Habari Mseto

Uchangamfu KWS kutangaza mbuga kwa picha ya vifaru wakijamiiana

March 22nd, 2019 1 min read

Na PETER MBURU

SHIRIKA la Huduma kwa Wanyamapori (KWS) limewachangamsha Wakenya kwenye mitandao ya kijamii, baada ya kuchapisha picha ya vifaru wakijamiiana huku nyuma yake mazingira mazuri ya Jiji la Nairobi yakionekana.

Kwa lugha ya kuibua ucheshi, KWS ilikuwa ikiuza huduma zake kwa wateja, kuonyesha uhalisia wa mbuga ya Nairobi kama ya pekee duniani iliyoko ndani ya jiji, ndipo ikaamua picha zijizungumzie.

“Alasiri ya Jumatano itafanikiwaje bila mahaba kidogo? Sema kuhusu ngono na Jiji,” KWS ikasema kwenye mitandao yake ya kijamii. Maneno hayo yalifuatwa na picha ya vifaru wawili, mmoja akiwa juu ya mwingine ‘kingono’ katika mazingira ya nyasi za kijani, na nyuma kabisa majengo marefu ya Nairobi yakifurahisha macho.

Wakenya walichangamkia ujumbe huo wa KWS kwa haraka, wengi wakicheka, wengine kushangaa kuhusu ujumbe ambao hawakutarajia kutoka kwa shirika hilo na wengine bado kufurahia uzuri wa mbuga ya pekee ndani ya jiji duniani.

“Kweli hata wanyama wetu pia wanaielewa kazi. Lakini nani huyu yuko kazini leo?” akauliza mtumizi mmoja wa Twitter, huku akicheka.

Wakenya wengine, hata hivyo, walishangaa ikiwa ni maadili mema kwa shirika hilo kuchapisha picha na ujumbe wa aina hiyo.

“Aibu kwenu KWS, Kenya ni jamii ya maadili,” akasema mtaalam wa kiuchumi David Ndii.

Lakini hata ‘askari wa maadili nchini Dkt Ezekiel Mutua alifurahia mbinu ya shirika hilo kuuza huduma zao, akisema “?Wacha wanyama wajienjoy” huku akicheka.

Shirika hilo liliendelea kuwataka Wakenya na watu wengine kuzuru mbuga ya Nairobi na zingine kujionea zaidi.

“Msimamizi wa akaunti yetu ako tu sawa, tembeeni mbugani mtambue jinsi tunatunza wanyama na wanavyoendeleza vizazi,” KWS ikasema.

“Lakini tunatumai hili litawafanya kututembelea mbugani hivi karibuni. Hivyo, mtafahamu zaidi kuhusu vifaru,” likamaliza.