Makala

Uchunguzi kuhusu mshukiwa wa mauaji ya Starlet Wahu wakamilika

January 17th, 2024 2 min read

NA SAMMY KIMATU

MAKACHERO waliokuwa wakipeleleza kesi kuhusu mshukiwa mkuu wa mauaji ya kikatili ya marehemu Starlet Wahu, Bw John Matara wamemaliza upepelezi wao.

Mkuu wa Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai kaunti ndogo ya Makadara, Martin Korongo, alisema kwamba walipewa siku 21 na mahakama ili kumaliza uchuguzi kabla ya kupeleka mshukiwa kortini.

Aliambia Taifa Leo kwamba mshukiwa anazuiliwa katika seli za kituo cha polisi cha Industrial Area.

Aliongeza kwamba anasubiri kupewa maagizo na mwelekeo kuhusu faili ya kesi dhidi ya Bw Matara.

“Kufikia sasa, tumefunga faili baada ya kukamilisha uchuguzi wetu kuhusu mshukiwa anayehusishwa na mauaji ya marehemu Wahu. Sasa ninasubiri kupewa mwelekeo na Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka ya Umma. Ikiwa hakutakuwa na mabadiliko, mshukiwa atafikishwa kortini kwa mashtaka ya mauaji,” Bw Korongo akasema Jumatano.

Vilevile, Bw Korongo aliwashauri vijana wa kike kujiepusha na kukimbilia kukutana na wageni na watu wasiowajua kwa mara ya kwanza wakiwa peke yao.

Alisema kwa kukaidi ushauri huo, ndio maana kuna ongezeko la visa vya wasichana wadogo kuuawa katika hoteli na maeneo mengine nchini.

“Natoa onyo kwa wasichana kwamba ni lazima wawe chonjo kwani kukutana na wanaume wasiowajua kwa mara ya kwanza ni hatari sana,” Bw Korongo akasema.

Wiki jana, Bw Matara alikiri kumdunga Wahu kisu mguuni lakini akadai kuwa hakumuua kama inavyoripotiwa kuwa alimdunga kifuani.

Aidha, Bw Korongo alisema alimsubiri mkuu wa polisi katika kitengo cha Jinai eneo la Ruiru ili kumkabidhi faili nyingine ambapo Bw Matara anahusishwa na kisa kingine kuhusu mwanamke mwingine aliyeibiwa pesa kimabavu.

Hata hivyo, katika hali hiyo aliambia wanahabari kwamba utaratibu ni kwamba sharti mkuu wa jinai atume ombi ndiposa akabidhiwe mshtakiwa ili kumfungulia mashtaka mapya kulingana na malalamishi katika kituo cha polisi ambako taarifa iliandikishwa.

Aliongeza kuwa katika tukio la pili, mshukiwa alikuwa amemwibia mwanamke hela zake kwa njia ya M-Pesa.

Alisema kufuatia kukamilika kwa uchuguzi, Matara atafunguliwa mashtaka ya kuua.

Alisema Bw Matara alikiri kwamba alikuwa ‘ameoa’ na kujaliwa mtoto mmoja lakini wakaachana na mke baada ya mzozo wa kinyumbani.

Mshukiwa aliangaziwa na Taifa Leo mapema Januari 2024 baada ya mauaji ya Bi Wahu katika chumba kimoja katika Papino Apartment eneo la South B.

Marehemu Starlet Wahu. PICHA | MAKTABA

Kulingana na mkuu wa Polisi katika kaunti ndogo ya Makadara, Bi Judith Nyongesa, siku ya kisanga cha South B, mwili wa Wahu ulipatikana sakafuni ukiwa umelowa damu nyingi na alama za kudungwa mwilini.

“Mwili ulikuwa na jeraha la kisu karibu na sikio la kushoto na pajani. Hakukuwa na majeraha mengine yaliyoonekana mwilini japo nguo za marehemu zilikuwa juu ya kiti cha Sofa,” Bi Nyongesa akasema.

Tukio hili liliripotiwa katika kituo cha polisi cha South B ambapo maafisa waliofika katika eneo la tukio walikumbana na mtiririko wa damu ulioashiria kutoka katika chumba cha kulala na ishara ya mapambano, kisu cha jikoni kilicholoa damu, kondomu, sindano zilizotumiwa, vifaa vya kupima maambukizi ya virusi vya Ukimwi na chupa ya mvinyo miongoni mwa vitu vya kibinafsi.
Polisi walimsaka Matara,34, baada ya kutoroka.

Alinaswa na polisi katika kukurukakara za matibabu katika hospitali ya Mbagathi na kukamatwa pamoja na rafikiye aliyekuwa akimsaidia kupewa huduma ya matibabu.

Kadhalika, makachero walipata nyumba alimokaa mshukiwa katika mtaa wa Kahawa West.

Polisi walisema walibaini katika nyumba aliyokodi kulikuwa na kitanda, nguo na kiti kimoja.

Ripoti za polisi zilionesha kwamba maafisa wa upelelezi wamepata ripoti nyingine kuhusu matukio mengine ya uhalifu katika eneo la Ngong na Kasarani yanayomlenga Bw Matara.

Haya hivyo, Bw Korongo alikitenga na matukio ya maeneo ya Ngong na Kasarani akisema hizo ni habari za mitandao ya kijamii ambazo hawezi kuzithibitisha.

[email protected]