Habari Mseto

Uchaguzi wa wakurugenzi KTDA wakumbwa na utata

October 17th, 2019 2 min read

Na NDUNG’U GACHANE na IRENE MUGO

UTATA umeibuka kuhusu mtindo wa upigaji kura kwenye uchaguzi wa Oktoba 25 wa wakurugenzi wa viwanda 65 vya wakulima wadogowadogo wa majanichai ambao ni wanachama wa Mamlaka ya Kilimo cha Majanichai Nchini (KTDA).

Uchaguzi huo unatimia wakati sekta ya majanichai inaendelea kukumbwa na matatizo tele na baadhi ya wakulima kuanza kung’oa mimea yao kutokana na bonasi ndogo wanayolipwa.

Wakurugenzi ambao watachaguliwa wanatarajiwa kuongoza kampuni hiyo kwa muda wa miaka mitatu huku wale wanaoshikilia vyeo hivyo kwa sasa pia wakipewa nafasi ya kuvitetea.

Hata hivyo, tofauti kubwa imeibuka kati ya wakulima wenye hisa chache kutokana na kumiliki vipande vidogo vya mashamba na wale wenye hisa nyingi na wanaomimiliki mashamba makubwa kuhusu mtindo wa upigaji kura.

Wakulima wadogo wanataka kila moja wao aruhusiwe kupiga kura kivyake huku mabwenyenye wakitaka idadi ya hisa itumike kuamua orodha ya watakaoshiriki kura hiyo.

“Kwa sasa wakulima wadogowadogo hawana usemi wowote kuhusu namna viwanda vya majanichai vinavyoendeshwa. Hii ni kwa sababu kura zimekuwa zikipigwa kutokana na idadi ya hisa ya kila mkulima. Juhudi zetu za kurai bunge la seneti kurekebisha sheria yetu ya uchaguzi zimegongwa mwamba,” akasema Bw Peter Wambugu mmoja wa wakurugenzi wa KTDA.

Wakulima hao pia wamekuwa wakipigania kupunguzwa kwa idadi ya hisa zinazohitajika kwa mwaniaji kuchaguliwa kama mkurugenzi kutoka hisa 5,000 hadi 1,000 ili kuwaruhusu wakulima wadogo kushiriki uchaguzi huo.

Sheria kutoa mwongozo

Hata hivyo, maafisa wa KTDA ambao wanaunga mkono kigezo cha idadi ya hisa kutumika kwenye uchaguzi huo wanasema mamlaka hiyo ni kampuni ya binafsi na sheria zake ndizo hutoa mwongozo wa upigaji kura kwa kutumia kiwango cha hisa.

“Huwezi kuvilinganisha vyeo vya KTDA na vile vya kisiasa. Tunaongozwa na kifungu cha sheria za kampuni na ni bunge pekee ambalo linaweza kubadilisha sheria hizo,” akasema Francis Macharia ambaye ni mwanachama wa bodi ya KTDA.

Baadhi ya mambo ambayo wakulima wanapigania ni kuongezwa kwa kiasi cha fedha kinacholipwa kwa kila kilo kutoka Sh16 hadi Sh20 kila mwezi.