Jamvi La Siasa

Uchanganuzi: Ujio wa Djibouti unaweza kuharibia Raila hesabu za kushinda kiti AUC

April 11th, 2024 3 min read

Na CHARLES WASONGA

HATUA ya Djibouti kudhamini mgombeaji uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC) imeongeza kiunzi kingine kwa kiongozi wa upinzani Raila Odinga aliyeonekana kuelekea kupata ushindi kwa urahisi.

Kujitosa kwa Waziri wa Masuala ya Kigeni wa taifa hilo Ali Mahmoud Youssouf katika kinyang’anyiro hicho kumefikisha watatu wagombeaji kutoka eneo la Afrika Mashariki.

Mwingine ni aliyekuwa Waziri wa Masuala ya Kigeni wa Somalia Fawzia Yusuf Adam ambaye alijitangaza kama mgombeaji mnamo Februari 19, siku 14 baada ya Odinga kutanganza azma yake.

Lakini kujitosa kwa Djibouti katika kinyang’anyiro hicho kunaonekana kama tishio kwa Kenya ikizingatiwa nchi hiyo ndio mojawapo zile “zilizoisaliti” 2017 na kupelekea kushindwa kwa aliyekuwa Waziri wa Masuala ya Kigeni Amina Mohamed.

Bi Amina alishindwa na mwenyekiti wa sasa wa AUC, Moussa Faki Mahamat, kutoka Chad, aliyepata kura 38 katika uchaguzi ulioendeshwa kwa awamu saba ya upigaji kura.

Hii ni baada ya Djibouti, Uganda na Burundi, kubadilisha misimamo yao dakika za mwisho na kukataa kuipigia Kenya kura.

Kwa mfano, katika awamu ya kwanza nchi hizo tatu ukanda wa Afrika Mashariki ziliipigia Kenya kura na kumsaidia Bi Mohamed kupata kura 16 na huku Mahamat akipata kuta 14.

Kura zingine ziligawanywa kati ya Botswana na Equatorial Guinea.

Kanuni za uchaguzi wa AUC

Kulingana na kanuni za uchaguzi wa AUC, mshindi sharti apate angalau thuluthi mbili ya kura zote zitakazopigwa uchaguzini.

Lakini ilidaiwa kuwa ulegevu katika kuzishawishi nchi majirani zake na masuala ya jinsia na lugha yalichangia pakubwa kushindwa kwa Kenya.

Kwa mfano, aliyekuwa balozi wa Sudan Kusini nchini Ethiopia James Morgan alinukuliwa akisema kuwa Kenya ilifeli hata kushawishi baadhi ya washirika wake kutoka Afrika Mashariki kumpigia kura Amina.

“Sudan Kusini iliipigia kura lakini inashangaza kuwa Uganda, Burundi, Djibouti na Tanzania hazikuipigia Kenya wakati wa hatua za awamu. Tunadhani hii inatokana na uhusiano hasi wa Kenya na majirani zake. Burundi ilisema Kenya huingilia masuala yake ya ndani kwa kulaani mapigano huko,” Bw Morgan akasema.

“Uganda pia haifurahishwi na jinsi Kenya inataka kila kitu. Nilimwona Rais wa Uganda akijadiliana kwa kina na mwenzake wa Tanzania wakati wa awamu ya sita ya upigaji kura. Na katika awamu ya saba Tanzania haikupigia Kenya kura,” akaongeza.

Hii ni licha ya kwamba wakati wa kampeni, Bi Amina alisemekena kuungwa mkono na mataifa ya mashariki mwa Afrika. Ilitokea kuwa ahadi hiyo haikuzingatiwa debeni.

Kuhusu suala la jinsia, ilidaiwa kuwa baadhi ya nchi, haswa zile za Afrika Magharibi, zilihisi kuwa haikuwa haki kwa mwanamke mwingine kumrithi mwenyekiti aliyeondoka, Nkosazana Dlamini Zuma, ambaye ni mwanamke.

Kwa upande wake aliyekuwa Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa na Mbunge wa Garissa Mjini Aden Duale alilaumu mgawanyiko wa lugha.

Ziliungana nyuma ya Mahamat

“Nchi za Afrika Magharibi na Afrika ya Kati ambako Kifaransa huzungumzwa kwa wingi ziliungana nyuma ya Mahamat baada nchini nyingi kunakozungumzwa Kiingereza kujiondoa katika awamu za sita na saba za upigaji kura,” akaeleza.

Lakini akikubaliana na kauli ya Duale Elias Ntungwe Ngalame, ambaye ni mchanganuzi wa masuala ya AU, akisema Mahamat alikuwa chaguo bora kwa sababu aliwahi kuhudumia umoja huo kwa muda mrefu haswa katika shughuli za kuleta amani.

“Mwenyekiti mpya amewahi kushiriki katika mazungumzo ya amani nchini Sudan Kusini. Aidha, aliwahi kuisaidia AU kuunda mkakati wa kupambana na Boko Haram katika eneo la Ziwa Chad,” akaongeza.

Ni kwa msingi ya matukio katika uchaguzi huo wa AUC, uliofanyika Januari 31, 2017 ambapo wadadisi wanasema Rais William Ruto anayo kibarua cha kurekebisha makosa ya mtangulizi wake Uhuru Kenyatta ili kuhakikisha kuwa Bw Odinga anapata ushindi.

Uchaguzi ujao, utakaoshirikisha nchi 54 wanachama wa AU, umeratibiwa kufanyika mapema mwaka ujao, 2025.

“Rais Ruto sharti ahakikishe kuwa amerekebisha makosa ambayo mtangulizi wake, Uhuru Kenyatta, huenda alitenda na kuikosesha Kenya wadhifa huo wenye ushawishi mkubwa Afrika na ulimwengu kwa ujumla,” anasema Benson Ogutu, ambaye ni mtaalam wa masuala ya Diplomasia na Mahusiano ya Kitaifa.

“Kwanza kabisa, Ruto ahakikishe kuwa Bw Odinga amepata uungwaji mkono katika mataifa mengi katika maeneo manne makuu; Afrika Mashariki, Afrika Kaskazini, Afrika ya Kati, Afrika Magharibi na Afrika Kusini. Anahitaji kufadhili kampeni kali katika nchi hizo,” anaongeza Dkt Ogutu ambaye ni mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Kenyatta.

Wiki hii nchini za Angola na Guinea-Bissau zilielezea nia ya kumuunga mkono Bw Odinga.

Angola inafahamu suala

Balozi wa Angola nchini Sianga Abilio alisema hivi:

“Angola inafahamu kuhusu suala hilo (azma ya Odinga) na itaunga Kenya mkono kama ‘ndugu yetu’.

Alisema hayo katika ubalozi wa Angola jijini Nairobi wakati wa maadhimisho ya miaka 22 tangu kukomeshwa kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo.

Mataifa mengine ya hivi punde kuunga mkono Kenya ni Ghana na Guinea-Bissau ambako Rais Ruto alizuru wiki jana.

Mwezi wa Machi, Bw Odinga alivuna uungwaji mkono kutoka Uganda na Rwanda.

Dkt Ogutu anaishauri serikali ya Kenya kuhakikisha kuwa imeendeleza kampeni hizo bila kulegea “kusudi nchi zingine zisibadili misimamo hapo katikati au dakika za mwisho.”

Tayari serikali imebuni jopo la kuendesha kampeni za kumtafutia Bw Odinga kura kote Afrika.

Jopo hilo, linashirikisha wawakilisha kutoka wizara mbalimbali za serikali, linaongozwa na Mkuu wa Mawaziri na Waziri wa Masuala ya Kigeni Musalia Mudavadi.

Bw Odinga sio mgeni katika AU kwani amewahi kuhudumu kama Mwakilishi wake kuhusu Miundo Msingi Afrika.

Sawa na mwenyekiti anayeondoka (Mahamat), Bw Odinga amewahi kuongoza mazungumzo ya kuleta amani katika mataifa yenye misukosuko kama vile, Ivory Coast mnamo 2010.

[email protected]