Uchaguzi 2022: Ruto, Raila wafuatana kwa karibu kura zikiendelea kujumlishwa

Uchaguzi 2022: Ruto, Raila wafuatana kwa karibu kura zikiendelea kujumlishwa

NA MWANDISHI WETU

KUFIKIA saa mbili na dakika 20 usiku wa Jumatano, Agosti 10, 2022 Naibu Rais Dkt William Ruto wa United Democratic Alliance (UDA) alikuwa akiongoza kwa kujizolea kura 3,542,291(asilimia 51.20) huku akifuatwa kwa karibu na Raila Odinga wa Azimio La Umoja-One Kenya aliyepata kura 3,330,461 (asilimia 48.14).

Matokeo hayo ni kwa mujibu wa data iliyokusanywa na timu ya kujumlisha matokeo ya Form 34A zilizowekwa kwenye tovuti ya IEBC lakini tu zile ambazo Nation Media Group (NMG) imeshapakua na kuzitathmini.

Tathmini hii inatokana na jumla ya kura 6,917,899 ambazo kikosi cha NMG kimeshaziangazia.

Wagombea George Wajackoyah (Roots Party) na David Waihiga (Agano) wamepata kura 29,390 na 15,757 mtawalia. Kura za wawili hao zinawakilisha asilimia 0.42 na 0.23 za wapigakura.

Matokeo hayo kufikia sasa yanaangazia tu vituo 22,578 kati ya jumla ya 46,229 ambavyo Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) imeainisha kisheria.

Matokeo yanaweza kubadilika kadri timu ya NMG inavyoendelea kujumlisha kura za wagombea wote wanne.

Wakenya walipiga kura jana Jumanne, Agosti 09, 2022.

  • Tags

You can share this post!

Ujumlishaji kura Kieni waendelea IEBC ikitarajia shughuli...

NGUVU ZA HOJA: Jinsi Kiswahili kilivyotumiwa na wanasiasa...

T L