Habari Mseto

Uchawi wazidi kanisani huku waumini wakiamini nguvu za giza kuliko Mola

March 21st, 2018 2 min read

Na MWANGI MUIRURI

WAUMINI wengi makanisani wanashiriki uchawi kuliko wanavyozingatia mafunzo ya kidini, Muungano wa Makanisa ya Kiprotestanti (KAPC) umedokeza.

Mwenyekiti wa KAPC, Askofu Peter Mburu aliambia kongamano la kuombea taifa linaloendelea katika uwanja wa Kasarani jijini Nairobi kuwa Wakristo wengi wamegeukia uchawi wakitafuta utajiri, vyeo na kinga maishani. Wengi wanaenda kanisani na kushiriki shughuli za kidini kama mazoea tu ama kulinda hadhi yao wasigunduliwe mienendo yao ya kisiri.

Askofu Mburu alikiri kuwa hata wahubiri wengi wametumbukia kwenye uchawi sawa na waumini wao. “Katika muungano wetu tumesimamisha kazi wahubiri 23 tangu Januari 2017 kwa kuwapata na makosa ya kushiriki ushirikina. Waumini wetu wengi wamekiri waziwazi kuwa wameenda kwa waganga kutafuta usaidizi kwa matatizo yao,” akasema.

Alieleza kuwa wanaoshiriki uchawi zaidi ni wafanyabiashara, wafanyakazi katika sekta ya umma na kibinafsi pamoja na wanasiasa. Wengine wanaotegemea waganga ni wanaotafuta kazi, wachumba na wanawake wanaotafuta nguvu za kutawala waume zao.

Padre Joseph Wamalwa wa Kanisa Katoliki Nairobi alisema idadi ya waumini wanaovaa hirizi imeongezeka wakitafuta kujikinga na mikosi ya kijamii, kiuchumi au kisiasa.

Padre Wamalwa alisema kuwa shirika la The Pew Research Center kutoka Amerika mwaka jana lilitoa ripoti ikionyesha kuwa Wakenya wengi huabudu sanamu, hutoa kafara, hushiriki ushirikina na pia kuamini maroho ya kuzimu.

“Ripoti hiyo inaonyesha kuwa Kenya imo mbele ya mataifa kama Demokrasia ya Congo, Ethiopia, Nigeria, Zambia na Rwanda katika kuamini ushirikina,” akasema.

Alisema kuwa robo ya Wakenya waliohojiwa, ambao ni waumini wa dini mbalimbali walikubali kuwa wanavaa hirizi na pia hutembelea wachawi maarufu.
Bw George Ongere, ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Center for Inquiry-Kenya, anasema wameandaa mikakati ya kuandaa warsha kote nchini kupambana na ushirikina.

Alisema mikakati hiyo imeanzishwa katika Chuo Kikuu cha Moi ambapo kikundi kiitwacho Moi Freethinkers kitashirikisha juhudi za kuhamasisha wananchi dhidi ya ushirikina na mila ambazo zimepitwa na wakati.

“Hatua kama hiyo inashirikishwa na kikundi kingine kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi ambapo tutawatumia wanafunzi wa vyuo vikuu,” akasema Bw Ongere . Aliongeza kuwa wameanzisha jarida liitwalo Skeptical Inquirer ambalo litatolewa bila malipo kwa wananchi kwa lengo la kuwashawishi kutupilia mbali ushirikina.

Padre Paul Kariuki wa Kanisa Katoliki alisema uchawi ni kinyume cha mafunzo ya Ukristo na ni sawa na uabudu shetani.

Naye Kasisi Paul Wanjohi wa Redeemed Gospel alisema kuwa wananchi wanapoteza pesa nyingi kwa wachawi ambao wamefurika katika kila pembe ya nchi na wanatangaza huduma zao waziwazi.