Habari Mseto

Ucheshi Twitter washukiwa kufika mahakamani wamelewa chakari

August 15th, 2019 2 min read

Na Mary Wangari

Mitandao ya kijamii ilizagaa ucheshi mnamo Alhamisi, Agosti 15, kufuatia kisa ambapo washukiwa sita walipoteza fahamu katika Mahakama ya Kibera kutokana na kinachodaiwa kuwa kulewa kupita kiasi.

Picha na video za washukiwa hao wakiwa wamelala chini wakiwa hawajijui hawajitambui kutokana na kuchapa mtindi kupindukia, zilienezwa mitandaoni na kuwavunja mbavu Wakenya mitandaoni.

Baadhi ya maafisa wa polisi walionekana wakijaribu kuwasaidia kusimama lakini washukiwa hao walikuwa walevi chakari na walizama katika ulimwengu mwingine kiasi kwamba hawangeweza kusikia chochote.

Kisa hicho kilivutia wengi mitandaoni huku Wakenya ambao kwa kawaida hawachelewi kutania kila tukio, wakijitosa kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter kwa jumbe za kuchekesha.

“Hawa itabidi wamekata rufaa jinsi walivyokata maji,” alitania Moredussy.

“Wataamka waanze afande kwani huku ni wapi,” alisema Januaryveryown.

“Maana halisi ya washukiwa walikuwa walevi chopi kiasi cha kushindwa kusimama ili kusomewa mashtaka dhidi yao,” naye George alisema.

“Hawa wamekunywa hadi exhibit,” alisema Arsenane

“Ni taifa lenye furaha linalopenda kuchapa mtindi. Hawajamsumbua mtu. Waache tu,” alisema Andie Entertainer. ‘Jaji pia anapaswa kulala chini,” alitania Toni Motanya.

Hata hivyo kuna baadhi ya Wakenya waliohisi washukiwa hao walibururwa kortini kwa kukosa hela za kutoa rushwa huku wakiishutumu serikali kwa masaibu yanayowatamausha raia kiasi cha kutojali tena.

“Huenda walipelekwa kortini kwa sababu hawangemudu hata Sh50 za kutoa hongo,” alisema Martin Ngugi.

“Walitenda uhalifu upi? Kuwa mlevi kupindukia ni hatia? Wana sheria tafadhali,” alihoji Joseh Keya

“Tangu lini ulevi ukawa hatia? Kwa nini polisi wa Kenya wsijishughulishe na mambo muhimu,” alishangaa Abu Daud.

Isitoshe, baadhi ya Wakenya waliwasuta maafisa wa polisi kwa kuwapeleka washukiwa kortini wakiwa katika hali hiyo ambayo ilikuwa bayana walhtaji usaidizi. Wengine pia walsihangaa ni wapi vijana hao walipotoa pombe.

“Wanaweza hata kufariki kirahisi. Wape maji na asilimia 50 ya dextrose wataanza kuongea baada ya dakika tano. Si kuwatupa sakafuni kama magunia jinsi hiyo. Kwa kutazama picha hiyo, hatuna utu ndani yetu,” alilalamika Lucy M.

“Badala ya kuwapekela kujibu mashtaka, mbona wasipelekwe katika vituo vya kurekebisha tabia,” alisaili Job Sammy.

“Swali ni, walitoa wapi pombe?” aliuliza Mwende.