Makala

UCHAMBUZI: Viongozi Mlima Kenya wajipanga kurithi nafasi ya usemaji kisiasa

September 14th, 2019 2 min read

Na NDUNGU GACHANE

WANASIASA Mlima Kenya wanazidi kung’ang’ana kujiweka katika nafasi nzuri kujaza mwanya utakaoachwa na Rais Uhuru Kenyatta baada ya kustaafu hapo mwaka 2022.

Siasa za urithi wa usemaji kisiasa zimesababisha mpasuko kushuhudiwa.

Baadhi ya wanasiasa ambao yaelekea wanamezea mate nafasi hiyo ni Mbunge wa Gatundu Kusini Bw Moses Kuria, Gavana wa Kaunti ya Murang’a Mwangi wa Iria, mwenzake wa Kirinyaga Bi Anne Waiguru (hupenda kuitwa Anne Kamotho tangu ahalalishe ndoa yake na Wakili Kamotho Waiganjo), mwaniaji wa zamani wa urais Bw Peter Kenneth na Waziri wa Biashara na Ustawi Kiviwanda Bw Peter Munya.

Huku Bi Waiguru akijitahidi kuwa msemaji wa Mlima Kenya na mtetezi sugu wa handisheki, Bw Munya anajiandaa kuongoza siasa za eneo hilo nao Bw Kuria na Bw Iria wamesajili vyama vya kisiasa ambavyo watatumia kama ngazi ya kupanda kwa meza ya kuamua atakayemrithi rais.

Bw Kenneth anasubiri kuona mambo yatakavyokuwa ili kukwepa mitego ya kisiasa iliyomponza hapo 2013 na 2017. Hata hivyo, anaaminika kuwa mfadhili mkuu wa mrengo wa Kieleweke.

Gavana Iria ambaye ndiye gavana wa pekee aliyechaguliwa tena 2017, amesajili chama ambacho kimejenga taswira ya mtetezi wa mwananchi wa kawaida kwa kukosoa sera hasi kama kupigwa marufuku kwa matatu jijini Nairobi na Gavana Mike Sonko.

Chama hicho, Civic Renewal Party (CRP) kilisajiliwa na wandani wa Bw Iria kimekuwa kikisajili wanachama ndani na nje ya Mlima Kenya.

Bw Iria Mr Iria hutumia kaulimbiu ya ‘Hapa Kazi Tu’ (No Wira Tu) kwa chama hicho na hii imemnasia wafuasi wengi.

Chama hicho kimekuwa kikitekeleza miradi ya kuwasaidia wakazi, hali ambayo imeboresha maisha yao.

Bw Iria alikuwa kiongozi wa pekee wa Jubilee aliyeongoza kampeni za uchaguzi wa pili wa urais baada ya mahakama kufuta uchaguzi wa kwanza 2017, na kutoa magari 300 yaliyobandikwa karatasi zenye maneno ‘Taifa La Jubilee’ na kueneza ujumbe huo akimpigia kampeni Rais Kenyatta. Alitumia fursa hiyo kujitambulisha kitaifa.

Bi Waiguru naye anatumia uelewa na tajriba yake ya miaka mingi katika uongozi wa kiserikali, kutoka Wizara ya Fedha hadi aliposimamia Wizara ya Ugatuzi.

Kwa sasa ameielewa barabara lugha ya Gikuyu na amesikika akitema methali na maneno ya wasia kwa lugha hiyo katika juhudi zake za kuunga mkono handisheki ya Rais Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga kwa kile kilitajwa ni manufaa ya Mlima Kenya.

Ana mpango wa kushirikiana na wanasiasa wote kutoka eneo hilo, bila kujali mirengo yao ya kisiasa kama Kieleweke, Tangatanga na Team Hema ya Bw Kuria.

Kwa uopande wake, Bw Kuria ametangaza rasmi nia yake ya kuwania urais 2022 na tayari ashaanza kufanya mikutano kote mlimani kusaka umaarufu.

Amenukuliwa akikejeli mirengo ta Tangatanga na Kieleweke akisema makundi hayo ni tisho kwa umoja wa Mlima Kenya.