Uchungu wa ‘lockdown’

Uchungu wa ‘lockdown’

Na BENSON MATHEKA

MARUFUKU ya kutotoka na kuingia katika Kaunti za Nairobi, Machakos, Kiambu, Nakuru na Kajiado kwa muda usiojulikana iliyotangazwa na Rais Uhuru Kenyatta mnamo Ijumaa, imeibua uchungu wa maisha magumu waliyopitia Wakenya mwaka jana nchi ilipofungwa pindi virusi vyla corona viliporipotiwa nchini.

Rais Kenyatta alifunga kaunti hizo tano akisema, zinachangia asilimia 70 ya maambukizi ya ugonjwa huo ambao unazidi kuongezeka nchini. Aliongeza muda wa kafyu katika kaunti hizo kutoka saa nne usiku hadi saa mbili usiku na akafunga baa na uuzaji wa pombe.

Rais pia alipiga marufuku uuzaji wa chakula katika mikahawa isipokuwa kwa wateja wa kununua na kuondoka na kufunga makanisa na misikiti.

Wakenya wanahofia kuwa hatua hizo zitaathiri shughuli zao za kiuchumi na maisha ya kila siku hata kabla ya kupata afueni kutokana na athari za nchi kufungwa mwaka jana.

Wataalamu wanasema, japo rais ana haki ya kuchukua hatua za kuzuia maambukizi, marufuku hiyo itatumbukiza maelfu ya wakazi wa mapato ya chini katika mateso makubwa.

Rais Kenyatta hakueleza hatua ambazo serikali imechukua kukinga wakazi wa kaunti hizo ambao wataathiriwa kiuchumi na marufuku hiyo ambayo itadumu kwa muda usiojulikana.

Nchi ilipofungwa 2020 serikali ilipunguza viwango vya kodi na benki zikawapa afueni walio na mikopo. Viwango vya kodi vilirejeshwa Januari na mashirika ya kifedha yakafuta afueni kwa walio na mikopo. Watu wengi waliokuwa ndani ya kaunti hizo tano walikwama kwa sababu hawakuwa na muda wa kujiandaa kuondoka. Wanafunzi wa vyuo vikuu walikosoa hatua ya serikali wakisema ingewapa muda wa saa 72 kujiandaa kusafiri. Baada ya Wakenya kulalamika, serikali kupitia Kanali (Mstaafu) Cyrus Oguna iltangaza afuaeni ya kuwaruhusu wanaotaka kuondoka eneo lililofungwa kufanya hivyo hadi leo. Hata hivyo, haikutangaza hatua ilizochukua kukinga watakaoathiriwa kiuchumi na marufuku hiyo.

Wamiliki na wahudumu wa magari ya uchukuzi wa umma wanalia kwamba watapata hasara zaidi kwa kupigwa marufuku kuingia kaunti hizo tano.

Wanasema kwamba, kaunti hizo tano ni kitovu cha uchumi wa nchi na marufuku hiyo imetonesha kovu la hasara wanayopata.

“Hili ni pigo kwetu kwa sababu bado tuko na mikopo tunayong’ang’a kulipa na hakuna afueni ambayo serikali ilitupatia,” alisema mmiliki wa matatu zinazohudumu kati ya Nairobi na Kitui kupitia Machakos.

“Tutafunga biashara na familia nyingi kuteseka,” asema.

Serikali ilipofunga nchi mwaka jana, biashara nyingi ziliporomoka, kampuni za biashara nyingi zikafungwa na kusababisha mamilioni ya watu kupoteza kazi.

Tayari kampuni za safari za ndege zimetangaza kuwa zitasimamisha huduma kuanzia kesho ishara kwamba huenda zikapunguza wafanyakazi.

Sekta ya utalii ambayo iliporomoka mwaka jana, itaathirika zaidi na marufuku hiyo ikizingatiwa kuwa wageni kutoka nje ya nchi hupitia uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) jijini Nairobi, kabla ya kusafiri maeneo tofauti ya kitalii nchini.

Rais Kenyatta alisema kwamba, wageni kutoka nje ya nchi hawataruhusiwa kutoka nje ya kaunti hizo tano alizofunga.

“Hii inamaanisha Watalii wanaotaka kutembelea mbuga za wanyama kama Masai Mara Kaunti ya Narok na Mlima Kenya kaunti ya Nyeri hawataweza kufanya hivyo. Hoteli zote katika maeneo hayo zitaathiriwa,” alisema mtaalamu wa uchumi Franc Oduor.

Wengi walifukuzwa nyumba kwa kushindwa kulipa kodi, mali ya wengi ikapigwa mnada waliposhindwa kulipa mikopo.

Wafanyakazi walionusurika kufutwa walipunguziwa mishahara na kuagizwa kuhudumu kutoka nyumbani. Wataalamu wanasema hii ilisababisha ongezeko la dhuluma za kinyumbani zilizochangiwa na matatizo ya kiuchumi.

You can share this post!

Wanachama wa chama tawala cha Zimbabwe wadungwa chanjo ya...

JAMVI: ODM imekoroga ngome yake kwa kumvua Malala wadhifa...