Uchaguzi mdogo wa useneta Machakos mtihani kwa umaarufu wa Kalonzo

Uchaguzi mdogo wa useneta Machakos mtihani kwa umaarufu wa Kalonzo

Na BENSON MATHEKA

Uchaguzi mdogo wa kiti cha useneta katika Kaunti ya Machakos utakuwa mtihani kwa umaarufu wa vyama na vigogo wa kisiasa eneo la Ukambani, wadadisi wanasema.

Kiti hicho kilibaki wazi kufuatia kifo cha wakili Bonface Kabaka aliyefariki baada ya kuugua kwa muda mfupi. Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) imetangaza kwamba uchaguzi mdogo utafanyika Machi 23.

Ingawa marehemu Kabaka alichaguliwa kwa tiketi ya Chama Cha Uzalendo (CCU), kinyang’anyiro cha kujaza kiti hicho kinatarajiwa kuwa kati ya vyama vya Maendeleo Chap Chap (MCC) cha Gavana wa kaunti hiyo, Dkt Alfred Mutua, Wiper cha aliyekuwa makamu wa rais Kalonzo Musyoka na United Democratic Alliance (UDA) kinachohusishwa na aliyekuwa Seneta wa Machakos, Bw Johnstone Muthama.

Tayari Maendeleo Chap Chap imemteua aliyekuwa waziri John Mutua Katuku kupeperusha bendera ya chama hicho kwenye uchaguzi huo mdogo na inasemekana kuwa Wiper inanuia kumkabidhi tiketi Bw Jackson Kala ambaye alishindwa na marehemu Kabaka kwenye uchaguzi mkuu wa 2017.

Bw Muthama ambaye alihama chama cha Wiper anataka UDA ambayo inahusishwa na Naibu Rais William Ruto, imsimamishe aliyekuwa naibu gavana wa Machakos Benard Kiala. Inasemekana wabunge washirika wa Dkt Ruto eneo la Ukambani wanataka aliyekuwa mbunge wa Kathiani Peter Kaindi kupeperusha bendera ya UDA.

Wadadisi wanasema ingawa UDA ilisajiliwa majuzi, inaweza kuwa mwiba kwa vyama vya Wiper na Maendeleo Chap Chap, si tu katika uchaguzi mdogo huo bali katika eneo zima la Ukambani kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

“Uchaguzi mdogo wa useneta katika Kaunti ya Machakos utakuwa mtihani kwa umaarufu wa vyama na viongozi wa kisiasa eneo la Ukambani. Lakini kwa kuzingatia idadi ya wawaniaji ambao UDA kimevutia, ni wazi kitapatia Wiper na Maendeleo Chap wakati mgumu sana,” asema mdadisi wa siasa John Kisilu.

Chama hicho kimevutia wawaniaji kumi wakiwemo Kiala, Kaindi, mfanyabiashara wa Nairobi Gilbert Maluki na mwanasiasa Patrick Mathuki.

Wengine ni aliyekuwa diwani wa wadi ya Matungulu Magharibi Magdaline Ndawa, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Nairobi, John Musingi, mtaalamu wa masuala ya Bima, Bw Urbanus Ngengele, Titus Ndambuki na mwanasiasa Winfred Mutua ambaye pia aliwania kiti hicho kwenye uchaguzi mkuu wa 2017.

Kulingana na Bw Kisilu, ushawishi na ukarimu wa Bw Muthama huenda ukanufaisha chama cha UDA ikiwa kitamsimamisha mgombeaji maarufu. Inasemekana kuwa ingawa Bw Muthama anamuunga Bw Kiala, wabunge washirika wa Dkt Ruto wanasema Bw Kaindi ndiye aliye na nafasi ya kuwabwaga wapinzani.

“Muthama anataka kudhihirisha kwamba ndiye jogoo wa siasa za Ukambani lakini itategemea na atakayepeperusha bendera ya chama hicho ikizingatiwa kwamba Wiper kingali chama maarufu eneo hilo na Dkt Mutua wa Maendeleo Chap Chap angali na ushawishi akiwa gavana wa Kaunti ya Machakos,” asema Kisilu.

Anasema UDA inaweza kushinda uchaguzi huo mapema iwapo Muthama atagombea kiti hicho.Dkt Mutua amekuwa akitaka kumbandua Musyoka kama msemaji wa jamii ya Wakamba naye Muthama amekuwa akijigamba kuwa umaarufu wa Wiper ulizimika alipokihama baada ya kutofautiana na Bw Musyoka mnamo 2017.

Muthama alijiunga na Dkt Ruto na ameapa kufadhili wagombeaji wa viti mbalimbali eneo la Ukambani kwenye uchaguzi mkuu ujao. Kulingana na mchanganuzi wa siasa za Ukambani, Silas Mutuku, uchaguzi mdogo wa useneta ktika Kaunti ya Machakos utaamua ni nani aliye maarufu katika eneo hilo.

“Ninaamini Wiper ingali maarufu Ukambani kwa sasa kwa kuwa ina idadi kubwa ya Wabunge na madiwani. Hata hivyo, wimbi la kisiasa linabadilika na uchaguzi mdogo wa useneta wa Machakos utaweka umaarufu wa chama hicho kwenye mizani. Ikiwa kitashinda, itakuwa pigo kwa Muthama na washirika wa Dkt Ruto Ukambani na iwapo UDA itashinda, itakuwa pigo kwa Wiper,” asema.

Bw Musyoka anaamini kwamba Wiper kitashinda uchaguzi huo kwa kura nyingi. “ Kuna kelele nyingi za watu wanaodai eti watashinda. Hatuna wasiwasi kwamba kiti hicho ni chetu. Propaganda zao zitaambulia patupu,” asema Bw Musyoka.

Kulingana na Bw Kisilu, ushindi wa UDA utaimarisha umaarufu wa Dkt Ruto eneo hilo na kudhihirisha Muthama kuwa jogoo wa siasa Ukambani.

You can share this post!

Pigo kuu kwa Raila Uhuru akishindwa kudhibiti Mlima Kenya

Matokeo ya uchaguzi mdogo Kwale yalivyowapa maadui wa Joho...