Makala

UCHAMBUZI: Viongozi waeleza ni kipi kinafaa kufanywa kuimarisha sekta ya viwanda

June 14th, 2019 3 min read

Na SAMMY WAWERU

BAADA ya kuchaguliwa kuhudumu awamu ya pili na ya mwisho 2017, Rais Uhuru Kenyatta alizindua mpango aliosema anataka Wakenya wamkumbuke kwa angalau mambo manne ambayo ni makao ya bei nafuu, kuwepo kwa chakula cha kutosha, matibabu bora kwa wote na kwa bei nafuu pamoja na uundaji wa viwanda.

Ili kutatua suala la ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana nchini na ambalo limekuwa donda ndugu, ujenzi wa viwanda unapigiwa upatu.

Kila mwaka vijana hufuzu na kutuzwa vyeti mbalimbali vya masomo kutoka taasisi za juu za elimu; vyuo vikuu, vyuo anuwai na vyuo vya kiufundi.

Nafasi za kazi Kenya ni finyu, na wengi wa waliofuzu wameishia kuwekeza katika biashara na kilimo na ufugaji.

Baadhi ya viongozi na wachanganuzi wa masuala ya kiuchumi wanasema ujenzi wa viwanda utafanikishwa kikamilifu ikiwa serikali itashirikisha wawekezaji wa humu nchini.

Wanasema hili litaafikiwa wakipewa motisha kwa kuwapiga jeki kifedha.

“Mataifa yaliyoimarika katika sekta ya kampuni na viwanda kama China na Korea Kusini, serikali hupiga jeki wawekezaji wake wa ndani kwa ndani. Viwanda tunavyoongea kuhusu vitajengwa na sisi wenyewe, Kenya tukiiga mkondo huo suala la ukosefu wa kazi litatatuliwa,” anasema Ndindi Nyoro, mbunge wa Kiharu.

Kulingana na mbunge huyu ambaye pia ni mwekezaji, Kenya ina vijana na hata wazee wenye ujuzi katika sanaa na ambao wakiinuliwa wataweza kubuni viwanda vya kutengeneza bidhaa.

Katika makadirio ya bajeti mwaka wa kifedha wa 2019/2020 iliyosomwa Alhamisi  na Waziri wa Fedha, Henry Rotich, uundaji na uboreshaji wa viwanda ulipokea mgao wa Sh125.4 bilioni.

Kenya pia ni miongoni mwa nchi zenye udongo na hali ya anga bora kufanya kilimo.

“Nchi hii huzalisha mazao mengi ya kilimo, wakulima wetu tukiwaonesha umuhimu wa kufungua viwanda vya kuongeza thamani (value addition) na serikali iwafadhili nafasi za ajira zitajitokeza,” anapendekeza Bw Nyoro.

Sekta ya kilimo ilipata kima cha Sh59.1 bilioni, katika makadirio ya bajeti 2019/2020.

Bi Beatrice Elachi, spika wa bunge la kaunti ya Nairobi ambaye madiwani walimwondoa na bado anashughulika hapa na pale kunusuru wadhifa huo, anasema kinachozima ari ya vijana kufungua biashara ni vikwazo vinavyowekwa na serikali.

Kiongozi huyu analalamikia zinavyotolewa leseni za kuweka biashara pamoja na kufungua kampuni na viwanda.

“Huyu kijana aliyejaaliwa uwezo wa kuunda bidhaa za juakali unapomuwekea vikwazo vya leseni na ada ya juu inayotozwa bila shaka hataweza kujiendeleza. Viwanda ni ubunifu wa kuunda bidhaa mbalimbali,” anaelezea Bi Elachi.

Tajiri kumnyonya maskini

Anasema mabwanyenye wenye uwezo kifedha ndio pekee wanaendelea kuimarika.

Elachi pia anaikosoa serikali kwa kutoza ushuru ghali mfanyabiashara mdogo ambaye anabembeleza biashara yake kukua.

“Serikali itathmini mfumo wa kutoza ushuru kwa kuwa wafanyabiashara wadogo ndio huchangia kuimarika kwa uchumi. Mazingira yao yakiendelea tunavyoona ni wazi uchumi utaendelea kidorora,” anaonya.

Anaendelea kueleza kwamba wafanyabiashara wadogo hawana mazingira bora kuendesha gange zao kwani baadhi ya maafisa wa halmashauri ya jiji wamekuwa wakiwahangaisha.

Baadhi ya wafanyabiashara wakuu nchini wanatuhumiwa kukwepa kulipa ushuru, kupitia mtandao wa maafisa katika halmashauri ya kutoza ushuru nchini KRA.

Ili serikali ya Jubilee ifanikishe ajenda ya ujenzi wa viwanda miaka mitatu iliyosalia, Michael Muriuki mtaalamu wa masuala ya kifedha na uchumi anahimiza serikali kukabiliana vilivyo na wanaohepa kulipa ushuru.

“Maendeleo yatafanyika serikali ikiwa na fedha, ukusanyaji ushuru ndio njia kuu kuyafanikisha. Kusiwe na yeyote anayekosa kulipa,” anasema Bw Muriuki.

Kukithiri kwa visa vya ufisadi na ubadhirifu wa mali ya umma ni kiini kikuu cha uchumi kuzorota.

Ni muhimu kutaja kuwa biashara zinazofanywa katika mazingira yaliyosheheni ufisadi matokeo yake huwa kufilisika.

Viwanda inavyonuwia kujenga serikali ya Jubilee itakuwa vigumu kuimarika kwa sababu ufisadi ni mithili ya virusi vinavyoua. Licha ya Rais Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga kuendesha kampeni dhidi ya ufisadi, sakata hazikosi kuripotiwa.

Hii ina maana Rais na kiongozi huyo wa upinzani, ambao mwaka uliopita walifanya salamu za maridhiano maarufu kama handisheki mojawapo ya ajenda ikiwa kuangamiza ufisadi, watalazimika kuimarisha mbinu kuukabili.