Uchaguzi 2022 ni lazima – Ruto

Uchaguzi 2022 ni lazima – Ruto

Na BENSON MATHEKA

NAIBU Rais William Ruto amepuuza wito wa kuahirishwa kwa uchaguzi mkuu ujao, akitaja pendekezo hilo kama kelele zitakazopita, na uchaguzi mkuu ujao ufanyike kwa amani.

Dkt Ruto alisema kwamba wanaopendekeza uchaguzi mkuu uahirishwe wanaharibu wakati kwa sababu ni lazima uchaguzi mkuu ufanyike Agosti 9, 2022 ilivyopangwa.

“Ninataka kuwaambia Wakenya msiwe na wasiwasi, msitishwe. Kenya hii ni ya Mungu. Tutakuwa na amani kutoka sasa hadi 2022. Hizi kelele mnazosikia zitapita na uchaguzi wa 2022 utafanyika kwa amani,” akasema Dkt Ruto.

Dkt Ruto alisema kwamba Mungu ataipa nchi hii viongozi watakaochukua usukani 2022.

“Maneno haya mengi ni mipango tu ya siasa. Na nyinyi si wageni kwa mambo ya siasa. Itapangwa hivi na vile na mambo yataenda sawasawa kwa sababu tuko na Mungu,” alisema.

“Msitutishe eti huenda kukaenda vingine na kuharibika. Hakutaharibika kwa sababu tunaamini Mungu na ni Mungu wa amani,” alisema.

Dkt Ruto alisema Mungu ni wa mipango na hivyo basi ni lazima Kenya isonge mbele kwa kuzingatia mipango iliyowekwa. Baadhi ya wanasiasa wanaounga Mpango wa Maridhiano (BBI) wamekuwa wakipendekeza uchaguzi mkuu ujao uahirishwe hadi kura ya maamuzi ya kubadilisha katiba iliyosimamishwa na Mahakama Kuu itakapofanyika.

Waandalizi wa mchakato huo wamekata rufaa wakitaka uamuzi huo ubatilishwe huku baadhi yao wakijitokeza wazi kusema kuwa iwapo rufaa haitaamuliwa kwa wakati, itabidi uchaguzi mkuu uahirishwe hadi refarenda ifanyike.

Mswada wa marekebisho ya katiba wa 2020, unapendekeza kubuniwa kwa wadhifa wa waziri mkuu na manaibu wake wawili na kubuniwa kwa maeneobunge mapya 70 miongoni mwa mabadiliko mengine ya kikatiba na usimamizi.

Dkt Ruto amekuwa akipinga mchakato wa kubadilisha katiba akisema Wakenya wanahitaji kuwezeshwa kiuchumi na si marekebisho ya katiba yenye madhumuni ya kubuni nafasi kwa wanasiasa wachache.

Wiki mbili zilizopita, Katibu Mkuu wa Muungano wa Vyama vya wafanyakazi nchini (Cotu), Francis Atwoli alisema kuwa itabidi uchaguzi mkuu uahirishwe kwa mwaka mmoja au miwili hadi katiba irekebishwe kupitia Mswada wa BBI.

Akizungumza akiwa katika kanisa la AIC Bomani, Kaunti ya Machakos jana, Dkt Ruto alisema baadhi ya kauli zinazotolewa na wanasiasa zinalenga kutia hofu Wakenya.

“Kutakuwa na amani Kenya kabla na kwenye uchaguzi mkuu wa 2022. Msibabaishwe na kelele hizi mnazosikia,” alisema Dkt Ruto.

Katika kauli inayoonekana kumlenga kiongozi wa chama cha ODM, Raila Odinga aliyekemea viongozi wa kidini na kuwataka wakome kuingilia masuala ya siasa, Dkt Ruto aliwaambia serikali inatambua wajibu wao.

Viongozi wa kidini wamepinga wito wa kuahirishwa kwa uchaguzi mkuu ujao.

“Serikali ya Kenya inatambua na inajihusisha na ushirikiano kati ya kanisa na serikali. Kuna mambo mengi ambayo kanisa hufanya kusaidia yale ambayo serikali inapaswa kufanya,” alisema Dkt Ruto.

“Kwa sababu hiyo, viongozi wa kanisa wanafaa kufahamu kwamba kama serikali tunatambua mnayofanya,” akiongeza Dkt Ruto.

Aliwataka viongozi wanaokosoa kampeni yake ya kuwawezesha maskini almaarufu ‘Hustler’, kwa kupanga miungano ya kisiasa kumkabili kwenye uchaguzi mkuu wasaidie wanyonge hao kwanza.

“Ninataka kuwaomba wanasiasa, na nimesikia wengi wakipanga miungano ya kukabili wapinzani wao, hata tunapounda miungano ya kumenyana na wapinzani, tusisahau wasiojiweza,” alisema.

Alisema kwamba wanasiasa wanafaa kufahamu kwamba wananchi ni muhimu kuliko viongozi.

You can share this post!

Jinsi ya kuandaa tosti mayai

NYABOLA: Vyama vilikiuka sheria ya faragha-data, viadhibiwe