Habari Mseto

Uchungu wa manusura ndani ya jengo Ruai

March 18th, 2018 2 min read

Na BERNARDINE MUTANU

WATU wawili walikwama ndani ya vifusi vya jumba lililoporomoka Jumamosi asubuhi mtaani Ruai, jijini Nairobi kwa zaidi ya saa kumi.

Wakati tukienda mitamboni, watu hao walikuwa bado hawajaokolewa kutoka kwa mabaki ya jumba hilo la orofa nne huku walioponea wakiendelea kupata matibabu hospitalini.

Katibu katika Wizara ya Nyumba Bw Patrick Bucha alisema jumba lililobomoka lilikuwa limejengwa vibaya kwa sababu “lilijengwa upesi kwa sababu limo katika eneo lililotengewa upanuzi wa barabara na chini ya nyaya za stima.”

Alisema kuwa ubora wa vifaa vilivyotumiwa kujenga jumba hilo vilikuwa vya kutiliwa shaka. Pia, lilikuwa limejengwa juu ya udongo mweusi, ambao ni maarufu kwa kuhifadhi maji.

“Tunawaonya wenye majumba kuhakikisha kwamba wanahusisha wanakandarasi waliosajiliwa, wataalam na michoro ambayo imeidhinishwa na mashirika husika,” alisema Bw Bucha.

Hilo ni jumba la tatu kuripotiwa kubomoka katika muda wa wiki moja. Jumamosi, jumba la orofa lilibomoka Kariobangi na katikati mwa wiki jana, jumba lingine lilibomoka eneo la Juja.

Bw Bucha alisema Serikali imebomoa manyumba 3,000 yaliyokuwa yamejengwa chini ya mfumo wa kupitisha umeme na karibu na reli.

“Wiki hii, tulibomoa majumba 3,000 yaliyokuwa yamejengwa chini ya nyaya za stima na juu ya reli. Wiki ijayo tutaanzisha operesheni kali ya kubomoa majumba hatari. Ni vyema kwa wamiliki wake kuyabomoa kabla hatujafika,” alisema.

“Hatuwezi kuendelea kuua wananchi kwa sababu majumba yanabomoka, lazima tuchukue hatua kali dhidi ya wamiliki wa majumba hayo,” alisema, na kuongeza kuwa wizara yake itahakikisha kuwa imebuni sheria ambayo inatoa faini na adhabu kali wamiliki wa majumba kama hayo, wataalamu waliohusika katika ujenzi na wanakandarasi.

Mwakilishi wa wadi hiyo, ambaye pia ni Naibu Spika wa Bunge la Kaunti la Nairobi, alisema jumba hilo lilianza kujengwa miaka minane iliyopita lakini likakwama kwa muda.

Alisema mmiliki alionywa kulibomoa lakini akapuuza. Jumatano, lilianza kuonyesha nyufa, lakini mmiliki wake, ambaye hajatambulishwa akalifanyia ukarabati kabla ya kulipaka rangi maeneo yaliyokuwa yamebomoka.

Watu hao walikuwa ni pamoja na mhudumu wa kuitunza orofa hiyo, aliyepelekwa katika Hospitali ya Mama Lucy.

Mashirika ya uokoaji likiwemo lile la Msalaba Mwekundu, Serikali ya Kaunti ya Nairobi na Shirika la Kukabiliana na Majanga yalifika upesi kuwasaidia watu hao. Juhudi za kuwaokoa waathiriwa hao zilikuwa zikiendelea kufikia jana usiku.