Uchambuzi: Jubilee ni chama imara au kigae?

Uchambuzi: Jubilee ni chama imara au kigae?

Na SAMMY WAWERU na MWANGI MUIRURI

MRENGO tawala wa Jubilee (JP) ungali imara na thabiti licha ya matukio yanayoonekana kufanyika, hivi ndivyo anavyohisi kiongozi wa wengi katika bunge la seneti Kipchumba Murkomen, anayesema JP ina zaidi ya wapigakura 8 milioni ‘waliokiweka chama’ mamlakani na wanaendelea kuongezeka kutokana na utendakazi wake.

Bw Murkomen alisema Rais Uhuru Kenyatta na Naibu wake Dkt William Ruto ambao ndio vinara wakuu, wana uhusiano wa karibu na wa kipekee.

“Vinara wetu wana uhusiano bora na hata katika utendakazi. Jubilee kwa sasa imeungana sawasawa kuliko tulivyoianzisha,” alisema Murkomen.

Alisema kiongozi wa taifa ana imani na naibu wake na ndio maana 2018 alimuamrisha kuwa akizunguka mashinani kukagua miradi ya maendeleo.

Akizungumza Jumatano kwenye mahojiano na runinga ya Citizen makala ya JKL Jumatano usiku, seneta huyu wa Elgeyo Marakwet alisema matamshi ya Rais akiongea kwa lugha yake ya mama siku kadhaa zilizopita hayakulenga viongozi wa kundi linalomuunga mkono Ruto bali yalinuia kuzima wanaoendesha ‘siasa duni’ badala ya maendeleo.

“Ndio Rais alikuwa ameghadhabika lakini hasira zake hazikulenga Jubilee ila ni viongozi wa mirengo yote wanaofanya siasa badala ya maendeleo. Hamaki tulizoshuhudia tunazichukulia kama upendo kwetu. Ni sawa na baba anayeona mambo katika boma lake hayafanyiki ipasavyo, hivyo basi lazima awake ili kuyalainisha. Sisi kama wanachama hatuna shida na matamshi hayo,” alifafanua Bw Murkomen.

Tangu salamu za maridhiano kati ya Rais Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga mnamo Machi 9, 2018, maarufu kama Handshake, chama cha Jubilee kimeonekana kugawanyika kwa makundi mawili; Kieleweke linalounga mkono Rais na Tanga Tanga linaloegemea upande wa Naibu Rais Dkt William Ruto.

Kundi la Ruto limekuwa likitilia shaka Handisheki na kuhoji ni njama ya kuzima azma ya Dkt Ruto kumrithi Rais Kenyatta 2022.

Katika hafla ya maombi ya dhehebu la Akorino inayofanyika kila mwaka, na ambayo 2019 ilifanyika Kasarani mnamo Juni 16, Rais Kenyatta kwa lugha ya Gikuyu alionekana kupandwa na mori, akilenga viongozi wanaojikita kwa kile alitaja ‘siasa duni’ Mlima Kenya.

Kiongozi wa taifa alisema atafanya ziara mbalimbali eneo hilo ili kuwazima, akiahidi kumwaga mtama njama zao. Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na Dkt Ruto.

Rais alisema wanaofanya siasa wanalemaza juhudi zake za maendeleo pamoja na lengo la kuunganisha taifa.

Kwa mujibu wa mkataba wa JP 2013, Dkt Ruto anapaswa kuunga mkono Rais Kenyatta kwa kipindi cha muda wa miaka 10, ambapo 2022 kiongozi wa taifa ataidhinisha naibu wake kumrithi.

Kulingana na seneta Murkomen ni kwamba njia rahisi ya Rais kufanikisha azma ya Naibu wake kumrithi ni kwa kuafikia maendeleo ambayo wawili hao waliahidi Wakenya walipoungana.

“2022 Jubilee itafanya kampeni kwa msingi wa rekodi ya utendakazi wake. Ifahamike, Ruto hatawania urais kama kiongozi kutoka tabaka la Kalenjin, ila kama Mkenya,” alisema.

Akieleza kauli yake kuhusu tetesi za njama ya kumuua Naibu Rais, taarifa ambayo imetawala vichwa vya habari nchini, Murkomen alisema ni suala linalopaswa kuchukuliwa kwa uzito.

Kiongozi huyu wa wengi seneti alisema mlalamishi ni serikali, ambapo idara ya upelelezi wa jinai (DCI) inasema Rais Kenyatta ndiye aliagiza uchunguzi ufanywe kuhusu madai hayo.

Idara hiyo pia inasema Naibu Rais alimpigia simu DCI George Kinoti kumfahamisha njama hiyo.

Habari hii ilichipuka mnamo Jumatatu ambapo mawaziri watatu kutoka Mlima Kenya na ambao ni Peter Munya wa Biashara na Viwanda, Joe Mucheru ICT na Waziri wa Afya Bi Sicily Kariuki, walitakiwa kuhojiwa na DCI kuhusu madai hayo.

Inadaiwa, mawaziri hao pamoja na wa Uchukuzi, James Macharia, na makatibu kadhaa, walifanya mkutano wa faragha katika La Mada Hotel ulioko kwa nia ya kumuua Naibu Rais.

Hata hivyo, waziri Munya amepinga vikali madai hayo, akisema walikutana ili kujadili maendeleo ya eneo la Mlima Kenya.

Anamtaka Dkt Ruto kuandikisha taarifa na DCI. Ni suala ambalo limeibua hisia mseto kutoka kwa baadhi ya viongozi wanasiasa eneo la Mlima Kenya.

Bw Murkomen alisema kuwa viongozi wa jamii mbalimbali nchini hufanya mikutano kujadili maendeleo ya maeneo yao, lakini haifanywi kwa usiri. “Kwa mfano, jamii ya Kalenjin hukutana na baadaye tunahutubia waandishi wa habari. Tunaskia mkutano wao hawakuruhusiwa kuingia na simu, ni yapi hayo yalikuwa yakijadiliwa?” alishangaa seneta huyo.

Alionya kuwa madai ya njama kumuua Naibu Rais yanapaswa kuchukuliwa kwa uzito na yanayoweza kuleta mgawanyiko nchini, akipendekeza mabunge yote mawili, kitaifa na la seneti, kuandaa vikao kulijadili.

Uhai wa Ruto unatumika kutekeleza mapinduzi ya usemi ndani ya Jubilee?

Sula la madai ya njama ya kumwangamiza Ruto limechambuliwa na wadadisi wa kisiasa kuwa lililo na uwezo wa kutekeleza mapinduzi ya kiusemi ndani ya chama tawala cha Jubilee dhidi ya Rais Uhuru Kenyatta.

Inasemwa kuwa jinsi habari hizo za njama hiyo zimepambwa na kuachiliwa kwa umma inaonyesha waziwazi kuwa mrengo wa DP Ruto uko katika vita vya kiubabe na mrengo wa Rais Kenyatta katika ule mpangilio asili wa United Republican Party (URP) na The National Alliance (TNA).

Muungano wa vyama hivi ukiwakilisha kwa kiwango kikuu jamii za Kalenjin na Agikuyu ndio uliishia kutwaa mamlaka ya kiutawala mwaka wa 2013 kwa manufaa ya UhuRuto na ikawa ndiyo merikebu ya kurejea kwa awamu ya pili mamlakani katika chaguzi mbili za 2017.

Sasa, mhadhiri wa somo la Sayansi ya Siasa, Gasper Odhiambo anasema madai kuwa Ruto anapangiwa njama ya kuuawa na wandani wa mrengo wa Rais Uhuru Kenyatta ni sawa na kudai kuwa Rais analenga kumwangamiza Naibu wake.

Anasema kuwa kwa sasa hoja kuu ni kuwa waliotajwa kuwa katika njama hiyo ni wandani wa dhati wa Rais Kenyatta na wa kutoka jamii yake na ambao wamewajibishwa majukumu nyeti ya kiserikali ya kumpa rais nembo ya kumbukumbu pendwa akiondoka afisini 2022.

“Ukiangalia mawaziri Sicily Kariuki (Afya), Peter Munya (Biashara na Viwanda), James Wainaina Macharia (Uchukuzi na Miundo mbinu na pia Nyumba) na Joe Mucheru (Teknolojia ya Habari na Mawasiliano), utapata kuwa watatu wao wamewajibishwa wizara zinazoshughulika na Ajenda Nne Kuu za Rais Kenyatta,” anasema Odhiambo.

Ajenda hizo ni Afya kwa wote (Bi Kariuki), Ustawi wa Kiviwanda (Munya), utoshelevu wa makao kwa wote (Macharia) hiyo nyingine ikiwa ni chakula cha kutosha kuwepo (Mwangi Kiunjuri ambaye hajatajwa katika sakata hii).

Bw Odhiambo anaongeza kuwa Mucheru ndiye anaaminiwa na Rais kushirikisha uafikiaji wa miradi na mawasiliano kwa umma, hivyo basi kuweka taswira tosha kuwa wandani wa Rais ndio wanahusishwa na njama ya kudaiwa kutaka kumuua Ruto.

Umma kupoteza imani kwao

Anasema kuwa lengo kuu katika madai haya ni kuwafanya wanne hao kupoteza imani ya umma, waangaziwe kama wakatili ambao wako katika njama za uhalifu mkuu na hatimaye wang’atuke kutoka nyadhifa zao na ikiwezekana, wahukumiwe kunyongwa au maisha gerezani kama watashtakiwa na kupatikana hatiani.

Ni mtazamo ambao Munya, ambaye amewajibishwa kuwa msemaji wa washukiwa hao kwa msingi kuwa taaluma yake ni uwakili, anakubaliana nao akisema kuwa “haya madai si ya haki kwetu kama mawaziri kwa kuwa sio tu ya kutuharibnia sifa bali ni ya kutugeuza kuwa sawa na majambazi.”

Tayari, wandani wa Ruto wameanza kuweka shinikizo washukiwa hao watimuliwe kutoka nyadhifa zao huku kukizuka hofu kuwa uhasama utakaofuatana na madai haya utaathiri uwiano ndani ya baraza la mawaziri.

“Hawa mawaziri wakikutana katika mkutano wa rais, na ambapo naibu wa Rais huhudhuria, wataweza kuwajibikia majadiliano kuhusu huduma kwa Wakenya au watakuwa na ule uhasama wa kutengana kwa msingi kuwa kuna wauaji na wanaolengwa kuuawa katika baraza hilo?” anahoji mbunge wa Kiharu, Ndindi Nyoro.

Nyoro anasema kuwa “hufai kuwa mtaalamu wa kisayansi kuelewa kuwa madai haya sio tu ya kutenganisha baraza kla mawaziri bali pia yanalenga kutenganisha uhusiano kati ya Rais na naibu wake.

Anasema kuwa binadamu ni binadamu na hadi sasa, Ruto amelalamika kwa mkubwa wake ambaye ni Rais kuwa anapangiwa kuuawa na mawaziri ambao wako katika mkutano huo wa baraza la mawaziri Rais akiwa ndiye mwenyekiti na ambapo hadi wakati kutaonekana kujituma kuchukukulia suala hili kwa uzito unaofaa, basi baraza hilo ni kigae tukiwa na waigizaji wa umoja wa kiserikali.

Mbunge wa Bahati, Kimani Ngunjiri anasema kuwa kwa sasa utengano ndani ya serikali umeingia na umeletwa na ukosefu wa kinidhamu ndani ya serikali, “tukianza na baraza la mawaziri.”

Anasema kuwa Munya tayari amesuta Ruto “kama anayecheza siasa za kipuuzi akilenga kujizolea umaarufu wa kuhurumiwa.”

Munya akiwa mfuasi wa chama cha Party of National Unity (PNU) na ambaye anahudumu ndani ya chama cha Jubilee kama waziri amekuwa akihusishwa na usaliti ndani ya serikali na sio sadfa kuwa mrengo wa Ruto umemchukulia kama kinara wa upangaji njama hiyo ya mauaji.

Bw Odhiambo anasema kuwa kwa sasa wandani wa Ruto wanawachukulia wandani wa Rais Kenyatta kama walio na njama mbovu ya ushindani.

“Hatari kuu kwa sasa ni Ruto akumbane na ajali (Mungu amjalie usalama wake) ya kumuathiri kimaisha. Itakuwa ni ishara tosha kuwa njama hiyo ilikuwa na wa kulaumiwa sio mwingine bali ni mrengo wa Rais. Rais hadi sasa hajazungumzia suala hilo na hilo lina hatari yake kwa kuwa wandani wa Ruto watachukulia kama ama ni mwoga, hajali au anakubaliana na wanaodaiwa kupanga njama hiyo,” anasema.

Ni katika hali hiyo ambapo Bw Odhiambo anasema kuwa “haya ni mapinduzi ya kiusemi na ambapo ikiwa rais Kenyatta hatacheza kadi zake kisawasawa za kisiasa, atajipata ndani ya sakata hii akiwa aidha mshirika kwa kutozungumza kupinga au kuunga, kufuta mawaziri hao au kujitokeza na ushahidi wa uchunguzi wa kutupilia madai hayo kama njama mbovu ya kisiasa na ambayo msukumo wake ni hila za kukatana miguu.”

Bw Odhiambo anasema kuwa ikiwa itaibuka kuwa madai hayo hayana msingi wowote, basi kwa kuwa Ruto ndiye anadaiwa kuwa aliyatoa kwa Rais na vitengo vya kiusalama, “basi Rais atajipata katika njia panda ya kutakiwa amfute kazi Ruto na ambapo atakumbana na athari kuu na hasi za kikatiba na kisiasa katika jaribio hilo.”

Kwa upande wake, Ruto akijaribiwa kwa kufutwa kazi, Odhiambo anasema Rais Kenyatta atajipata katika hatari nyingine ya kupoteza wengi wa ufuasi wake ndani ya utawala, apoteze imani ya wengi ambao watamuona kama msaliti wa urafiki wa kufaana ikizingatiwa jinsi ambavyo Ruto “alimsaidia kutwaa urais.”

Katika hali hizo zote, Bw Odhiambo anasema: “Kwa asilimia 100 ongeza lakini sio upunguze, suala hili ni la kimapinduzi na Rais Kenyatta yuko katika njia panda kisiasa.”

You can share this post!

UONGEZEAJI THAMANI: Kiwanda kipya cha maziwa ya ngamia...

AKILIMALI: Siri ya kufaulu katika ufugaji ng’ombe wa...

adminleo