Uchumi, sanaa na desturi za kabila la Wadigo uswahilini

Uchumi, sanaa na desturi za kabila la Wadigo uswahilini

NA HAWA ALI

Zaidi ya kuwa Wadigo wengi huishi katika katika Mkoa wa Tanga, hasa kwenye mji wa Tanga, wako Kenya wanakoishi upande wa Kusini wa mji wa Mombasa. Katika Kenya huhesabiwa kati ya Mijikenda. Lugha yao ni Kidigo.

Wadigo wanajishughulisha na kilimo cha mazao ya chakula na biashara hususan mahindi, mpunga, muhogo, mboga na matunda. Wanalima korosho kama zao kuu la biashara na pia minazi kwa ajili ya chakula na biashara.

Wadigo pia ni wafugaji wa ng’ombe, mbuzi na kuku. Wanawake wa Kidigo wana kipaji katika masuala ya sanaa za mikono na hutumia vipaji hivyo kusuka mikeka, majamvi na vikapu. Ili kuongeza kipato Wadigo hujihusisha pia na uvuvi, na biashara ndogo ndogo. Zamani. nyumba zao za asili zinaitwa Msonge.

Nyumba hizo zenye umbo la duara ni kubwa kwa wastani, hujegwa kwa miti na udongo na kuezekwa kwa nyasi.Nyumba hiyo huwa na vyumba viwili na sebule moja kwa ajili ya kulala wavulana.

Chumba cha wasichana hutumika pia kama jiko na kuwa katikati ya chumba cha wazazi na chumba cha wavulana ambacho pia hutumika kama sebule. Hata hivyo, Wadigo wamebadilisha mfumo wa maisha na hivi sasa wanajenga nyumba za kisasa zenye vyumba zaidi ya vitatu.Walikuwa na miiko mbalimbali inayowatofautisha na makabila mengine.

Kwa mfano, ikiwa kijana wa kiume amefanikiwa kujenga nyumba na kufariki kabla ya kuoa ni lazima kufanyike tambiko maalumu ili kuzuia balaa kwa vijana wengine.

Kabla ya kuzikwa anaingizwa kwenye nyumba yake mpya na kuombewa kasha kwenda kuzikwa.Ikiwa kijana huyo atafia mbali na kuzikwa mbali na nyumbani kwao basi nyumba yake itabomolewa na kujengwa upya.

Nyumba mpya inapokamilika kundi la vijana ambao wameoa huhamia huko kwa pamoja na iliaminika kuwa wakihamia mmoja mmoja watapatwa na balaa.

Hata hivyo, imani hiyo imemalizwa na kuenea kwa dini ya Kiislamu na dini ya Kikristo miongoni mwa jamii ya Wadigo. Pia walikuwa na miiko kuhusiana na mapishi na chakula. Wakati wa kupika ilikuwa mwiko kwa mwanamume kuingia jikoni na wakati wa kula wanawake hawakuruhusiwa kujumuika na waume zao.

Wanawake walikula wakiwa jikoni pamoja na watoto wao wa kike na wanaume walikaa sebuleni? pamoja na watoto wao wa kiume. Hata hivyo, mambo yamebadilika, siku hizi, baadhi ya wanaume huwasaidia wake zao kupika. Pia baadhi ya familia za Kidigo na watoto wao wa kike na wa kiume wanaweza kuchanganyika wakati wa kula.

Pia baba na mama wanaweza kukaa na kula pamoja na watoto wao. Kama ilivyo kwa makabila? mengine ya Kiafrika, Wadigo walikuwa na imani ya kipekee kabla ya kuingia dini ya Kikristo na? Kiislamu. Waliamini mizimu ya babu zao maarufu kwa jina la Madibwe au Adibwe.

Waliamini kuwa mtu akifa hubadilika na kuwa na nguvu ya kipekee inayoweza kulinda au kusumbua binadamu. Ili kuimarisha amani katika jamii mtawala wao maarufu kama Bandiwe alitenga siku maalumu ya kufanya tambiko la kuomba amani na baraka.

Wadigo walikuwa na desturi ya kugawana majukumu katika malezi ya vijana ambapo akinamama huwafundisha wasichana juu ya majukumu ya kutunza familia na wanaume waliwafundisha wavulana juu ya jukumu la kulinda? na kuongoza familia.

You can share this post!

Wilbaro ya Ruto imeshika kutu, Kieleweke wadai

LEONARD ONYANGO: Handisheki itakufa baada ya refarenda