Habari Mseto

Uchunguzi kuhusu mama aliyetupwa ndani miaka 10 kwa madai ya unajisi waanza

January 29th, 2019 1 min read

Na PETER MBURU

KIONGOZI wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji ameagiza uchunguzi kufanywa kufuatia habari za kituo cha runinga ya Inooro, kuhusu masaibu ya mwanamke anayedai kufungwa jela miaka kumi bila makosa.

Kwenye habari hizo, ambazo zimesambaa sana mitandaoni na kuibua ghadhabu miongoni mwa Wakenya, Bi Lydia Achieng’ anadai kuwa alihukumiwa kifungo cha miaka kumi gerezani kwa dai kuwa alimnajisi mtoto wa jirani yake, japo hakufanya hivyo, wala hakukuwa ushahidi wowote.

Bi Achieng alisema kuwa mtoto yatima ambaye alikuwa akimlea na kumsomesha (wa kike) alidaiwa kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mtoto mwenzake, ndipo mamake mvulana akaamua kumsingizia kuwa alimnajisi mvulana wake.

Hata hivyo, alieleza kituo hicho kuwa hata walipofika kortini, mama huyo alikiri kuwa alimsingizia n ahata afisa wa polisi aliyekuwa akichunguza kesi hiyo akaeleza korti kuwa hakupata ushahidi wowote.

Lakini kwa hatua ya kushangaza, korti iliendelea kumhukumu kifungo cha jela kwa miaka kumi, na sasa amehudumu kifungo hicho, akisalia na miezi michache tu.

“Wakati nilikuja hapa, nilichanganyikiwa, nikashindwa la kufanya, nikakata tamaa kabisa kwa maisha yangu,” akasema mfungwa huyo.

“Niliskia vibaya sana sana, hata sahii naskia vibaya kwa sababu nahudumu kifungo kwa kitu chenye sijui. Mimi ninafanya nini jela?”

Mwanamke huyo sasa amelilia haki, akisema kuwa kifungo bila hatia kilimharibia ujana wake, na kumrejesha nyuma kimaisha.

“Huyo mama ameniharibia maisha kwa kesi yenye hakuna, amenirudisha nyuma hata sijui. Usichana wangu wote umeishia jela. Hapa si mahali pazuri mtu kukuleta hapa,” akasema huku akilia.

Kufuatia habari hiyo, Bw Haji aliagiza uchunguzi wa mara moja ili kubaini kilichopelekea mwanamke huyo kufungwa na ikiwa kulikuwa na ushahidi.

“Kanda hii ya habari imetazamwa na DPP. Licha ya kuwa mfungwa alishtakiwa wakati polisi walikuwa wakishtaki kortini na kabla ya katiba ya 2010, DPP ameelekeza kuwa ifuatiliwe mara moja,” afisi yake, kupitia akaunti ya twitter ikasema.