Uchaguzi wafanyika kundi maarufu likisusia

Uchaguzi wafanyika kundi maarufu likisusia

NA MASHIRIKA

ALGIERS, Algeria

RAIA wa Algeria jana walipiga kura katika uchaguzi uliosusiwa na kundi maarufu linalopinga vikali shughuli hiyo na kudhihakiwa na wengi.

Misukosuko ya kisiasa, kushuka pakubwa kwa mapato ya mafuta pamoja na janga la virusi vya corona imetatiza pakubwa mageuzi mengi yaliyoahidiwa na serikali iliyochukua usukani baada ya maandamano ya raia yaliyomshinikiza aliyekuwa Rais Abdelaziz Bouteflika kujiuzulu 2019.

Kauli mbiu ya mwaka huu ilikuwa “unataka mabadiliko, piga kura yako,” huku serikali ikihofia kurejelewa kwa historia ambapo idadi ndogo ya raia wanaojitokeza imekuwa ikishuhudiwa katika chaguzi za hivi majuzi.

Wagombea zaidi walijitokeza kushinda ilivyowahi kushuhudiwa mbeleni kutokana kwa kiasi fulani na sheria mpya kuhusu ufadhili, na kwa mara ya kwanza, katika uchaguzi wa Algeria, nusu ya wagombea ilijumuisha wanawake.

Matokeo ya uchaguzi yanatarajiwa kufikia kesho (Jumatatu).Huu ni uchaguzi wa tatu kufanyika katika taifa hilo ambalo ni kubwa zaidi Afrika tangu Rais

Bouteflika alipobanduka mamlakani, baada ya mamia ya watu kushiriki maandamano ya kitaifa dhidi ya azma yake ya kugombea awamu ya tano afisini huku wakiitisha mwisho wa ufisadi na uteuzi wa viongozi kwa misingi ya kirafiki.

Mrithi wake Abdelmadjid Tebboune alisema kura hii mpya ya kuwachagua wabunge 407 utakomesha utawala wenye “ufisadi” na kuweka msingi kwa Algeria mpya.Kwa wanaoikosoa serikali, shughuli ya mabadiliko haijafanyika kwa kasi ya kutosha.wakihoji kwamba viongozi wale wale ndio wanaoshikilia mamlaka nchini humo.

Hata hivyo, sheria mpya zinamaanisha kuwa wabunge waliohudumu mihula miwili au zaidi moja kwa moja walizuiwa kugombea tena.Wagombea zaidi ya 1,200 waliohusika katika “shughuli na malipo ya kutiliwa shaka” walifutiliwa mbali kushiriki kinyang’anyiro hicho na tume ya uchaguzi.

Wafadhili wa kigeni pia walipigwa marufuku huku wagombea huru wenye umri wa miaka 40 kwenda chini wakinufaika kutokana na mikopo ya serikali ya Sh243, 326 za kufadhili kampeni zao.Kutokana na sheria mpya, zaidi ya nusu ya wagombea wote walikuwa wawaniaji huru hali iliyofanya chama kuorodhesha idadi ndogo zaidi kwa mara ya kwanza.

Wachanganuzi hata hivyo, walisema kuwa wagomeba kadhaa maarufu wa chama waligeuza jambo hilo kujinufaisha kwa kusimama kama wawaniaji huru.“Kufanya chaguzi si suluhisho kwa matatizo yetu,” alisema Samir Belarbi wa kundi maarufu linalofahamika kama ‘Hirak’, lililomg’atua mamlakani aliyekuwa Bouteflika.

Hirak haina kiongozi rasmi, anwani wala nambari ya simu lakini matakwa yake ni wazi na hayabadilika – inataka mfumo wote wa siasa ufutiliwe mbali.

  • Tags

You can share this post!

Hatukutengewa fedha za referenda, IEBC yafafanua

Aliyetishia kumuua mpenziwe ahukumiwa