuki atumie njia zote kubomoa zaidi ya vibanda 16,046 zilizojengwa katika kingo za mto. Bw Raila alikuwa ameongoza kamati ya mawaziri 17- wakati wa uzinduzi huo.

Zaidi ya miaka kumi baadaye, hakuna chochote kilichobadilika.

Jumatano wiki hii, kulikuwa na taka tele katika Mto Ngong unaopitia katika mitaa ya Mabanda ya Mukuru ipatao zaidi ya kumi.

Uchafuzi huo wa mazingira huchagiwa na wenyeji mitaani kutupa taka ndani ya mto.

Mwaka 2019 Mamlaka ya Kitaifa ya Kuhifadhi Mazingira (Nema) iilifanya msako wa kampuni na viwanda vilivyokuwa vikichafua mazingira kwa kuelekeza maji machafu ndani ya mito.

Baadhi ya kampuni zilijipata pabaya baada ya mkono wa sheria kuwanasa.

Zingine zilifungwa kwa kufofuata sheria na kanuni zilizowekwa kuhusu uchafuzi wa mazingira.

Jumatano, kwenye mtaa wa mabanda wa Mukuru-Kaiyaba katika kaunti ndogo ya Starehe, wakazi walionekana wakitupa taka kwenye Mto Ngong sehemu ya daraja la Kaiyaba / Hazina.

Taka hizo ni pamoja na mifuko ya plastiki, sodo, maganda ya mboga na matunda, vipande vya magondoro, katoni, mabaki ya vyakula, chupa na vipande vya nguo miongoni mwa uchafu mwingine.

Maji machafu ya Mto Ngong. Picha/ Sammy Kimatu

Isitoshe, sehemu zingine za mto ambazo hutumiwa kama maeneo ya kutupa taka ni pamoja na Daraja la Mukuru Commercial/Fuata Nyayo, Kvukio cha Mukuru-Fuata Nyayo / Kenya Wine,daraja linalopakana na ua wa Shule ya Msingi ya St Catherine.

Eneo lingine ni katika daraja la linalounganisha mtaa wa mabanda wa Mukuru-Maasai / daraja la Express miongoni mwa maeneo mengine yam to huo yaliyoelekea chini.

“Mto ulikuwa safi sana wakati wa Mradi wa Kazi kwa Vijana. Tulikuwa na vijana wa kushika doria usiku dhidi ya wale waliotupa au kumwaga taka mtoni wakati wa usiku,” Bw Christopher Lunalo Mandevu alisema.

Mbali na hilo, wanyakuzi wa ardhi wamenyakua kingo za mto na kusababisha mto kuwa mwembamba.

Mwaka 2019 afisa wa mazingira kutoka kaunti ndogo ya Starehe alilia wakati akikagua hali ya mto Ngong katika maeneo kadhaa ya mtaa wa South B.

Wakati huo, alikuwa ameambatana na naibu kamishna wa Starehe, Bw Boen Kibet.

Wawili hao walipeana ilani ya kubomoa makazi yote yaliyojengwa kando ya mto, na tangu wakati huo, hamna mabadiliko yaliyofanyika fauka ya ilani kutolewa katika mkutano na wakazi wa mitaa ya mabanda ya iliyo katika tarafa ya South B.

Baadaye, Bw Boen alihamishiwa. Agosti 26, 2020, bwanyenye mmoja anayedaiwa kumiliki msururu wa nyumba kadhaa katika Kaunti ya Nairobi alikuwa akipanua nyumba yake kuelekea mtoni Ngong karibu na daraja la Mukuru-Maasai.

Vibarua zaidi ya watano walikuwa kazini wakipanga magunia yaliyojazwa mchanga wakiyapanga taratibu kisha wajenge nyumba za kukodisha.

Kuongeza chumvi kwenye donda sugu, kliniki kadhaa hutumia mto kutupa sindano na glavu zilizotumiwa miongoni mwa vifaa vingine vya matibabu.

Vilevile, kila mwezi visa vya vijusi kutupwa ndani ya mto Ngong huripotiwa katika mitaa ya Mukuru.

Shirika moja lisilo la serikali mkabala wa barabara ya Likoni lijulikanalo Mukuru Promotion Centre (MPC) limeathiriwa vibaya na shughuli haramu katika mto huo hususan katika eneo la Express katika eneo la Viwanda.

Mkurugenzi Mkuu wa MPC, Mtawa Mary Kileen alisema mradi wa MPC husaidia watu masikini wanaoishi katika maeneo ya Mukuru .

Mitaa hiyo ni pamoja na mtaa wa mabanda wa Mukuru-Kayaba, Mukuru-Kwa Reuben na mtaa wa Mukuru- Lunga Lunga.

Mitaa hii imo katika kaunti ndogo ya Starehe, Embakasi Kusini na Makadara mtawaliwa.