Makala

UCHORAJI: Kijana Sifuma amebobea katika sanaa za maonyesho

May 13th, 2020 1 min read

Na MAGDALENE WANJA

KEVIN Sifuma, 26, ni msanii wa uchoraji wa kazi za sanaa za maonyesho yaani visual arts.

Anasema anategemea sana mawazo yanayojengeka akilini mwake anapofanya kazi yake ili matokeo yawe ni mchoro ambao watu watautazama na ukawa wenyewe unaleta maana fulani.

Kiufupi ni kwamba mchoraji huchora matukio akilini.

Sifuma anasema anatumia mtindo huu kupata michoro ya kuburudisha na kupitisha jumbe mbalimbali.

“Nilianza kuchora nikiwa katika shule ya upili kabla ya kujiunga na Chuo Kikuu cha Kenyatta ambako nilifanya kozi ya Sanaa ya Ubunifu yaani Fine Art and Design,” anasema Sifuma.

Sifuma anasema aina hii ya uchoraji humfanya kuridhika na pia humpa fursa ya kushughulisha akili yake ili apate mawazo na mitazamo mipya ya kumsaidia kuzalisha kazi ya kufana.

Mchoro wa kazi mojawapo ya sanaa za maonyesho. Picha/ Magdalene Wanja

Kupitia michoro hiyo anapitisha ujumbe wa matumaini wakati wa majanga kama vile ugonjwa wa Covid-19 na mambo mengineyo yanayoathiri jamii.

Sanaa hii ya ubunifu kutoka taswira inayojengeka akilini mwa msanii – imaginative – bado haijakuwa maarufu sana humu nchini.

Mchoro wa kazi mojawapo ya sanaa za maonyesho. Picha/ Magdalene Wanja

Michoro mbalimbali humuwezesha kupata riziki yake ya kila siku.

Sifuma utampata katika sehemu mbalimbali za maonyesho ya kazi za sanaa jijini Nairobi, hasa katika Junction Mall.

Pia anasema anatumia mitandao ya kijamii kupata wateja wake.

“Mimi hutumia sana mitandao ya kijamii kama vile Instagram na Twitter,” anaongeza.